Friday, January 23, 2009

BoT 'wizi mtupu'

Na Saed Kubenea
WIZI wa mabilioni ya shilingi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ulifanywa kwa baraka za serikali, MwanaHALISI limegundua.

Nyaraka za benki na Hazina ambazo nakala zake zimeifikia gazeti hili zinaonyesha ushirika usiokuwa wa kawaida katika kuwezesha uchotaji wa fedha za umma.

Ushirika huo unahusisha makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Company na benki ya Nedbank ya Afrika Kusini.

Kwa mfano, kile ambacho BoT inaonyesha kuwa ni hati za dhamana zilizouzwa kwa kampuni ya Tangold Limited, kimegundulika kuwa ni “hewa.”

Nyaraka zinaonyesha kuwa mwaka 2005 Tangold ilinunua hati za dhamana za Sh. 50 bilioni, lakini taarifa kutoka ndani ya BoT na Hazina zinaeleza kinyume chake.

Kwa mujibu wa taarifa Na. 001/2005 ya BoT, Tangold Limited ilinunua na kupewa hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. 25 bilioni, tarehe 1 Mei 2005. Hii ilikuwa Siku Kuu ya Wafanyakazi (Mei Dei) ambayo huwa ni siku ya mapumziko kwa ofisi zote za serikali.

Vilevile kwa taarifa Na. 002/2005 ya BoT, Tangold ilinunua na kupewa hati ya dhamana ya thamani ya Sh. 25 bilioni, tarehe hiyohiyo.

Kufuatana na masharti ya mkataba, Tangold ilipaswa kulipwa na serikali riba ya asilimia 10 kila mwaka, kwa mikataba yote miwili kwa kipindi cha miaka 10 hadi mwaka 2015.

Lakini kumbukumbu za BoT ambazo ni nadra sana kuonekana hata kwa wakaguzi zinaonyesha kuwa hakukuwa na mnada wala tangazo la serikali la kuuza dhamana ambako Tangold ilinunua dhamana hizo.

“Kwa utaratibu, dhamana za serikali hutangazwa rasmi kwa umma kupitia Gazeti la Serikali (Official Government Gazette) au hata kwenye vyombo vingine vya habari,” ameeleza ofisa mwandamizi wa BoT.

“Nakwambia kama kungekuwa na hati ya dhamana ambayo imenunuliwa na Tangold, ingetangazwa na kujulikana kwa umma. Haikuwepo,” amefafanua ofisa huyo.

Mbali na gazeti la serikali na vyombo vya habari, matangazo huweza pia kutolewa kupitia tovuti ya BoT ambayo ni www.bot-tz.org ambako imethibitishwa kwamba hakukuwa na matangazo kuhusu uuzaji dhamana hizo, ameeleza.

Kauli hizo na ukweli wa nyaraka vinathibitishwa na hali halisi ya Tangold kama ilivyoonyeshwa kwenye akaunti yake iliyoko mjini Port Luis, Mauritius.

Taarifa ya akaunti ya Tangold ya tarehe 31 Julai 2005 inaonyesha kiwa Tangold ilikuwa na amana ya kiasi cha dola za Marekani 996.75 tu.

Tangold ilipofungua akaunti yake Na. 04413136 katika benki ya Federal Trust mjini Port Louis, tarehe 31 Desemba 2004, iliweka dola 2,455.00. Kiasi hicho hakikuongezeka hadi 31 Julai 2005.

Aidha, hata kwenye akaunti yake nchini Tanzania, katika benki ya NBC, makao makuu, haikuwa na fedha za kununulia dhamana za serikali.

Fedha za kwanza kuingia akaunti ya Tangold hapa nchini zilikuwa Sh. 1.5 bilioni na ilikuwa 1 Agosti 2005. Fedha hizo zilitoka BoT na haikuelezwa ni kwa kazi ipi.

Siku hiyo hiyo zilihamishwa Sh. 1.5 bilioni kwenda kampuni ya Deep Green kutoka BoT vilevile kwa kazi ambayo haijaweza kugundulika.

Tangold ni moja ya makampuni yenye utata katika miliki na usajili wake. Wakati inaonyeshwa ilisajiliwa Mauritius na baadaye kufungua tawi Tanzania, serikali ilieleza bungeni kuwa ni kampuni yake kwa asilimia 100.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), wakurugenzi wa Tangold ni pamoja na Daudi Ballali, Gray Mgonja, Andrew Chenge, Patrick Rutabanzibwa na Vincent Mrisho.

Nayo Deep Green inaonyesha ilisajiliwa Tanzania mwaka 2005 na kwamba anwani yake ya usajili ni IMMA House, Kiwanja Na. 357 Barabara ya Umoja wa mataifa, Upanga Dar es Salaam.

IMMA ni kampuni ya mawakili Protase Ishengoma, Aloysius Mujulizi, Lawrance Masha na Sadock Magai ya Dar es Salaam. Hivi sasa Mujulizi ni jaji wa mahakama kuu na Masha ni waziri wa mambo ya ndani.

Gazeti hili liliwahi kufichua ukwapuaji wa Sh. 8 bilioni kutoka BoT uliofanywa na Deep Green, kati ya Septemba na Desemba 2005 (MwanaHALISI Na. 087). Haikuelezwa pia zilikuwa kwa shughuli ipi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Tangold inayodaiwa kuwa kampuni ya serikali, iliingia mkataba na Deep Green ambayo ni ya binafsi ambao uliipa Deep Green haki zote za mikataba yake na BoT na serikali.

Nyaraka za Tangold zinaiagiza serikali na BoT kutii mikataba yake na bila swali, na gavana Ballali na Katibu Mkuu Hazina Gray Mgonja wanakubaliana kutii.

Kwa mfano vifungu Na. 3 na 4(e) vya mkataba wa Tangold na Deep Green, vinafanya Tangold, ambayo inadaiwa kuwa mali ya serikali, kukosa kabisa maamuzi katika mkataba.

Hili linajidhirisha katika barua Na. PST/GEN/2005 ya 25 Mei 2005 kutoka Hazina kwenda Deep Green ikikubali masharti ya kutobadili lolote katika mikaba ya makampuni hayo.

Kwa mfano, BoT ilikubali kuwasilisha malipo yoyote, pamoja na kile kinachoitwa riba kwa dhamana hewa, katika akaunti Na. 011103024840 katika NBC makao makuu na akaunti nyingine ambazo Deep Green itaagiza.

“Tutalipa bila masharti yoyote kwetu, fedha zote zinazohitajika katika akaunti Na. 011103024840 au kama itakavyoelekezwa na Deep Green,” ilisema barua ya serikali.

Barua hiyo ina saini ya “mwenye mamlaka ya kusaini kwa niaba ya serikali” – Authorised Signatory for and on behalf of the government of the United Republic of Tanzania na nakala kupelekwa Tangold.

Ni hali hii ambayo inafanya wafuatiliaji wa masuala ya utawala wa fedha BoT kuwa na mawazo kuwa Deep Green ama ni ya Watanzania au wana ubia ndani yake.

Kufuatia serikali kujifunga kulipa katika akaunti za Deep Green, gavana Daudi Ballali aliagiza malipo ya Sh. 1, 546,778,770.92 (1.6 bilioni) yafanywe kwenye akaunti ya Tangold Na. 011103024840 iliyoko NBC makao makuu.

Katika maelekezo kwenye karatasi isiyo na tarehe wala saini (maofisa BoT wamethibitisha), Ballali anasema dhamana tayari imejikusanyia riba tangu 1 Mei 2005.

Mkanganyiko hapa ni kwamba Tangold haikuwa na fedha kwenye akaunti zake ndani na nje ya nchi. Ilikuwa haijasajiliwa Tanzania.

Aidha, siku inayotajwa kuwa Tangold tayari ina limbikizo la riba, ni siku hiyohiyo inayoonyeshwa kuwa ndipo kampuni hiyo ilifunga mkataba wa kununua dhamana!

Bila kujali kuwa Tangold haina dhamana, haijasajiliwa, haijawa na lundo la riba, wala fedha kwenye akaunti zake, gavana Ballali anaagiza kuwa fedha zinazobaki, zipelekwe akaunti Na. 011103024852.

Tangold, Deep Green na benki ya Nedbank wanatumia karatasi na anwani zilezile za mitaa na jengo mjini Sandton, Afrika Kusini nakupitia msemaji mmoja aliyetajwa kuwa Wayne Khoury katika Nedbank.

Gazeti lilijitahidi kumpata Bw. Khoury kwa baruapepe yake ili kujua uhusiano wake na taarifa za malipo. Hata hivyo hadi tunakwenda mitamboni baruapepe ilikuwa haijajibiwa. Simu yake haikujibu.

Nedbank, kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, ilitumika pia kupitisha malipo kwa ajili ya kampuni ya Meremeta, moja ya makampuni yanayodaiwa kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka BoT na serikalini.

Wiki iliyopita, gazeti hili liliripoti ukosefu wa kanuni za utoaji fedha katika akaunti ya EPA; udhaifu katika utendaji na wizi wa nyaraka za BoT.

Imefahamika kuwa gavana Ballali alikuwa akimwagiza meneja wa tawi la NBC makao maku, P.J. Mapunda kulipa mabilioni ya shilingi kwa Deep Green, Tangold na Meremeta.

Mwandishi alipotaka kupata maoni ya Bw. Mapunda kuhusu madai hayo, aliambiwa na maofisa wa NBC kuwa kuwa ameishafariki.

Gavana Ballali alifariki Mei mwaka jana katika mazingira yaliyoacha maswali mengi; baada ya serikali kuficha alipo kwa kipindi kirefu.

No comments: