Wednesday, April 9, 2008

Siri ya Muwafaka yafichuka


Karume alia mbele ya Kikwete

Na Saed Kubenea


RAIS wa Zanzibar Amani Abeid Karume, alilia katika vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijijini Butiama wakati akipinga kuwepo serikali ya pamoja kati ya chama chake na Chama cha Wananchi (CUF).

Akiongea kama Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Karume alisema muwafaka utafuta historia na hasa juhudi za baba yake, Abeid Aman Karume za kuasisi mapinduzi Visiwani.

Hii ilikuwa wakati wa kujadili hoja ya kuunda serikali ya pamoja kati ya CCM na CUF kufuatia mapendekezo ya kamati ya Rais Jakaya Kikwete ya kuondoa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

Karume ni mmoja wa wachangiaji katika vikao vya Butiama ambao walilia sana, kushawishi na kutoa tahadhari kuwa muwafaka wa kuunda serikali ya pamoja na CUF utaua maana halisi ya mapinduzi Zanzibar.

“Mnataka kuvunja historia,” amesema mpasha habari akimnukuu Karume. “Baba yangu alipigania jambo hili (Mapinduzi) na alikufa kwa kupigania jambo hili. Kukubali CUF kuingia serikalini, mnataka kufuta historia,” alimnukuu Karume akisema.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya vikao zinasema, kilio cha Karume kilikuwa mwanzo wa vilio vingine vya wajumbe wa Zanzibar ambao, mmoja baada ya mwingine, walieleza wasiwasi wa kupoteza jina “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – SMZ.”

Ni Rais Karume, ambaye kwa kutumia ujanja na nafasi yake, alipenyeza hoja ya kura ya maoni katika taarifa ya Kamati ya Rais Kikwete hata kabla haijawasilishwa katika Kamati Kuu (CC).

Hoja ya Karume ilikuwa ni pamoja na kutaka ushirika serikalini, kama utakuja, iwe baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 jambo ambalo tayari CUF wamelikataa kwa kishindo.

Kutokana na ushawishi wa Karume, wajumbe watatu wa Kamati ya Rais upande wa CCM ambao ni Yusuph Makamba, Kingunge Ngombale-Mwiru na Ali Ameir Mohamed, walipenyeza mawazo ya kura ya maoni bila kujadiliwa ndani ya kamati ya pamoja.

Chozi la Karume katika CC ndilo linasadikiwa kumlainisha Rais na Mwenyekiti Kikwete, kumsahaulisha ahadi yake na huenda kumbadilisha mawazo kuhusu umuhimu wa kumaliza haraka mpasuko Zanzibar.

Kikubwa zaidi ambacho wajumbe walililia ni “kupoteza madaraka” Viswani. Wengi waliona kushiriki kwa CUF katika utawala kutaweka chama hicho karibu na ushindi na hatimaye kukumba madaraka na kuizamisha CCM.

Mjumbe mmoja alikaririwa akiloloma, “Kulikoni? Kuna nini ndani ya CCM? Viongozi wetu mmetufikisha wapi? Utaratibu wetu unasema bwana, ninyi (CUF) hamna chenu.”

Mjumbe huyo ambaye ametajwa kuwa Mustapha Ahamada wa Kaskazini Unguja, alihoji, “Tunajadili nini hapa? Mnaturudisha nyuma. Wapinzani Zanzibar hawana wanachotambua; kwao mapinduzi haramu, serikali haramu na maendeleo haramu…mnatupeleka wapi?”

Alisema, “Wanatuita wahafidhina, mahafidhina. Watasema…tumeishawaweza. Leo sisi CCM, haki ya Mungu na Mtume, hatutashika tena madaraka Zanzibar,” akimaanisha iwapo CUF watashiriki utawala.

Kwa sauti ya juu na kuhema, Ahmada alisema, “Wafahamu (CUF) kuwa hatuko tayari. Kama mmeishachoka (akimaanisha viongozi wa CCM), acheni. Turudi na ASP Zanzibar.”

ASP – Afro-Shirazi Party – ndicho chama kilichoungana na Tanganyika Afrikan Union (TANU) kuunda CCM, 5 Februari 1977.

Mjumbe mwingine kuchangia hoja ya kuwa na serikali shirikishi Zanzibar alisema kwa kuwa CCM pamoja na kura ya maoni, sharti CUF wakubali masharti kadhaa.

Aliyataja masharti hayo kuwa ni kutamka hadharani kwamba wanautambua uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kuwa ulikuwa halali; kwamba wanatambua kuwa rais aliyeko madarakani Zanzibar ni halali na amechaguliwa kihalali.

Mjumbe huyo akijadili hoja ya kuweka uwanja linganifu wa kisiasa pemba, alisema, “Na Pemba ukiwapa uhuru wa mambo hayo, haki ya Mungu CCM itashindwa mwaka 2010. Hatuponi.”

Hata hivyo, mjumbe huyo alisema baada ya kutoa uwanja sawa na CUF kukiri kutambua serikali, Kamati ya mazunguzo ya CCM ipeleke mapendekezo yake katika Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya taifa Zanzibar kabla ya kufikishwa kwenye CC.

Katika sauti ya ushawishi na kuonyesha wasiwasi, mjumbe huyo alisema, “Bila kufuata haya, sisi wenyewe CCM tutakuwa tumejisokota.”

Akigeukia wajumbe wote na kukazia macho kwa mwenyekiti, alisema, “Mnatuacha wenzetu…mnatuacha! Leo Seif (Shariff Hamad) huyuhuyu, ambaye hataki mapinduzi, mnakaa naye eti kuridhisha wafadhili? Mimi sikubali hili. Mapinduziiiii!”

Hoja ya kuwa na serikali ya pamoja ilizua ubishi wa chinichini na hatimaye mlipuko wa ubishi na kung’aka kwa baadhi ya wajumbe.

Hali hiyo ilianzia kwa Kingunge alipoanza kutoa mapendekezo aliyoita ya Kamati ya Rais ambayo yalikuwa tayari yamefanyiwa marekebisho na CC.

Ilikuwa pale wajumbe walipoanzisha zogo na kumkatisha Kingunge mara kadhaa, Kikwete aliingilia kati ili kurejesha utulivu.

Akijaribu kuwatuliza wajumbe, Kikwete alisema tayari mapendekezo ya kamati yake yamefanyiwa kazi sana na CC na kuongeza kuwa, hata nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, ambaye ni msimamizi wa shughuli za serikali, atatoka katika chama cha rais.

Wakati Kamati ya Rais ilipendekeza chama kilichopata ushindi wa pili kitoe Waziri Kiongozi (msimamizi wa serikali), CC ilipeleka NEC pendekezo la kuwa na makamu wawili wa rais.

Kwa kuzingatia hoja ya “kuipiku” CUF, Kikwete alisema pendekezo la CC linataka makamu wa pili wa rais ndiye awe msimamizi wa shughuli za serikali. Huyo atatoka chama kilichotoa rais na ndiye atachukua nafasi ya rais wakati rais hayupo.

Alifafanua kuwa idadi ya mawaziri kwa kila chama itazingatia uwiano wa viti vya Baraza la Wawakilishi.

Katika hali ya sasa ambapo CCM ndicho chama kilichotoa rais, kama kungekuwa na serikali ya pamoja, basi makamu wa kwanza wa rais ambaye anatoka CUF angekuwa “picha tu.” Hana majukumu yanayoeleweka.

Mchangiaji mwanamke alitahadharisha CCM kuwa wakishindwa watapigwa mawe. Alisema, “Mmekaa, mmejadili yote haya; mnasema ni mambo mazuri. Haya! Lakini tusije tukapigwa mawe njiani.”

Tarehe 30 Desemba 2005, Rais Kikwete aliahidi Watanzania na dunia kwamba atamaliza kile alichoita “mpasuko wa kisiasa Zanzibar.”

Kamati yake imekutana mara 21 katika miezi 14 na kutumia karibu shilingi 2 bilioni kwa kazi ambayo, kutokana na mapendekezo ya Butiama, ndio kwanza imeanza upya.

Nayo CUF imeitisha maandamano nchi nzima kupinga kuwepo mapendekezo mapya ambayo yanatibua kazi nzima na kufanya mabilioni ya fedha za umma na wafadhili yaliyotumika, kuwa kama yamechomwa moto.

Maandamano ya CUF yataanzia Zanzibar, Jumamosi ijayo ambako kumbukumbu za mauaji ya Januari 26 na 27, 2001 zingali hai. (MwanaHALISI, Aprili 2008

Mwisho

1 comment:

zemarcopolo said...

Si sahihi kwa Tanzania kuwa mstari wa mbele kupinga apartheid Afrika ya Kusini na kwingineko Afrika halafu wakati huohuo apartheid Zanzibar inapewa heshima za kihistoria!