Saturday, March 8, 2008

Watendaji MwanaHALISI wanatishwa

tanzania Daima, Machi 8,2008
MKURUGENZI na Mhariri Mtendaji wa gazeti la MwanaHALISI, Saed Kubenea, anaendelea kupata vitisho vya kuuawa kupitia simu yake ya mkononi, huku akishinikizwa kuacha kuandika habari.
Vitisho hivyo ameanza kuvipata siku 60 baada ya kukumbwa na mkasa wa kuvamiwa katika ofisi za gazeti hilo Mwananyamala na kwamba amepokea ujumbe zaidi ya mara 20 wenye vitisho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Kubenea alisema Machi 5, mwaka huu, saa 5:10 usiku, alipokea simu ambayo haikuonyesha namba iliyosema “Sali sala yako ya mwisho.”
Kubenea alisema, siku tano kabla ya kupigiwa simu hiyo, yaani Februari 29, saa 6:12 mchana, alipokea ujumbe wa simu uliosheheni matusi, lakini moja ya ujumbe aliousoma mbele ya waandishi wa habari ulisema: “Hivi wewe umekosa habari za kuandika magazetini eeh! Ss bac kama umechoka kuishi tutakuondoa duniani kuanzia ss.”
Akielezea vitisho hivyo, alisema si vidogo kwani vinaonyesha ni mwendelezo wa tukio lililomsababishia maumivu ya macho na kujeruhiwa kwa mshauri wa habari wa gazeti hilo, Ndimara Tegambwage.
Alisema, kabla ya kumwagiwa tindikali, alipokea vitisho kama hivyo na kukumbwa na matatizo ya kugongwa na gari, kuchomewa gari, kusutwa, kutukanwa na kutishiwa kuuawa kwa njia ya simu.
Kubenea alisema, taarifa za matukio yote hayo zipo kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana na kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema kwa kuwa jukumu la serikali ni kulinda wananchi.
“Polisi lazima watakuwa wanajua hawa watu wanaofanya vitendo hivi, haiwezekani kushindwa kuwatafuta… tumetoa vielelezo chungu nzima kwa vyombo vya usalama kuhusu namba na muda wa simu iliyopigwa wao kama wao sidhani kama watashindwa kufuatilia, basi waseme hawawezi kwenda katika kampuni za simu kufuatilia namba za hao wahalifu.
“Ninataka ninyi mjue kwamba watendaji wa MwanaHALISI wanafanyiwa hila kwa kutishiwa kuuawa, lakini pia wanawatisha na ninyi… wanatishia haki ya kukusanya na kusambaza habari, wanatishia uhuru wa wananchi kutoa mawazo, lakini pia wanavunja haki zetu za msingi na za katiba,” alieleza Kubenea.
Alisema, Rais Jakaya Kikwete alipokwenda kumuona hospitali ya Muhimbili alipokuwa amelazwa, aliwataka waandishi wa habari waendelee kuandika habari bila woga isipokuwa wachukue tahadhari ya maisha yao.
“Tulimwelewa Rais Kikwete kuwa yeye binafsi hawezi kufanya vitendo vya kihuni, lakini alijua kwamba kuna watu wenye ujasiri wa kufanya vitendo vichafu… hatuna shaka kwamba hao ambao rais alitaka tujihadhari nao ndio wanaoendelea kututishia na labda wanaendelea kuandaa mipango mikubwa ya kuteketeza maisha yetu,” alisema.
Naye mshauri wa gazeti hilo, Tegambwage alisema zaidi ya miaka 30 anaandika habari ila aliwataka waandishi wasitiliane mashaka kwani wataigawa taaluma iliyojengwa kwa muda mrefu.
“Fanyeni kazi, hudumieni wananchi lakini tusiwekeane vidole machoni tutaharibu taaluma yetu ambayo wakongwe waliijenga kwa muda mrefu,” alisema.
Awali, Januari 5, mwaka huu, Kubenea na Tegambwage walivamiwa na watu wenye kemikali na mapanga katika ofisi za gazeti hilo na kujeruhiwa, ambako Kubenea alimwagiwa kemikali hiyo machoni wakati Tegambwage alikatwa kwa panga mgongoni na kichwani.

2 comments:

Anonymous said...

wahalifu ni hatari na wanajulikana,lakini kazi mliyoianza muendelee kuifanya wapenda haki wapo pamoja nanyi,tunawaombea kwa Mungu,tutapigana,tutafunga na kusali kwa ajili ya taifa letu na kwa ajili yenu,sina shaka serikali,usalama wa taifa, polisi(mwema Na tibaigana)wanawwafahamu wahalifu hawa lkh hawachukui hatua sijui kwa nini,sababu wanazo wao,hawa hawana sifa ya kuliongoza taifa hili kwa sababu hawana thubutu na ni wanafiki.mwisho ni rahisi kumuangamiza mtu lkn ni vigumu kuhuwa changamoto mliyoianza Tanzania yenye neemayaja,msikate tamaa.

Anonymous said...

See Here or Here