Friday, April 10, 2009

ZITTO

ZITTO Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini ameomba radhi wananchi kutokana na kile alichoita, "msimamo usio sahihi" wa kuunga mkono Dowans. Taarifa kamili katika MwanaHALISI la wiki ijayo.

Saturday, February 7, 2009

Kikwete kumfukuza Masha


Kikwete kumfukuza Masha
• Ni kutokana na zabuni ya vitambulisho
• Adaiwa kumpotosha Waziri Mkuu Pinda

Na Saed Kubenea


RAIS Jakaya Kikwete huenda akalazimika kumtosa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kutokana na kashfa mbichi inayomkabili, MwanaHALISI limeelezwa.

Masha anadaiwa kuingilia isivyo halali mchakato wa kutafuta mzabuni katika mradi wenye thamani ya Sh. 200 bilioni.

Huu ni mradi mkubwa na wa aina yake serikalini wa kutengeneza Vitambulisho vya Taifa. Suala la vitambulisho vya uraia liko chini ya wizara ya mambo ya ndani.

“Kama serikali itakuwa makini na kutaka kulinda hadhi yake mbele ya taifa na dunia nzima, basi Masha hana kazi,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.

Masha anadaiwa kuingilia mchakato wa zabuni kwa kutoa siri za zabuni kabla ya Bodi ya Zabuni kumaliza kazi yake na kutetea mmoja wa waombaji.

Haijafahamika waziri Masha ana uhusiano gani na mwenye kampuni hiyo, lakini mawasiliano yake na Katibu Mkuu wa wizara yake, Bodi ya Zabuni na ikulu yanaonyesha “anatetea” kampuni ya Sagem Securite.

Zaidi ya waombaji 54 wa zabuni ni mmoja tu anayedai kutoridhika na ndiye Masha amebebea bango la kumtetea wakati hata mchakato wenyewe wa zabuni haujakamilika.

Katika dokezo lake kwa Katibu Mkuu wa wizara yake na katika barua kwa Katibu Mkuu Kiongozi (ikulu), Masha anapendekeza Bodi ya Zabuni iombe ushauri wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi serikalini (PPRA) wakati hilo halihusiki katika hatua hii ya mchakato.

Kwa hiyo, kama waziri, Masha anajaribu kuvunja sheria ya ununuzi ya mwaka 2004 inayoelekeza taratibu za kuchukua hadi kuhitaji maoni ya PPRA.

Utaratibu wa kwenda PPRA unahitaji kuwepo kwa upande ambao haukuridhika kati ya Katibu Mkuu, Bodi ya Zabuni au Kamati ya Ununuzi. Kwa hiyo Katibu Mkuu hana sababu ya kwenda PPRA kama alivyotaka waziri.

Masha anadai kupelekewa malalamiko na Sagem Securite, lakini taarifa zilizopo zinasema majibu ya matokeo ya mchakato wa kutafuta kampuni zitakazoendelea na hatua ya pili, hayajatangazwa na wala waombaji hawajapelekewa taarifa.

Hii ina maana mgombea anayelalamika kwa waziri, kama kweli ameishadondoka, amepata taarifa kwa njia isiyo sahihi na waziri anatumia njia isiyo halali kutetea aliyeko nje ya taratibu za mchakato.

Taarifa zinasema Waziri, hata alipopata malalamiko, hakuyapeleka kwenye Bodi, badala yake aliamua kwenda moja kwa moja kutetea mwombaji kwa kutaka kurejewa kwa hatua ambazo tayari zilikuwa zimepitwa.

Kuingilia shughuli za zabuni ambako waziri amefanya kunavunja Kifungu 33 cha Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2004 na kanuni zake kwani mamlaka aliyojaribu kutumia siyo yake bali ni ya Katibu Mkuu (Accounting Officer).

Hatua yake pia, ambayo inaonekana kumpendelea na kumpigania mwombaji mmoja, inakiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 na Kanuni 101(6) ya Taarifa ya Serikali (GN) Na. 97.

Kwa kuangalia mawasiliano ya waziri Masha kupelekewa malalamiko kwa waziri kunavunja vifungu 79-82 vya sheria ya ununuzi.

Kwa mujibu wa sheria, malalamiko sharti yapelekwe kwa Katibu Mkuu ndani ya muda wa siku 28; majibu yapatikane katika siku 30; kama mlalamikaji hakuridhika atakata rufaa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi.

Baada ya hapo mlalamikaji akiwa bado hajaridhika atakata rufaa kwa Mamlaka ya Rufaa ya Ununuzi na siyo kwa waziri.

Katika kutaka kujua zaidi juu ya mawasiliano ya Masha na ikulu, mwandishi wa habari hizi aliambiwa kuwa waziri huyo alimpotosha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kumweleza kuwa Katibu Mkuu wa wizara yake ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni. Ukweli ni kwamba Katibu Mkuu anateua mwenyekiti wa Bodi hiyo.

Barua ya Masha kwa waziri mkuu ambayo MwanaHALISI inayo nakala yake, iliandikwa 19 Desemba 2008 ikiwa na Kumb. Na. CAB.214/364/01/H/45.

Kwa kuangalia mwenendo wa mchakato wa zabuni ya Vitambulisho vya Taifa hadi sasa, unaelekea kuwa kama ule wa zabuni ya kufua umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya Richmond wa mwaka 2006.

Katika mchakato huo, kiongozi wa serikali wakati huo, Edward Lowassa anadaiwa kushinikiza mawazo yake ndiyo yakubaliwe na kukiuka sheria ya ununuzi ya umma, ushauri wa wataalam na maelekezo ya baraza la mawaziri, mambo ambayo yalimgharimu nafasi yake ya waziri mkuu.

Aidha, mawaziri wa nishati wa wakati huo ambao walifanya kazi ya “kuitangaza” Richmond kana kwamba ni maofisa wake wa uhusiano – Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujiuzulu.

Wakati wa mchakato wa mkataba wa umeme, Masha, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mbunge wa Nyamagana, alikuwa naibu waziri wa nishati na madini chini ya waziri Dk. Msabaha.

Kuingiliwa kwa mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya uraia kunaweza kusababisha taratibu kusimamishwa au kuanza upya; jambo ambalo litaiingiza serikali katika hasara kubwa.

Kwa zaidi ya miaka kumi sasa, kumekuwepo “wimbo” wa kutengeneza vitambulisho vya uraia nchini na wananchi wakafikia kuamini kuwa ni mradi wa “kutafutia fedha za wakubwa.”

Habari kutoka bungeni zinasema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge, imemwita waziri Masha ili kutaka kujua kinachoendelea kuhusu mchakato wa zabuni ya vitambulisho.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wilson Masilingi amesema, “Ni kweli. Kamati inataka kujua kama kweli amevunja taratibu za ununuzi.” Amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuona hoja binafsi ya Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa Karatu.

“Kama amevunja sheria na taratibu kama inavyoelezwa, tutachukua hatua. Hilo ndilo jukumu letu. Ni vizuri tukapata taarifa kutoka kwake kabla ya kuchukua hatua. Hatuwezi kumhukumu mtu bila kumsikiliza,” amesema Masilingi.

Alipoulizwa iwapo Kamati yake inamwita ili kumlinda, Masilingi alipaza sauti na kusema, “Hatumlindi Masha. Tunatekeleza wajibu wetu.”

Naye Dk. Slaa anatarajiwa kuwasilisha bungeni hoja binafsi akimtaka Masha ajiuzulu au serikali impumzishe kazi. Haijafamika hoja hiyo itawasilishwa lakini taarifa zinasema ni wiki hii.

Mwisho

Wednesday, February 4, 2009

Friday, January 23, 2009

BoT 'wizi mtupu'

Na Saed Kubenea
WIZI wa mabilioni ya shilingi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ulifanywa kwa baraka za serikali, MwanaHALISI limegundua.

Nyaraka za benki na Hazina ambazo nakala zake zimeifikia gazeti hili zinaonyesha ushirika usiokuwa wa kawaida katika kuwezesha uchotaji wa fedha za umma.

Ushirika huo unahusisha makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Company na benki ya Nedbank ya Afrika Kusini.

Kwa mfano, kile ambacho BoT inaonyesha kuwa ni hati za dhamana zilizouzwa kwa kampuni ya Tangold Limited, kimegundulika kuwa ni “hewa.”

