Wednesday, April 9, 2008

Siri ya Msabaha dhidi ya Lowassa

Na Mwandishi Wetu

SIRI nzito moyoni mwa aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, ndiyo ililazimisha Edward Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu kutokana na kashfa ya Richmond, MwanaHALISI limegundua.

Habari nyeti zilizolifikia gazeti hili zinasema Lowassa alijiuzulu ili kuepusha mawaziri kuanza kutajana. Kama ingefikia hatua hiyo, Dk. Msabaha alikuwa tayari kuweka hadharani majina ya wakurugenzi halisi wa Richmond, akiwamo mtoto mmoja wa kigogo mzito serikalini.

Kwa mujibu wa habari hizo, Dk. Msabaha ndiye alikuwa na nakala halisi ya awali kabisa, yenye majina ya wakurugenzi wa kampuni hiyo feki; nakala ambayo hata Kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa hiyo haikuiona.

Lakini kutokana na mambo kuwa mazito dhidi ya Dk. Msabaha, huku akishinikizwa na Kamati ya Uongozi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ajiuzulu, yeyé alisema “nimesikia.”

Kamati hiyo hiyo, ilimshauri aliyekuwa waziri wa madini, Nazir Karamagi, naye ajiuzulu ili kulinda heshima ya serikali, akakubali.

Kwa mujibu wa Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM, ambayo nayo ilikuwa inajua fika sakata zima la Ridhmond, lakini inaogopa kuligusa kwa kuwa lilikuwa la wakubwa, baadaye Dk. Msabaha alisikika akijiapiza kwamba “sitakubali kutolewa kafara, lazime nife na mtu.”

Haikujulikana kama ‘mtu’ huyo alikuwa mtoto wa kigogo au kigogo mwenyewe; jambo lililoleta wasiwasi mkubwa na kulizimu ufanyike uamuzi mzito kuikoa serikali.

Lowassa hakuwa mmoja wa watu waliokuwa wametajwa na kamati hiyo, wala hakushauriwa kujiuzulu, lakini ilidhihirika kuwa alikuwa ameshiriki kushinikiza kampuni ya Richmond ipewe mradi wa kufua umeme wa dharura.

Kwa kuhisi kwamba Dk. Msabaha angeweza kuiumbua serikali kwa kuwataja hata wale ambao hawakutajwa na Kamati ya Bunge – ambao walikuwa wazito zaidi, na ambao Lowassa alikuwa akiwalinda wasiguswe – inasemekana aliamua kujiuzulu ili kumfunga mdomo Dk. Msabaha.

Habari nyingine zinasema hata Rais Jakaya Kikwete alijua ‘kila kitu’ kuhusu mradi huo, na kwamba alipoona mambo yamekuwa magumu zaidi alimshauri Lowassa afanye uamuzi ambao usingefumua makubwa zaidi, hata kama ungemgharimu nafasi yake ya uwaziri mkuu.

Habari za uhakika zinasema Kamati ya Uongozi nay a Wabunge wa CCM haikuwa imedhamiria kumtaka Lowassa ajiuzulu, lakini tishio la Dk. Msabaha dhidi ya vigogo ndilo lilimlazimisha Lowassa kuondoka.

Katika kikao chake cha majuzi Butiama, mkoani Mara, Kamati ya Usalama na Maadili iliitaarifu Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) juu ya mchakato uliokuwa umechukuliwa kuwalinda vigogo hao; na kwamba katika orodha ya waliopaswa kujiuzulu, Lowassa hakuwamo.

Hata hivyo, ilisisitiza kuwa Lowassa aliwashinikiza wahusika katika wizara ya nishati na madini, wakati huo chini ya Dk. Msabaha, kuikubali Richmond kwa sababu ya maslahi ya waliokuwamo.

Dk. Msabaha alikuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati mkataba wa kufua megawati 100 za umeme wa dharura unasainiwa kati ya serikali na kampuni hiyo.

Taarifa zimesema kwamba Kamati ya Uongozi iliwahoji Lowassa, Karamagi, Msabaha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, na uamuzi uliofikiwa ni kwamba watu wa kuwajibika walikuwa wawili tu, Karamagi na Dk. Msabaha.

“Wajumbe walifikia maamuzi yafuatayo:- Mhe Dk. Ibrahim Msabaha (Mb) Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mhe Nazir Karamagi Waziri wa Nishati na Madini wawajibike kwa kujiuzulu, kwa kuzingatia hali ilivyokuwa na kwa maslahi ya chama na Taifa.

“Viongozi hao waliitwa kwenye vikao na kuelezwa uamuzi wa vikao uliokuwa umefikiwa. Mhe. Karamagi alikubaliana na maamuzi na akaahidi kuandika barua ya kujiuzulu. Mhe. Dk. Msabaha alikijulisha kikao (kuwa) alikuwa amesikia na (kwamba) angekwenda kwenye mamlaka iliyokuwa imemteua,” inasema taarifa.

Kutokana na mlolongo huo wa mambo, kitendo cha Dk. Msahaba kutotamka kuwa tayari kujiuzulu, kilizusha hisia kuwa angekwenda kueleza kila anachokijua katika sakata zima la maandalizi na utiaji saini wa mkataba.

Vyanzo vya habari vinasema kutokana na Dk. Msabaha kusema tu ”nimesikia” bila kusema wazi kwamba angejiuzulu kama alivyofanya Karamagi, iligundulika kuwa jambo kubwa lilikuwa linakaribia kulipuka, hatua iliyomfanya Lowassa kuona umuhimu wa kuachia ngazi ilki walau kulinda mengine yasiibuke.

Habari zinasema kama kuna mtu anayejua fika namna mkataba wa awali wa Richmond ulivyoandaliwa, na majina yaliyokuwamo katika orodha ya wamiliki wa iliyoitwa kampuni ya Richmond, ni Dk. Msabaha.


Mwisho

No comments: