Wednesday, March 5, 2008

Mtoto wa Kikwete ahusishwa na ufisadi

Na Saed Kubenea

MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete anafanya kazi katika kampuni iliyoshiriki kusajili kampuni ya Deep Green Finance Ltd., ambayo ilikwapua mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

MwanaHALISI linazo taarifa kwamba kampuni ya mawakili ya IMMA Advocates and Co. ya Dar es Salaam ndiyo ilisadia usajili wa Deep Green Finance Ltd iliyochota Sh. 8 bilioni kutoka BoT.

Hakuna maelezo yoyote yaliyowahi kutolewa kueleza kwa nini Deep Green Finance Limited ililipwa mabilioni hayo na BoT wakati wa uongozi wa gavana Daudi Billali ambaye Rais Jakaya Kikwete alifukuza kazi miezi miwili iliyopita.

Mtoto wa rais, ambaye anafanya kazi katika kampuni iliyosaidia kusajili Deep Green Finance Ltd., ni Ridhwani Kikwete.

Deep Green Finance Limited ilichota fedha hizo kati ya Septemba na Desemba 2005 wakati wa mchakato kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

IMMA inasimamia majina ya wamiliki wa kampuni hiyo ya mawakili ambao ni Protase Ishengoma, Lawrence Masha, Aloysius Mujulizi na Sadock Magai.

Mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha aliithibitishia MwanaHALISI kwamba ni mwanzilishi na mmiliki wa IMMA.

Hata hivyo aliharakisha kusema kwamba kwa sasa amekabidhi majukumu yake kwa wakurugenzi wake wengine baada ya kuchukua wadhifa serikalini.

“Ni kweli kwamba mimi ni mmoja wa wakurugenzi waanzilishi wa IMMA, lakini kwa sasa siko huko. Nimeacha kujishughulisha na shughuli za kampuni hiyo tangu mwaka 2005 nilipoingia serikalini,” alisema Masha.

Aidha, Masha alithibitisha pia kwamba kampuni ya IMMA ndiyo iliyosajili kampuni ya Deep Green Finance Limited na kwamba ni kweli kuwa inamwajiri Ridhwan.

Hata hivyo, Masha amesema mwenye nafasi nzuri zaidi ya kuzungumzia masuala ya IMMA hivi sasa ni mkurugenzi mwendeshaji, Protase Ishengoma.

Ridhwani alifanya kazi katika kampuni hiyo ya uwakili akiwa bado kwenye mafunzo mara baada ya kupata shahada yake ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa jina ameliambia MwanaHALISI, “Tuombe kusipatikane ushahidi wa moja kwa moja kati ya IMMA na mafisadi; vinginevyo hadhi ya rais wetu itaathirika vibaya sana.”

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, kipindi mabilioni ya shilingi yalipokwapuliwa na Deep Green Finance Limited iliyoanzishwa kwa msaada wa IMMA, Ridhwani alikuwa tayari anafanya kazi katika kampuni ya mawakili.

Masha amethibitisha kuwa Ridhwani bado anafanya kazi kwenye kampuni hiyo hadi sasa.

Ridhwani hakupatikana hadi tunakwenda mitamboni kujibu swali iwapo hana wasiwasi wa kufanya kazi katika kampuni inayotuhumiwa kuibia taifa.

Kuhusu vigezo vya kuajiriwa, Masha amesema Ridhiwani alitimiza vigezo vyote na kwamba ana sifa zinazohitajika.

Imefahamika pia kuwa Fatuma Karume, mtoto wa Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, anafanya kazi IMMA.

Ni katika kampuni ya IMMA pia rais aliteua wakili Aloysius Mujulizi, ambaye ni mmoja wa wanahisa, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Hivi karibuni kumekuwa na minong’ono na tuhuma za chichini kuhusu kampuni iliyosaidia kusajili Deep Green Finance Limited ambako mtoto wa rais anafanya kazi na ambako rais ameteua wakili kuwa jaji na wakili mwingine kuwa waziri.

Taarifa kutoka kwa Msajili wa Makampuni zinawataja watu wawili, Protase Ishengoma na Stella Ndikimi kuwa wakurugenzi waanzilishi wa Deep Green Finance Limited.

Ishengoma alithibitisha katika mahojiano yake na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu juzi Jumatatu, kwamba alishiriki kusajili Deep Green Finance Limited.

Kampuni ya Deep Green ilifilisiwa mwaka 2006, kabla ya kufikisha hata mwaka moja wa uhai wake, katika kile wachunguzi wa mambo wanasema, “baada ya kukidhi matakwa na matarajio yake.”

Hadi sasa haijafahamika Sh. 8 bilioni zilizochotwa zilichukuliwa ili zifanye kazi gani na wapi.

Wakili Ishengoma alikiri pia kuwa ni yeye aliyeteuliwa kuifilisi kampuni aliyoanzisha.

MwanaHALISI ina ushahidi wa malipo kutoka Deep Green Finance Limited kwenda IMMA ingawa haikufahamika ilikuwa kwa kazi gani; kama vile ambavyo malipo kutoka BoT kwenda Deep Green hayajapatiwa maelezo hadi sasa.

Taarifa za ukwapuaji mabilioni ya shilingi kutoka BoT ziliwahi kuanikwa na kundi la wanasiasa likiongozwa na Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa siku lilipotangaza “orodha ya mafisadi” kwenye viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaamn mwaka jana.

Kutopatikana maelezo halisi juu ya kazi ya Deep Green Finance Limited; maelezo kuhusu matumizi ya mabilioni yaliyochukuliwa benki na sababu za kufilisiwa haraka kwa kampuni hiyo, vinamweka mtoto wa rais karibu na lawama na tuhuma lukuki.

Shutuma na tuhuma, za chinichini na za wazi zinatokana na matukio makuu yafuatayo:

Kwanza, IMMA ndio walirahisisha usajili wa kampuni ya Deep Green Finance Limited iliyokwapua mabilioni ya shilingi kutoka benki kuu.

Pili, baadhi ya wakurugenzi wa IMMA ndio walikuwa waanzilishi wa Deep Green Finance Limited inayotuhumiwa kufanya ufisadi.

Tatu, kampuni ya mawakili waliohusika katika shughuli zinazotiliwa mashaka, ndiyo imepata “ngekewa” ya mawakili wake kuteuliwa, mmoja kuwa jaji na mwingine kuwa waziri.

Nne, ni kampuni hiyohiyo ambayo inamwajiri mtoto wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na mtoto wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hata kama malalamiko hayana msingi, mlolongo huo unastua watazamaji.

Deep Green inadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na makampuni ya Meremeta Gold Limited na Tangold Limited. Meremeta ambayo nayo imefilisiwa. Ndiyo ilikuwa ikiendesha mgodi wa dhahabu wa Buhemba ulioko mkoani Mara. Tangold ndiyo ilirithi mali za Meremeta.

Makampuni yote yalichota mabilioni ya shilingi nchini na kutokomea.

Deep Green Finance Limited ambayo wakurugenzi wake wote watatu wanatajwa kuwa raia wa nje, Mark Ross Weston (New Zealand), Anton Taljaard na Rudolph van Schalkwyk wa Afrika Kusini), ilichotewa fedha hizo katika kipindi ambacho taifa hili lilikuwa katika hekaheka za uchaguzi mkuu mwaka 2005.

Baada ya kujineemesha kwa mabilioni ya shilingi kutoka BoT, Deep Green Finance Limited iliamua, Aprili mwaka jana, kujifilisi na kuteua kampuni ya Protase Rwezahura Gervas Ishengoma (IMMA) kuwa mfilisi kuanzia Julai 27 mwaka jana.

Waziri Masha, mmoja wa wamiliki wa IMMA, aligombea ubunge mwaka 2005 katika jimbo la Nyamagana, mkoani Mwanza na kushinda. Rais alimteua kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kabla ya kumhamishia Wizara ya Mambo ya Ndani kwa nafasi ya unaibu wakati wa mlipuko wa kwanza wa sakata la Richmond.

Katika mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri ya hivi karibuni, ambapo Wizara ya Usalama wa Raia na ile ya Mambo ya Ndani ziliunganishwa kama zamani, Masha aliteuliwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.

Kama itathibitika kuwepo mahusiano ya kifisadi kati ya IMMA na Deep Green Finance Limited; wakati huohuo mtoto wa rais akiwa na ajira katika kampuni ambamo tayari rais ameteua mawakili kwa kazi za uwaziri na ujaji, hadhi ya rais inaweza kuwa mashakani.

Mwisho

2 comments:

Anonymous said...

excellent piece.

next question is, who are the clients of the big well connected law firms such as IMMA and Mkono? I'd be surprised if most investors in the natural resources and mining sectors do not have such firms on retainer. But facts would be stronger. And the ever decreasing circles of networks would be further revealed.

Anonymous said...

Hapo lazima mchezo mchafu umechezwa. Hiyo kampuni ya IMMA ipo kama njia ya kujipatia pesa kwa njia za ujanja ujanja. Mtoto wa Rais kuendelea kufanya kazi ujue kuna ulaji wa uhakika hivyo hna haja ya kufanya kazi kwingine kunapolipa zaidi ya IMMA. Yetu ni macho tutaona mwisho wake. Endelea kutupa habari KLH News!