Wednesday, March 5, 2008

Mkulo tutajie mafisadi waliorejesha fedha za EPA

Na Mbasha Asenga

MATAIFA mengi duniani yanapambana na kitu kinachoitwa ‘utamaduni wa wahalifu kutoadhibiwa.’ Wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, lilizaliwa kundi lililohusishwa na kuendesha mauaji lakini wajumbe wake wakawa wanatembea bila ya kushughulikiwa kama wahalifu.

Kuishi kwao huru kama vile walifanya jambo la manufaa kwa taifa lao, kulifikia kikomo ilipoanzishwa mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Rwanda (ICTR) iliyoweka maskani yake Arusha, Tanzania. Hadi leo, wamekuwa wakisakwa ili wajibu mashitaka dhidi yao.

Utamaduni wa wahalifu kutoadhibiwa uko wa aina nyingi. Upo huu wa wazi kabisa wa watu walioshiriki mauaji, iwe ya kupanga au vinginevyo, kutoguswa. Upo mwingine ulio mbaya zaidi, wa kuwaenzi na kuwavumilia wezi, majambazi na wahalifu wengine waliopora rasilimali za taifa na kujilimbikizia ukwasi wa kutisha. Na hawa huonekana ni watu wa maana; wajanja. Hali hii ya kuenzi wezi na majambazi walipora mali ya umma bila uficho ni sawa kabisa na kujenga utamaduni wa kutokuadhibu wahalifu.

Nchini kwetu pana kashfa ya ufisadi uliofanywa katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi katika akaunti hiyo ulioendeshwa na kampuni ya Ernst & Young kwa mwaka 2005/2006, zaidi ya Sh 133 bilioni zimetafunwa na wajanja.

Makampuni 22 yametajwa kuhusika na utafunaji fedha hizo, yakiwemo ambayo hayana usajili unaofahamika. Hadi sasa, msimamo wa serikali kuhusu jambo hili ni wa wale waliohusika kurejesha fedha walizoiba.

Sambamba na hilo, Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa aliyekuwa gavana wa BoT, Daudi Ballali. Tunaelezwa kwamba uongozi mpya wa BoT umetakiwa kuchukua hatua zaidi za kiutawala dhidi ya watumishi wake waliosaidia kufanikiwa kwa wizi huo.

Wakati serikali ikichukua hatua hizo, kuna habari ambazo wiki iliyopita zilithibitishwa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, kwamba kiasi cha Sh 50 bilioni zimerejeshwa tayari kutokana na watuhumiwa. Waziri wa Fedha ametoa taarifa hiyo kwa ujumbe wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFM) uliokuwa nchini kwa ziara, akisema kwamba hatua hiyo ni mafanikio makubwa.

Sina nongwa na kiasi kilichorejeshwa hata kama kingekuwa ni nusu ya kilichotajwa. Hata watuhumiwa wangekuwa wamerejesha Sh 20 bilioni tu, ningesema bado hiyo ni hatua muhimu maana hapa tunazungumzia fedha za Watanzania.

Tatizo langu ni moja: Kwamba kumekuwa na usiri sana wa kuwataja hao waliorejesha fedha. Ndipo hapa panapoibuka ule utamaduni wa kutoadhibu watuhumiwa uhalifu. Hapa kuna fedha zilizoibwa, zimerejeshwa. Sasa siri ya nini katika kujua waliozirejesha? Hawatajwi kwa kuwa serikali inawaona ni watu wa heshima au vipi?

Ikumbukwe kwamba kwa muda mrefu maadili ya kupenda taifa yamepotea na utumishi wa umma umekuwa utumishi wa maslahi binafsi ya mtu. Siku hizi, mtumishi wa umma anayeiba na kufisidi nchi kama mtu anayekimbia kifo na kuishi maisha ya ukwasi asioweza kueleza alivyoupata amekuwa akisifiwa. Huyu askistaafu, anapongezwa, lakini mtumishi muadilifu akistaafu anazomewa na kung’ong’wa kwamba amejitakia umasikini.

Katika kudumisha utamaduni huu, sasa hatuthubutu hata kutaja waliorejesha fedha zetu ambao ni wale waliothibitishwa kuwa waliziiba kupitia makampuni yao.

Waziri wa Fedha anaogopa kuwataja hadharani kwa sababu katika fikra zake anaamini wamiliki wake ni watu wenye staha mbele ya jamii. Mkulo hataki kuyataja kwa sababu amelelewa na kutambua kwamba wezi wa mali ya umma ni mashujaa, ni watu wa kuenziwa, ni watu wa kutetemekewa.

Ndiyo maana nasema kinachofanyika sasa ni ufisadi ndani ya ufisadi. Kwamba viongozi wa serikali wanashindwa kuwafichua wahalifu walioiba fedha za umma. Nahisi kuna sababu mbili za udhaifu huu: Moja, labda si kweli kwamba kuna fedha zimerejeshwa bali kinachofanywa na serikali ni kuvungavunga tu katika mbinu za kupoza joto liliopo.

Au kama zimerejeshwa, wahusika hawatajwi kwa sababu serikali haikusudii kuwashitaki hawa. Ni kumaliza mambo ‘kishkaji’. Kwamba we bwana, maadamu umerejesha fedha zetu na wewe ni mtu wangu basi yaishie hapa tunakushukuru! Iwapo ndivyo hali ilivyo, ni nini basi kama si ufisadi ndani ya ufisadi?

Sote tu mashuhuda jinsi kibaka aliyeiba kuku au kukwapua mkufu wa dhahabu wa dada mrudi kazini, anavyokabiliwa na hukumu ya umma. Hapewi hata nafasi ya kujitetea kwamba labda ni njaa tu ya siku inamsumbua. Ni kipigo cha mbwa mwizi hadi kufa. Kibaka anahukumiwa mtaani si mahakamani.

Lakini mafisadi waliothubutu kutia mkono kisayansi ndani ya BoT na kuiba, wakachafua jina la taasisi na sifa ya taifa, wanaachiwa, wanafichwa. Kama hawafichwi au hawajaachiwa kishkaji na kama si danganya toto ni kweli fedha zetu zimerejeshwa, lazima Watanzania watajiwe watu hawa wakati wakisubiri hatua za kuwashitaki.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, amekuwa na staili hii ya kukwepa kutaja makampuni yaliyorejesha fedha. Tunajua kwamba ipo Kamati ya taasisi tatu iliyoundwa kufuatilia ugunduzi wa wakaguzi katika EPA, na Mwanasheria Mkuu yumo na ndiye kiongozi wao.

Wenzake ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema. Nao pia hawajasema lolote wala siwo waliosema fedha zimeanza kurejeshwa.
Ni vema watawala wakaelewa jambo moja, kwamba kadri hatua zaidi za kufuatilia ufisadi katika EPA zinavyozidi kufanywa siri, ndivyo imani ya wananchi kwa serikali yao inavyozidi kupungua.

Wananchi walikwishasema katika hadhira mbalimbali kuwa wangependa kuiona ripoti yote ya Ernst & Young; na waone hasa hatua madhubuti zinachukuliwa dhidi ya watuhumiwa wote walioiba fedha zao. Hawawezi kuvumilia serikali inayoendeleza utamaduni wa “kutoadhibu wahalifu.”
ends

1 comment:

Anonymous said...

hili suala mimi nilishakata tamaa,toka siku ya kwanza niliposikia Rais ametangaza Tume ambayo ina viongozi wa juu kabisa katika vyombo vya usalama.Lengo kubwa ni kuficha siri ambayo wote wanaijua kwamba fedha za EPA,ZILITUMIKA KATIKA UCHAGUZI na sio huu wa Kikwete, bali toka vyama vingi vianze CCM ndio walikuwa wanachota huko. Ndio maana hata mzee Mwinyi akasema muda ukifika atasema,kwani anaelewa kila kitu.jambo la kushangaza ni kwanini hayo makampuni ambayo yametajwa na kampuni ya ukaguzi yamechota mapesa yasipelekwe mahakamani? nilitegemea Rais baada ya kupata taarifa ya ukaguzi angewakabidhi Polisi ili WASHITAKIWE wote mahakamani.Sasa hivi wanatuambia pesa zinarudi kwa cheki wanashindwa kujua nani karudisha, je hizi cheki anasaini nani? wanadebiti Akaunti ya nani? basi watutajie hata hao wahasibu wanao saini tuwajue! kama cheki hazijulikani maana yake hata pesa huwezi kulipwa,maana ili ulipwe inabidi wewe mlipwaji ujaze pay slip uandike jina lako unaye lipwa,anayekulipa,na tawi lake!!!
HII NIDANGAYA TOTO PESA HAZIJARUDI,NA BWANA KUBENEA NIMESOMA LEO KWENYE GAZETI WAHARIRI MNAITWA,TUNAJUA MNAITWA KUNYAMAZISHWA, TUNASUBULI BAADA YA KIKAO HICHO MAMBO YA EPA YATAENDELEA???