Nyaraka zinaonyesha kuwa mwaka 2005 Tangold ilinunua hati za dhamana za Sh. 50 bilioni, lakini taarifa kutoka ndani ya BoT na Hazina zinaeleza kinyume chake.

Kwa mujibu wa taarifa Na. 001/2005 ya BoT, Tangold Limited ilinunua na kupewa hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. 25 bilioni, tarehe 1 Mei 2005. Hii ilikuwa Siku Kuu ya Wafanyakazi (Mei Dei) ambayo huwa ni siku ya mapumziko kwa ofisi zote za serikali.

Vilevile kwa taarifa Na. 002/2005 ya BoT, Tangold ilinunua na kupewa hati ya dhamana ya thamani ya Sh. 25 bilioni, tarehe hiyohiyo.

Kufuatana na masharti ya mkataba, Tangold ilipaswa kulipwa na serikali riba ya asilimia 10 kila mwaka, kwa mikataba yote miwili kwa kipindi cha miaka 10 hadi mwaka 2015.

Lakini kumbukumbu za BoT ambazo ni nadra sana kuonekana hata kwa wakaguzi zinaonyesha kuwa hakukuwa na mnada wala tangazo la serikali la kuuza dhamana ambako Tangold ilinunua dhamana hizo.

“Kwa utaratibu, dhamana za serikali hutangazwa rasmi kwa umma kupitia Gazeti la Serikali (Official Government Gazette) au hata kwenye vyombo vingine vya habari,” ameeleza ofisa mwandamizi wa BoT.

“Nakwambia kama kungekuwa na hati ya dhamana ambayo imenunuliwa na Tangold, ingetangazwa na kujulikana kwa umma. Haikuwepo,” amefafanua ofisa huyo.

Mbali na gazeti la serikali na vyombo vya habari, matangazo huweza pia kutolewa kupitia tovuti ya BoT ambayo ni www.bot-tz.org ambako imethibitishwa kwamba hakukuwa na matangazo kuhusu uuzaji dhamana hizo, ameeleza.

Kauli hizo na ukweli wa nyaraka vinathibitishwa na hali halisi ya Tangold kama ilivyoonyeshwa kwenye akaunti yake iliyoko mjini Port Luis, Mauritius.

Taarifa ya akaunti ya Tangold ya tarehe 31 Julai 2005 inaonyesha kiwa Tangold ilikuwa na amana ya kiasi cha dola za Marekani 996.75 tu.

Tangold ilipofungua akaunti yake Na. 04413136 katika benki ya Federal Trust mjini Port Louis, tarehe 31 Desemba 2004, iliweka dola 2,455.00. Kiasi hicho hakikuongezeka hadi 31 Julai 2005.

Aidha, hata kwenye akaunti yake nchini Tanzania, katika benki ya NBC, makao makuu, haikuwa na fedha za kununulia dhamana za serikali.

Fedha za kwanza kuingia akaunti ya Tangold hapa nchini zilikuwa Sh. 1.5 bilioni na ilikuwa 1 Agosti 2005. Fedha hizo zilitoka BoT na haikuelezwa ni kwa kazi ipi.

Siku hiyo hiyo zilihamishwa Sh. 1.5 bilioni kwenda kampuni ya Deep Green kutoka BoT vilevile kwa kazi ambayo haijaweza kugundulika.

Tangold ni moja ya makampuni yenye utata katika miliki na usajili wake. Wakati inaonyeshwa ilisajiliwa Mauritius na baadaye kufungua tawi Tanzania, serikali ilieleza bungeni kuwa ni kampuni yake kwa asilimia 100.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), wakurugenzi wa Tangold ni pamoja na Daudi Ballali, Gray Mgonja, Andrew Chenge, Patrick Rutabanzibwa na Vincent Mrisho.

Nayo Deep Green inaonyesha ilisajiliwa Tanzania mwaka 2005 na kwamba anwani yake ya usajili ni IMMA House, Kiwanja Na. 357 Barabara ya Umoja wa mataifa, Upanga Dar es Salaam.

IMMA ni kampuni ya mawakili Protase Ishengoma, Aloysius Mujulizi, Lawrance Masha na Sadock Magai ya Dar es Salaam. Hivi sasa Mujulizi ni jaji wa mahakama kuu na Masha ni waziri wa mambo ya ndani.

Gazeti hili liliwahi kufichua ukwapuaji wa Sh. 8 bilioni kutoka BoT uliofanywa na Deep Green, kati ya Septemba na Desemba 2005 (MwanaHALISI Na. 087). Haikuelezwa pia zilikuwa kwa shughuli ipi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Tangold inayodaiwa kuwa kampuni ya serikali, iliingia mkataba na Deep Green ambayo ni ya binafsi ambao uliipa Deep Green haki zote za mikataba yake na BoT na serikali.

Nyaraka za Tangold zinaiagiza serikali na BoT kutii mikataba yake na bila swali, na gavana Ballali na Katibu Mkuu Hazina Gray Mgonja wanakubaliana kutii.

Kwa mfano vifungu Na. 3 na 4(e) vya mkataba wa Tangold na Deep Green, vinafanya Tangold, ambayo inadaiwa kuwa mali ya serikali, kukosa kabisa maamuzi katika mkataba.

Hili linajidhirisha katika barua Na. PST/GEN/2005 ya 25 Mei 2005 kutoka Hazina kwenda Deep Green ikikubali masharti ya kutobadili lolote katika mikaba ya makampuni hayo.

Kwa mfano, BoT ilikubali kuwasilisha malipo yoyote, pamoja na kile kinachoitwa riba kwa dhamana hewa, katika akaunti Na. 011103024840 katika NBC makao makuu na akaunti nyingine ambazo Deep Green itaagiza.

“Tutalipa bila masharti yoyote kwetu, fedha zote zinazohitajika katika akaunti Na. 011103024840 au kama itakavyoelekezwa na Deep Green,” ilisema barua ya serikali.

Barua hiyo ina saini ya “mwenye mamlaka ya kusaini kwa niaba ya serikali” – Authorised Signatory for and on behalf of the government of the United Republic of Tanzania na nakala kupelekwa Tangold.

Ni hali hii ambayo inafanya wafuatiliaji wa masuala ya utawala wa fedha BoT kuwa na mawazo kuwa Deep Green ama ni ya Watanzania au wana ubia ndani yake.

Kufuatia serikali kujifunga kulipa katika akaunti za Deep Green, gavana Daudi Ballali aliagiza malipo ya Sh. 1, 546,778,770.92 (1.6 bilioni) yafanywe kwenye akaunti ya Tangold Na. 011103024840 iliyoko NBC makao makuu.

Katika maelekezo kwenye karatasi isiyo na tarehe wala saini (maofisa BoT wamethibitisha), Ballali anasema dhamana tayari imejikusanyia riba tangu 1 Mei 2005.

Mkanganyiko hapa ni kwamba Tangold haikuwa na fedha kwenye akaunti zake ndani na nje ya nchi. Ilikuwa haijasajiliwa Tanzania.

Aidha, siku inayotajwa kuwa Tangold tayari ina limbikizo la riba, ni siku hiyohiyo inayoonyeshwa kuwa ndipo kampuni hiyo ilifunga mkataba wa kununua dhamana!

Bila kujali kuwa Tangold haina dhamana, haijasajiliwa, haijawa na lundo la riba, wala fedha kwenye akaunti zake, gavana Ballali anaagiza kuwa fedha zinazobaki, zipelekwe akaunti Na. 011103024852.

Tangold, Deep Green na benki ya Nedbank wanatumia karatasi na anwani zilezile za mitaa na jengo mjini Sandton, Afrika Kusini nakupitia msemaji mmoja aliyetajwa kuwa Wayne Khoury katika Nedbank.

Gazeti lilijitahidi kumpata Bw. Khoury kwa baruapepe yake ili kujua uhusiano wake na taarifa za malipo. Hata hivyo hadi tunakwenda mitamboni baruapepe ilikuwa haijajibiwa. Simu yake haikujibu.

Nedbank, kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, ilitumika pia kupitisha malipo kwa ajili ya kampuni ya Meremeta, moja ya makampuni yanayodaiwa kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka BoT na serikalini.

Wiki iliyopita, gazeti hili liliripoti ukosefu wa kanuni za utoaji fedha katika akaunti ya EPA; udhaifu katika utendaji na wizi wa nyaraka za BoT.

Imefahamika kuwa gavana Ballali alikuwa akimwagiza meneja wa tawi la NBC makao maku, P.J. Mapunda kulipa mabilioni ya shilingi kwa Deep Green, Tangold na Meremeta.

Mwandishi alipotaka kupata maoni ya Bw. Mapunda kuhusu madai hayo, aliambiwa na maofisa wa NBC kuwa kuwa ameishafariki.

Gavana Ballali alifariki Mei mwaka jana katika mazingira yaliyoacha maswali mengi; baada ya serikali kuficha alipo kwa kipindi kirefu.

Thursday, January 15, 2009

Nyaraka EPA zaibwa
• Zimo za Kagoda, Deep Green
• Jinamizi lazidi kutanda BoT

Na Saed Kubenea

UWEZEKANO wa serikali na Benki Kuu (BoT) kufanikiwa kupata ushahidi wa kuwatia hatiani waliokwapua mabilioni ya shilingi ni mdogo kufuatia taarifa kuwa nyaraka muhimu zimeibwa.

Hata mafaili na taarifa nyingine juu ya kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyokwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni, zinaweza kupatikana tu kwa ngekewa, chanzo cha habari ndani ya BoT kimeeleza.

MwanaHALISI lina taarifa kuwa tangu mwaka 1996, wakati fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zilipoanza kuchotwa, hakukuwa na utaratibu maalum wa kuchukua fedha kutoka benki.

“Hakukuwa na utaratibu kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji fedha – Financial Management Manual. Zilikuwa zikitolewa tu. Wahusika walikuwa wakifanya wanavyotaka, kama kuandikiana vimemo,” kimeeleza chanzo cha habari hizi.

Utaratibu huu, kimeeleza chanzo cha habari, “haukubaliki katika taasisi za fedha na hautambuliki kimataifa. Ingejulikana hakuna kanuni za utawala wa fedha, benki ingepata aibu na shughuli zake kukataliwa.”

Ni katika mazingira haya kampuni ya Kagoda ilifanikiwa kuchukua fedha BoT na kuzipitisha katika matawi saba ya benki ya CRDB jijini Dar es Salaam kwa mtindo wa “kuingiza na kutoa papo hapo.”

Hadi sasa serikali haijasema nani anamiliki Kagoda, yuko wapi. Haifahamiki pia iwapo kuna yeyote aliyekamatwa kuhusiana na kampuni hiyo.

Haijafahamika pia iwapo Kagoda, yenye utata wa miliki na usajili, ni moja ya walioiba fedha BoT ambao walizirejesha kukidhi matakwa ya rais ili wasishitakiwe.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akichokonolewa na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, wakitaka kujua iwapo kweli Kagoda “imeiweka serikali mfukoni,” alisema “serikali haiogopi mtu yeyote. Hakuna wa kuigopesha. Tunafuatilia haya na tutatoa taarifa.”

Hadi sasa, mwanasiasa na mfanyabiashara mmoja, Rostam Aziz ndiye amekuwa akitajwa kuwa na uhusiano na Kagoda.

Kabla MwanaHALISI halijafungiwa, lilikuwa limeoanisha mawasiliano kati ya Kagoda na BoT yaliyoonyesha matumizi ya simu ya kampuni ya Caspian inayodaiwa kuwa mali ya Rostam Aziz.

Utoaji fedha kutoka akaunti ya EPA uliidhinishwa 30 Oktoba 1996 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Peter Ngumbullu.

Katika barua yake, Kumb. Na. TY/AG/BOT/INST/1/12, kwenda kwa gavana wa BoT, Dk. Idris Rashid, Ngumbullu alisema serikali imeagiza matumizi ya Sh. 100 bilioni kutoka akaunti ya EPA kila mwaka kwa kipindi cha miaka 50.

Utoaji holela wa fedha kwenye akaunti ya EPA – bila uhakiki wa wanaodai, viwango wanavyodai, mahali walipo na uhalali wa madai yao – uliendelea hadi mwaka 2007.

Taarifa za ndani ya BoT zinasema mwaka 2007 BoT ndipo walipotengeneza utaratibu wa dharura unaolingana na mwongozo wa utoaji fedha na kubuni nyaraka zinazoonyesha kulikuwa na utaratibu tangu 1997.

“Nakuhakikishia hakukuwa na nyaraka kati ya 1996 na 2007. Hii ni kwa kuwa hakukuwa na utaratibu. Kwa hiyo nyaraka zinazoonyeshwa ni za kughushi,” kimeeleza chanzo chetu.

MwanaHALISI iliongea na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu kutaka kujua iwapo nyaraka zinazotumiwa na benki hivi sasa na kipindi cha miaka 10 hadi 2007 zilikuwa za kughushi.

Akiongea taratibu, kwa njia ya simu, Profesa Ndullu alisema hana taarifa juu ya nyaraka za kughushi ndani ya benki na kwamba anaona ni zilezile.

Kuhusu nyaraka zilizoibwa alisema, “Sina taarifa hizo. Kama unasema kuna taarifa za aina hiyo, nitafuatilia ili kujua ukweli.”

Profesa Ndullu aliteuliwa na rais kuwa gavana wa BoT, Januari mwaka jana, baada ya uteuzi wa Daudi Ballali kutenguliwa. Ballali alikuwa gavana wa benki tangu 1997. Ballali alifariki dunia

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, hata baadhi ya nyaraka ndogo na chache zilizokuwepo na ambazo hazikidhi utaratibu wa utoaji fedha, zimetoweka “katika mazingira tatanishi.”

Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi walioongea na mwandishi wa habari hizi walisema ni maofisa wa BoT walioghushi nyaraka na kurudisha tarehe nyuma ili kuweza kuonyesha kuwa utaratibu ulibuniwa na kuanza kutumika tangu mwaka 1997.

Lengo la kufanya hivyo, lilikuwa kuzuia wakaguzi wa nje kugundua udhaifu wa miaka 10; kuridhisha wafadhili pamoja na wananchi waliokuwa wameshupalia taarifa za utawala wa fedha BoT.

Mtoa taarifa hizi alisema ni jambo linaloeleweka kwa viongozi waandamizi wa benki hiyo kuwa uwekaji nyaraka za kughushi ulilenga kufunika uhalifu na kulinda baadhi ya wahusika wakuu.

Makampuni 22 yalighushi majina na madai na kujichotea Sh. 133 bilioni kutoka akaunti ya EPA katika kipindi cha 2005 na 2006.

Mbali na makampuni 22 yaliyotajwa, kuna makampuni mengine yanayodaiwa kuchota zaidi ya Sh. 400 bilioni kutoka BoT kinyume cha taratibu.

Miongoni mwa makampuni hayo ni Tangold, Deep Green Finance Limited, Meremeta na Mwananchi Gold Ltd.

Fedha nyingi zilizoibwa BoT zilicukuliwa kati ya Julai na Desemba 2005 kipindi ambacho kilikuwa cha kampeni na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Habari za ndani ya BoT zinasema bila kuwa na utaratibu, Gavana wa wakati huo, Dk. Daud Ballali, aliendesha BoT kama chombo binafsi.

Taarifa zinasema ukiukaji wa taratibu ulishika kasi sana muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Hapa ndipo Ballali aliamua kutumia hata watendaji wa ngazi ya chini kuidhinisha malipo.

Imeelezwa kwamba Ballali alichukia sana kuona faili la Kagoda likikabidhiwa kwa maodita wa Ernst & Young waliokagua akaunti yaEPA. Baada ya hapo aliagiza utengenezaji wa kabati maalum kwa ajili ya kuhidashi nyaraka nyeti likiwemo faili la Kagoda.

Taarifa zinasema funguo za kabati la “mafaili nyeti” zilikabidhiwa kwa mmoja wa wafanyakazi wa BoT ambaye tayari yuko mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi kwenye akaunti ya EPA.

Hata hivyo, ukosefu wa utaratibu wa kutoa fedha akaunti ya EPA bado unaisumbua hadi leo. Kwa mfano, tarehe 25 Julai 2005 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja alimwandikia Katibu mkuu wa Hazina barua yenye Kumb. Na. EB/AG/40/01/49.

Katika barua hiyo, Mgonja aliruhusu BoT kutumia kiasi cha Sh. 66 bilioni tu ili kukamilisha kiasi cha Sh. 100 bilioni kinachoruhusiwa baada ya maombi ya benki hiyo.

Alikuwa akijibu barua Kumb. Na. DESED/60/48/VOL/VI ya tarehe 18/7/2005 ambamo BoT ilikuwa inasema tayari ziliishatumika Sh.34 bilioni; hivyo ilihitajika ruhusa ya serikali ili kupata Sh. 66 bilioni ili kufikia kiwango cha Sh.100 bilioni kilichoruhusiwa.

Katika hali inayoacha maswali megi bila majibu, Gavana Ballali, siku nne tu baada ya barua ya serekali, kupitia kwa Mgonja, iliyoruhusu matumizi ya Sh. 66 bilioni, aliandika barua ya kuikana barua ya awali iliyoandikwa na maofisa wake na kuomba ruhusa ya matumizi ya Sh. 80 bilioni juu ya hizo 66 bilioni.

Katika barua yake ya tarehe 29 Julai 2005 yenye Kumb. Na. DCSED/60/48/VOL.VI/101, Gavana Ballali anamkumbusha Mgonja mazungumzo yao kwenye simu. Anasema, “Kama tulivyoongea katika simu kuwa barua ya awali ilikuwa mkanganyiko mtupu.”

Ballali alimtaka Mgonja kuifuta barua hiyo ambayo kimsingi ndiyo iliyokuwa inafuata na kuzingatia utaratibu uliowekwa na serikali mwaka 1996.

Kwa mujibu wa barua hiyo Na. EB/AG/40/01/56 ya 9 Agosti 2005 Mgonja alifuta barua yake ya awali na kutoa ruhusa ya matumizi ya Sh. 80 bilioni bila kupata maelezo yoyote kuhusu fedha zinazodaiwa kuombwa kimakosa.

Utata wa matumizi ya fedha hizo ulikuwa bado unaendelea hadi mwaka jana ambapo Profesa Ndullu anafafanua masharti ya mwaka 1995 yanayohusu matumizi ya fedha kwenye akaunti ya EPA.

Katika barua hiyo Kumb. Na. A10/48 TEMP ya 28 Februari 2008, Professa Ndullu anamwambia Mgonja kuwa masharti ya mwaka 1995 hayaendani na mfumo wa viwango vya kimataifa vya kutoa ripoti za fedha – International Financial Accounting Reporting Standards (IFRS).

Lakini mtoa taarifa hizi anasema Ballali alikuwa na jeuri pia hata kataika mawasiliano na serikali. Mathalani, tarehe 8 Julai 2005 aliijibu serekali kwamba ni vigumu kutoa taarifa za matumizi ya fedha za EPA katika muda mwafaka kutokana na malipo kufanyika kwa maombi maalum na bila ratiba maalum.

Katika barua yake kwa katibu mkuu hazina, Kumb. Na. DCSED60/48/VOL.VI/IOI, Ballali alisema kompyuta za benki zilizohusika katika malipo zilikuwa zimeharibika na kwamba zitakapopona taarifa hizo zitafikishwa serekalini.

Mpaka sasa ni watuhumiwa wanne tu ambao wameshafikishwa mahakamani kwa upande wa BOT.

Mwisho

MwanaHALISI larejea mtaani



Gazeti la wananchi- MwanaHALISI limerejea tena mitaani baada ya kumaliza kile kilichoitwa na watawala, "Kifungo." Pata uhondo wake.

Thursday, January 8, 2009

Kubenea arejea nyumbani



Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mtendaji wa gazeti la MwanaHALISI, Saed Kubenea, amerejea nchini na anasema, "nimekuja kupambana na mafisadi."

Kubenea alikuwa nchini India katika hospitari ya Apollo alikokuwa anatibiwa macho kutokana na kumwagiwa tindikali baada ya kuvamiwa ofisini kwake 05 Januari 2008. Katika shambulio hilo, Kubenea alikuwa pamoja na mshauri wa kitaaluma wa gazeti hilo, Ndimara Tegambwage.