Saturday, January 26, 2008

NAWASHUKURU WOTE





NAPENDA kuwafahamisha ndugu, marafiki na wote wanaopenda maendeleo na mafanikio ya gazeti la MwanaHALISI na yangu binafsi, kwamba nimerejea nchini kutoka New Delhi, India ambako nilikwenda kupata matibabu zaidi.

Matibabu yanafuatia shambulio kwa gazeti letu, kwangu mimi na kwa mshauri wetu, Ndimara Tegambwage. Mimi nilimwagiwa madawa machoni na ililazimu nipelekwe India kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Napenda kuwashukuru wote walioniombea kwa sala na dua. Nashukuru wote walionijulia hali wakati wote nilipokuwa hospitalini Muhimbili, hospitalini Apollo, nchini India na hata baada kurejea ya nyumbani.

Nawashukuru walionichangia hadi kufanikisha matibabu yangu. Wote nawapa shukurani za dhati.

Namshukuru sana balozi wa Tanzania nchini India, pamoja na maofisa wake kwa msaada na ushirikiano walionipa; na wote waliokuwa pamoja nami katika kuniuguza na kunifariji.

Pamoja na kwamba siwezi kuwataja kwa majina wote walionisaidia, lakini nitakuwa mkosefu wa fadhila, kutomtaja Ndimara Isaya Tegambwage.

Huyu ni mwanataaluma mahiri katika uandishi wa habari na uongozi. Huyu ni mwanamapinduzi na mwanaharakati wa kweli. Ni mchango wa Ndimara, kwa njia ya ushauri, uliolifikisha MwanaHALISI hapa lilipo sasa.

Kila mwandishi na kila mwalimu anaweza kuandika na hata kufundisha. Lakini ualimu na uandishi wa Ndimara umekuza vipaji vyetu na unaendelea kutuimarisha kila siku kama inavyodhihirika katika miezi sita iliyopita.

Nakiri kwamba kutoka kwa Ndimara, nimevuna ujasiri wa aina yake katika kushughulikia masuala mbalimbali na mazito ya taifa hili.

Jumamosi ya 5 Januari 2008, saa mbili na nusu usiku, wakati tulipovamiwa ofisini, Ndimara alinionyesha ujasiri mwingine nje ya taaluma. Alipambana na wavamizi wawili wakati mimi nikipambana na mmoja.

Mapambano yalidumu takribani kwa dakika tano huku Ndimara akijeruhiwa vibaya kwa panga kichwani na mgongoni na kumwagiwa aina ya tindikali ambayo hatujaelezwa ni ya aina gani.

Hadi sasa ninapoandika waraka huu, Ndimara amepata afueni tu; hajapona sawasawa. Mimi nilipigwa na kitu kizito pembeni mwa jicho la kulia na kumwagiwa tindikali machoni. Hii iliniathiri kwa kiasi kikubwa.

Nimepata matibabu nchini na nje ya nchi na sasa nimerejea nyumbani. Nashukuru mungu kwamba nimerejea salama na naweza kuona japo kwa kutumia miwani.

Kama alivyosema Ndimara katika makala yake ya wiki iliyopita, “Najiridhisha kuwa sura zile; maumbile yale; umri ule ni vya watu wa kutumwa, lakini kigazeti hiki kidogo...hakijawahi kuwasakama wala kuwasaliti watu wa aina ile.”

Sina mashaka yoyote katika kusema kwamba wavamizi wale walitumwa kutuvamia: wahariri na wachapishaji wa MwanaHALISI kwa lengo moja la kutuua na kuua gazeti.

Tangu kuanzishwa kwake, MwanaHALISI limekuwa gazeti la wananchi; limekuwa nao na haikutarajiwa kwamba, miongoni mwa wananchi, watapatikana wachache wa kukubali kutumika kuharibu kazi inayofanywa na gazeti hili.

Hadi sasa, bado najiuliza, watu hawa wametumwa na nani? Sipati jibu. Lakini ni dhahiri wametumwa. Hata hivyo, nafarijika kwamba kazi tunayofanya inasemwa na wengi kuwa ni nzuri, ingawa ni kweli kwamba wapo wachache wanaochukizwa nayo.

Napenda kuwafahamisha kwamba nimerejea nyumbani na nguvu na moyo wa ujasiri kuliko nilivyokuwa kabla ya tukio hili. Kwetu sasa, ndio kumekucha.

Pamoja na kwamba visa na vitimbi dhidi yangu na gazeti kwa ujumla havikuanza jana, na inawezekana vikaendelea huko tuendako, lakini bado nathubutu kusema kwamba tumeweza kufikisha ujumbe kule unakohitajika. Tutaendelea na kazi hiyo

(Saed Kubenea ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers, wachapishaji wa magazeti ya MwahaHALISI na MSETO).

1 comment:

Anonymous said...

pole sana kaka pamoja na yote umeonyesha umahiri na ujasiri mkubwa wa kutoogopa hawa mafisadi, pole sana kaka angalia sana majamaaa hawa si watu wema sana.