Thursday, May 1, 2008

Tahariri dhidi ya Rostam

mwisho
Rostam, tukutane mahakamani


TUMESOMA katika vyombo vingine vya habari kwamba mfanyabiashara kizito na Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi, amefungua kesi dhidi ya gazeti hili-MwanaHALISI. Anataka gazeti hili limlipe Sh 3 bilioni kama fidia ya “kusafisha” jina lake. Hiyo ndiyo thamani yake.

Zaidi ya hayo, Rostam Azizi anaiomba mahakama iamuru habari zake wakati wa mwenendo wa kesi hiyo, zisiandikwe na gazeti hili. Wakati tunasubiri taarifa rasmi kuhusu kushitakiwa kwa gazeti hili, tunapenda kusisitiza kwamba kwetu, hiki ni kitisho kingine.

Anachojaribu kufanya Rostam Azizi, ni kufunga mdomo wa wananchi wanaommulika yeye kama mfanyabiashara na mwanasiasa, ambaye matendo yake yanagusa moja kwa moja maslahi ya wananchi wa Tanzania.

Ifahamike wazi kuwa Rostam naye ni mmiliki wa vyombo vya habari, vinavyofanya kazi kama inayofanywa na MwanaHALISI, ingawa kwa viwango na malengo tofauti.

Lengo la MwanaHALISI linafahamika. Gazeti hili ni mdomo wa wananchi maskini wa Tanzania. Ni kioo cha kuwamulika wote walio na dhamana katika jamii, wanaozitumia vizuri na vibaya – Rostam akiwamo. Ni kauli ya wanyonge wanaonyanyasika kutokana na uroho wa wakubwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Inawezekana Rostam Azizi alidhani nasi tungeingizwa katika mkumbo wa vyombo vya habari vilivyoanzishwa au kununuliwa kwa ajili ya kulinda majina ya viongozi wa serikali ya awamu ya nne na maswahiba wao. Amekosea!

Kinachomsibu Rostam Azizi kimeshawasibu wengine pia walio katika mkondo mmoja naye. Kinafahamika. Faraja kubwa tuliyo nayo ni kwamba walau sasa jamii inaanza kuwajua watu wasiopendezwa na kazi yetu, wanaotutisha na kutudhulumu.

Kwa muda mrefu, baadhi ya wanasiasa walijifunika utukufu wa kisiasa ambao walidhani wangeendelea kuwa nao kwa sababu wanazozijua. Hawakutarajia kumulikwa na kukosolewa, kazi ambayo tumeifanya vema.

Kwa hatua hii ya sasa ya Rostam Azizi ni dhahiri hataki kukosolewa. Lakini hatutaki kuamini kwamba Rostam Azizi amesahau wasifu wake katika jamii ya Watanzania.

Na hatutaki kuamini kwamba hajui kuwa hata haya yaliyoandikwa juu yake anayolalamikia sasa ni matone tu katika bahari ya mengi ambayo sasa anajaribu kuyazuia kwa kitisho cha mahakama.

Rostam Azizi si maskini. Lakini hilo halikumzuia kuwadai maskini Sh bilioni tatu, ambazo kwake ni thamani ya jina lake. MwanaHALISI halina pesa ya kuwagawia matajiri.

Pesa kidogo inayopatikana ni kwa ajili ya kuwaunga mkono Watanzania wazalendo na maskini katika vita dhidi ya mafisadi kwa kutumia uhuru wao wa kuhabarishana na kuwasiliana.

Tunaamini kwamba vitisho hivi vya Rostam Azizi na ’amri’ anazoipa mahakama, havina nia njema kwa taifa, bali vina lengo la kuficha ukweli kwa umma kuhusu siasa na biashara zake.

Rostam Azizi anataka wananchi wafungwe mdomo, macho na masikio dhidi yake. Yeye ana pesa, na anadhani atazitumia pesa hizo hizo kutunyamazisha, na kuwadhulumu wananchi maskini tunaowatetea.

Tungependa kumweleza wazi wazi kwamba vitisho vyake havitawazuia wananchi kufikiri, kuchunguza, kusema na kujadili kuhusu ufisadi unaofanywa na vigogo na maswahiba wao.

Tuna hakika kwamba gazeti hili halijamkashifu Rostam Azizi, bali limeandika habari asizopenda zijulikane kwa umma. Tuna hakika kwamba shida ya Rostam Azizi – ambaye pia ni mmiliki wa magazeti - katika suala hili si pesa, kwani anazo nyingi kuliko hizi, bali anataka kulifilisi na kuliua gazeti hili.

Gazeti hili halipo tayari kuwasujudia mafisadi. Kama ambavyo tumekuwa tunafanya huko nyuma, licha ya vitisho kadhaa tunavyoendelea kukabiliana navyo, tutaendelea kuandika bila kumwonea, kumpendelea au kumwogopa mtu yeyote.

Tutasimamia ukweli na haki na tutafichua ufisadi kwa maslahi ya taifa. Katika hili, hatutarudi nyuma; na kama Rostam Azizi anataka kutupeleka mahakamani, atangulie tutamkuta huko; na asubiri matokeo.

Ends

No comments: