Saturday, February 7, 2009

Kikwete kumfukuza Masha


Kikwete kumfukuza Masha
• Ni kutokana na zabuni ya vitambulisho
• Adaiwa kumpotosha Waziri Mkuu Pinda

Na Saed Kubenea


RAIS Jakaya Kikwete huenda akalazimika kumtosa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kutokana na kashfa mbichi inayomkabili, MwanaHALISI limeelezwa.

Masha anadaiwa kuingilia isivyo halali mchakato wa kutafuta mzabuni katika mradi wenye thamani ya Sh. 200 bilioni.

Huu ni mradi mkubwa na wa aina yake serikalini wa kutengeneza Vitambulisho vya Taifa. Suala la vitambulisho vya uraia liko chini ya wizara ya mambo ya ndani.

“Kama serikali itakuwa makini na kutaka kulinda hadhi yake mbele ya taifa na dunia nzima, basi Masha hana kazi,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.

Masha anadaiwa kuingilia mchakato wa zabuni kwa kutoa siri za zabuni kabla ya Bodi ya Zabuni kumaliza kazi yake na kutetea mmoja wa waombaji.

Haijafahamika waziri Masha ana uhusiano gani na mwenye kampuni hiyo, lakini mawasiliano yake na Katibu Mkuu wa wizara yake, Bodi ya Zabuni na ikulu yanaonyesha “anatetea” kampuni ya Sagem Securite.

Zaidi ya waombaji 54 wa zabuni ni mmoja tu anayedai kutoridhika na ndiye Masha amebebea bango la kumtetea wakati hata mchakato wenyewe wa zabuni haujakamilika.

Katika dokezo lake kwa Katibu Mkuu wa wizara yake na katika barua kwa Katibu Mkuu Kiongozi (ikulu), Masha anapendekeza Bodi ya Zabuni iombe ushauri wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi serikalini (PPRA) wakati hilo halihusiki katika hatua hii ya mchakato.

Kwa hiyo, kama waziri, Masha anajaribu kuvunja sheria ya ununuzi ya mwaka 2004 inayoelekeza taratibu za kuchukua hadi kuhitaji maoni ya PPRA.

Utaratibu wa kwenda PPRA unahitaji kuwepo kwa upande ambao haukuridhika kati ya Katibu Mkuu, Bodi ya Zabuni au Kamati ya Ununuzi. Kwa hiyo Katibu Mkuu hana sababu ya kwenda PPRA kama alivyotaka waziri.

Masha anadai kupelekewa malalamiko na Sagem Securite, lakini taarifa zilizopo zinasema majibu ya matokeo ya mchakato wa kutafuta kampuni zitakazoendelea na hatua ya pili, hayajatangazwa na wala waombaji hawajapelekewa taarifa.

Hii ina maana mgombea anayelalamika kwa waziri, kama kweli ameishadondoka, amepata taarifa kwa njia isiyo sahihi na waziri anatumia njia isiyo halali kutetea aliyeko nje ya taratibu za mchakato.

Taarifa zinasema Waziri, hata alipopata malalamiko, hakuyapeleka kwenye Bodi, badala yake aliamua kwenda moja kwa moja kutetea mwombaji kwa kutaka kurejewa kwa hatua ambazo tayari zilikuwa zimepitwa.

Kuingilia shughuli za zabuni ambako waziri amefanya kunavunja Kifungu 33 cha Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2004 na kanuni zake kwani mamlaka aliyojaribu kutumia siyo yake bali ni ya Katibu Mkuu (Accounting Officer).

Hatua yake pia, ambayo inaonekana kumpendelea na kumpigania mwombaji mmoja, inakiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 na Kanuni 101(6) ya Taarifa ya Serikali (GN) Na. 97.

Kwa kuangalia mawasiliano ya waziri Masha kupelekewa malalamiko kwa waziri kunavunja vifungu 79-82 vya sheria ya ununuzi.

Kwa mujibu wa sheria, malalamiko sharti yapelekwe kwa Katibu Mkuu ndani ya muda wa siku 28; majibu yapatikane katika siku 30; kama mlalamikaji hakuridhika atakata rufaa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi.

Baada ya hapo mlalamikaji akiwa bado hajaridhika atakata rufaa kwa Mamlaka ya Rufaa ya Ununuzi na siyo kwa waziri.

Katika kutaka kujua zaidi juu ya mawasiliano ya Masha na ikulu, mwandishi wa habari hizi aliambiwa kuwa waziri huyo alimpotosha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kumweleza kuwa Katibu Mkuu wa wizara yake ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni. Ukweli ni kwamba Katibu Mkuu anateua mwenyekiti wa Bodi hiyo.

Barua ya Masha kwa waziri mkuu ambayo MwanaHALISI inayo nakala yake, iliandikwa 19 Desemba 2008 ikiwa na Kumb. Na. CAB.214/364/01/H/45.

Kwa kuangalia mwenendo wa mchakato wa zabuni ya Vitambulisho vya Taifa hadi sasa, unaelekea kuwa kama ule wa zabuni ya kufua umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya Richmond wa mwaka 2006.

Katika mchakato huo, kiongozi wa serikali wakati huo, Edward Lowassa anadaiwa kushinikiza mawazo yake ndiyo yakubaliwe na kukiuka sheria ya ununuzi ya umma, ushauri wa wataalam na maelekezo ya baraza la mawaziri, mambo ambayo yalimgharimu nafasi yake ya waziri mkuu.

Aidha, mawaziri wa nishati wa wakati huo ambao walifanya kazi ya “kuitangaza” Richmond kana kwamba ni maofisa wake wa uhusiano – Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujiuzulu.

Wakati wa mchakato wa mkataba wa umeme, Masha, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mbunge wa Nyamagana, alikuwa naibu waziri wa nishati na madini chini ya waziri Dk. Msabaha.

Kuingiliwa kwa mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya uraia kunaweza kusababisha taratibu kusimamishwa au kuanza upya; jambo ambalo litaiingiza serikali katika hasara kubwa.

Kwa zaidi ya miaka kumi sasa, kumekuwepo “wimbo” wa kutengeneza vitambulisho vya uraia nchini na wananchi wakafikia kuamini kuwa ni mradi wa “kutafutia fedha za wakubwa.”

Habari kutoka bungeni zinasema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge, imemwita waziri Masha ili kutaka kujua kinachoendelea kuhusu mchakato wa zabuni ya vitambulisho.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wilson Masilingi amesema, “Ni kweli. Kamati inataka kujua kama kweli amevunja taratibu za ununuzi.” Amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuona hoja binafsi ya Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa Karatu.

“Kama amevunja sheria na taratibu kama inavyoelezwa, tutachukua hatua. Hilo ndilo jukumu letu. Ni vizuri tukapata taarifa kutoka kwake kabla ya kuchukua hatua. Hatuwezi kumhukumu mtu bila kumsikiliza,” amesema Masilingi.

Alipoulizwa iwapo Kamati yake inamwita ili kumlinda, Masilingi alipaza sauti na kusema, “Hatumlindi Masha. Tunatekeleza wajibu wetu.”

Naye Dk. Slaa anatarajiwa kuwasilisha bungeni hoja binafsi akimtaka Masha ajiuzulu au serikali impumzishe kazi. Haijafamika hoja hiyo itawasilishwa lakini taarifa zinasema ni wiki hii.

Mwisho

No comments: