Saturday, January 26, 2008

RICHMOND: VIGOGO KUUMBUKA


MwanaHALISI Januari 23- 29, 2008.


VIONGOZI wa ngazi ya juu serikalini wanahaha kutafuta ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kuzalisha umeme uliosainiwa na serikali na kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC) kabla ya kuwasilishwa bungeni, MwanaHALISI limegundua.

“Kuna kiwewe; karibu kila mmoja anataka kujua kilichomo ndani ya ripoti kabla ya bunge kuanza kikao chake. Viongozi kadhaa wanahisi vikaratasi walivyokuwa wakitumia kuelekeza Richmond ipewe mkataba, vitakuwa vimegundulika,” zimeeleza taarifa rasmi.

Katika mkutano wake wa Novemba mwaka jana, Bunge liliunda kamati maalum ya kuchunguza mkataba wa Richmond kufuatia malalamiko, lawama na tuhuma dhidi ya kampuni hiyo iliyoshindwa kuzalisha umeme wa dharula kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Kamati hiyo ambayo iliongozwa na mbunge wa Kyera (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe, ilikabidhi ripoti yake 2 Januari, mwaka huu kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta na inatarajiwa kujadiliwa na bunge katika mkutano wake unaoanza tarehe 29 mwezi huu.

Vyanzo vyetu vya habari vinasema viongozi wa ngazi ya juu wanatumia baadhi ya wabunge na maofisa wa serikali kupata ripoti kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati Teule ya Mwakyembe.

“Tunaoona wanahangaika kupata taarifa ni wabunge na viongozi waandamizi katika Idara ya Usalama wa Taifa.

Angalau wabunge watatu akiwemo mbunge wa Viti Maalum (CCM) na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, ni miongoni mwa watu waliotajwa kuhusika na juhudi za kusaka ripoti kwa niaba ya vigogo serikalini.

Imeelezwa kwamba dhamira ya kutaka kuvujisha taarifa hizo ni kujaribu kuziba mazingira yanayoweza kuwatokomeza kisiasa baadhi ya vigogo wakubwa ndani ya serikali.

Gazeti hili lina orodha ya wabunge na maofisa wanaotumiwa kusaka ripoti hiyo lakini hawakuweza kupatikana kutoa maoni yao juu ya kuhusika kwao katika fukuto hilo.

Habari za kibalozi ambazo zinafanana na zile za bunge zinasema kutakuwa na patashika kubwa bungeni wakati ripoti hiyo itakapowasilishwa kwa ajili ya kujadiliwa.

“Vikaratasi (memo) kutoka kwa wakubwa, vikielekeza watendaji kuipendelea Richmond wakati wa mchakato wa kupata kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura, vimenaswa na kuwekwa kama viambatisho,” taarifa za kibalozi zimeeleza.

MwanaHALISI limefahamishwa na ofisa mmoja wa ngazi ya juu katika ofisi moja ya kibalozi jijini Dar es Salaam, kwamba ripoti inaweza kuwa mwisho wa harakati za kisiasa za baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu serikalini ambao wanaonekana kuhusika moja kwa moja na upendeleo kwa Richmond.

Licha ya viongozi waliokuwa wakielekeza kwa vimemo, kuna wale ambao walinyamazia taratibu zisizofaa na kukiuka kanuni za kupata mzabuni anayestahili. Nao wanaanikwa, taarifa zinasema.

Baadhi ya viongozi wanatuhumiwa moja kwa moja kuhusika na “uvunjaji utaratibu wa tenda uliowekwa na Bodi ya Tenda ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwa manufaa yake binafsi.”

Angalau wajumbe watatu wa Kamati Teule kuhusu Richmond, wamelalamikia kupigiwa simu na wabunge na maofisa wa serikali wakitaka wawape ripoti kabla haijajadiliwa bungeni.

Hoja ya Richmond imekuwa ikipigwa danadana bungeni hadi pale ilipoundiwa Kamati teule; na Waziri Mkuu Edward Lowassa aliwahi kuwaambia wananchi kuacha kujadili Richmond kwa kuwa mabwawa ya kusukuma maji ya kuzalisha umeme yalikuwa yamejaa maji.

Hata hivyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilijitwisha mgogoro huo na kutoka na kauli kwamba “serikali haikupata hasara yoyote kutokana na Richmond kushindwa kuzalisha umeme.”

Kauli hiyo na wasiwasi wa viongozi serikalini ndivyo vilizidisha shauku ya kutaka kujua nani alitoa zabuni kwa Richmond, uwezo wa kampuni na kwa nini ilishindwa kutekeleza mkataba.

Mwenyekiti wa Kamati teule ya Bunge iliyofanya uchunguzi, Harrison Mwakyembe alikataa katakata kujadili lolote jana alipotakiwa kueleza chochote anachojua juu ya wanaosaka ripoti ya kamati yake.

Naye injinia Stella Manyanya, aliyekuwa makamu wa Dk. Mwakyembe, hakupatikana kutoa maoni juu ya suala hilo.

Kampuni ya Richmond ilipewa zabuni ya kuzalisha megawati 100 za umeme wa kutumika wakati taifa lilipokabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme kutokana na ukame uliosababisha mabwawa ya maji yanayotumika kuzalisha umeme kukauka.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilishindwa kutekeleza mkataba huo wa gharama ya Sh. 172 milioni na matokeo yake iliuza kazi hiyo kwa kampuni iliyoitwa Dowans, ambayo ilifanikiwa kuzalisha umeme baada ya muda uliowekwa na mkataba kupita.

Mazingira ya uuzaji wa kazi hiyo kwa Dowans, yenyewe yalizidisha shaka huku yakiwepo maoni kuwa huenda kampuni hiyo ina uhusiano wa kikazi na Richmond.

No comments: