Thursday, May 1, 2008

Rostam ajianika

Rostam ajianika
· Hoja yake bungeni hii hapa
· Kibiliti kitupu, CCM watishiwa nyau
· Aishia kumtkana Dk. Mwakyembe


Saed Kubenea

Na Saed Kubenea


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kilitishiwa “nyau” na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, na kikatishika. Alichotaka kukiwasilisha bungeni, hakikuwa na nguvu za kuadhirisha Bunge wala CCM, MwanaHALISI limegundua.

Kwa mujibu wa waraka wa Rostam ambao MwanaHALISI linao, hoja yake ilikuwa dhaifu, haikuwa na nguvu ya kulidhuru Bunge wala CCM.

Vile vile, Rostam ameshindwa kujiokoa na tuhuma kwamba anahusika na kampuni ya Richmond kwa sababu katika sehemu ya maandishi yake, ingawa anakiri kwamba haifahamu, anakiri kuwa alikuwa na maslahi ya kibiashara na kampuni ya Dowans iliyochukua kazi za Richmond iliyoshindwa kazi.

”Mheshimiwa Spika, hakuna hata mfanyakazi mmoja wa Caspian anayeifanyia kazi Dowans. Isipokuwa narejea tena maelezo niliyoyatoa katika mchango wangu kwamba watumishi wa kampuni yangu wanaweza kushirikiana na kampuni yoyoye ambayo kampuni yetu ina nia ya kufanya nayo biashara,” anasema katika hali ya kung’ang’ana.

Anasema, „„Na hilo lilifanyika kama ambavyo pia ni kweli kuwa kampuni ya Caspian ambayo mimi ni Mwenyekiti wake iliruhusu Dowans kutumia anuani ya posta na barua pepe yake kwa sababu tulikuwa tunatarajia kupata kazi ya ukandarasi wa ujenzi kutoka kwao, ambayo ndiyo biashara kuu ya kampuni ya Caspian.”

Anasema, „Mheshimiwa Spika, hiki si kioja kama ambavyo Mheshimiwa Mwakyembe na Kamati Teule alitaka ionekane. Ni taratibu za kawaida kabisa katika shughuli za biashara kuwa na kitu kinachoitwa “hospitality arrangement” yaani kupeana fursa za kutumia baadhi ya huduma baina ya kampuni zinazokusudia kufanya biashara au kupeana kazi.”

Anasema, „Hili linaweza likaonekana ni jambo kubwa la kuzua maswali kwa watu wasio na uelewa wa uendeshaji biashara lakini ni jambo la kawaida kabisa katika ulimwengu wa ushindani wa kibiashara ambapo kila kampuni inatafuta kandarasi kutoka kwa mwenzake.”


Licha ya kushindwa kujinasua, alitumia muda mwingi kumtuhumu Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba kati ya serikali na Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe, akimshambulia moja kwa moja na kumuita kwa majina kadhaa yasiyopendeza, na hivyo kuimaliza nguvu hoja yake mwenyewe.

Hoja ya Rostam haikuwasilishwa bungeni baada ya Spika wa Bunge, Samwel Sitta kuikataa kwa maelezo kwamba imejaa matusi na haikuwa na jipya.

Spika Sitta alisema kilichotaka kuwasilishwa na Rostam kilikuwa ni kile kile alichokitoa wakati alipochangia katika mjadala wa ripoti ya Kamati Teule.

Ni kutokana na hali hiyo, Spika Sitta aliamua kuwasilisha mbele ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM, hoja ya Rostam ili baada ya kuijadili, upatikane ufumbuzi.

Hatimaye, Kamati hiyo iliridhia maoni ya Sitta na kuamuru kuzuia hoja hiyo kuwasilishwa mbele ya Bunge. Uamuzi huo uliyoibua maswali mengi huku baadhi ya wabunge wakiona walinyimwa haki ya kupata kile Rostam alichotaka kuwasilisha.

Hata pale wabunge wa kambi ya upinzani, waliposimama bungeni kuomba mwongo wa Spika ili kupata kile kilichoandikwa na Rostam, wabunge wa CCM walikuja juu.

Anna Abdallah, akitetea uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya CCM, alihoji, “ninyi mna maslahi gani na masuala ya wabunge wa CCM?”

Katika maelezo yake, Rostam amekana ushahidi uliotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Salva Rweyemamu. Alipohojiwa na Kamati Teule ya Bunge, Salva alisema ni yeye aliyemtambulisha kwa bosi wa Richmond.

Salva, aliyemtaja kama mwenye kampuni ya ushauri katika masuala ya habari (G&S Media Consultancy), amekaririwa katika ripoti ya Kamati ya Bunge akieleza kwamba alitambulishwa kwa Richmond na Rostam.

Rostam ametoa maelezo akisema ushahidi huo hauna nguvu kwa kuwa Salva “alidhani” kuwa yeye (Rostam) ndiye mwenye Richmond, akimaanisha kuwa Salva hakuwa na uhakika wa jambo hilo.

Katika hoja yake iliyozuiwa na CCM kuwasilishwa bungeni kikao kilichomalizika wiki iliyopita, Rostam ameshindwa kutoa vielelezo vya kuthibitisha madai aliyoyatoa kuwa Kamati Teule ya Bunge ya Mwenyekiti Mwakyembe, iliendelea kufanya kazi hata baada ya muda wake kwisha.

Waraka wa Rostam wa kurasa sita, haukueleza kwa namna yoyote ile mazingira ya kuthibitisha kwamba ni kweli kamati hiyo ilikuwa kazini baada ya 31 Desemba, siku iliyopangwa kuwa ya mwisho wa kazi kwa kamati hiyo.

Kitu ambacho Rostam amefanikiwa kukitetea ni kwamba hakuwepo nchini wakati alipoitwa na Kamati Teule, kwani amewasilisha pasipoti yake aliyodai ina mihuri ya Idara ya Uhamiaji inayoonyesha iligongwa wakati akitoka na kuingia nchini aliporejea kutoka likizoni nchini Uingereza.

“…kama nilivyoeleza katika mchango wangu wa maandishi, nilikuwa nje ya nchi kuanzia 17 Desemba, 2007 hadi 3 Januari, 2008. Nawasilisha kwako nakala ya photocopy ya Paspoti yangu ikiwa na mihuri ya Idara ya Uhamiaji inayoonyesha kutoka na kurejea kwangu hapa nchini kama kielelezo kinachothibitisha maelezo yangu hayo,” amesema.

Soma hoja kamili ya Rostam katika uk 12 wa gazeti hili.

mwisho

No comments: