Wednesday, April 9, 2008

MwanaHALISI ndani ya vikao vya CCM

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimelalamikia baadhi ya viongozi wake kwa kutoa taarifa za siri za vikao vyake kwa vyombo vya habari.

Taarifa ya CCM iliyowasilishwa katika Halmashauri Kuu (NEC) iliyokutana Butiama wiki iliyopita, imesema majadiliano yake yamekuwa “yakivuja na kuandikwa kwenye magazeti.”

Taarifa imesema gazeti la MwanaHALISI, katika toleo lake la Februari 20-26 mwaka huu lilichapisha taarifa za vikao kama habari muhimu.

“Majadiliano ya vikao hivyo yalivuja na kuandikwa kwenye magazeti,” imelelemika taarifa.

“Gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano Februari 20-26, 2008 limeelezea kwa undani jinsi majadiliano yalivyofanyika katika vikao hivyo na hasa kikao cha wajumbe watatu wa Kamati ya Uongozi iliyokutana na Mwenyekiti wa chama, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,” imeeleza taarifa.

Kwa njia ya kutoa onyo, taarifa hiyo ya Usalama na Maadili iliyoko kwenye Waraka Na.3, imesema “Chama hakina budi kujielekeza katika kupata ufumbuzi wa tatizo la uvujaji wa siri za vikao ambao sasa unaonekana ni utaratibu wa kawaida.”

Suala la kuvuja kwa taarifa za habari na kuchapishwa katika MwanaHALISI lilisisitizwa pia na Rais na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.

Rais Kikwete amesema mtindo wa viongozi kutoa siri za vikao vya chama kwa watu wasiohusika, utakibomoa chama, maana utachochea viongozi kutoaminiana na kutuhumiana.

Alikuwa akijadili hoja ya Usalama na Maadili juu ya hali ya siasa nchini kati ya Agosti 2007 na Machi 2008.

“Hakuna anayeshinda vita kama siri zake zinatoka nje. Kamati Kuu tunasema wenzetu hawana vikao vyao, mbona vyao haviandikwi kwenye magazeti? Kwanini vinavyoandikwa ni vyetu tu,” alihoji Kikwete.

Aliwatahadharisha wajumbe wa NEC kwamba utaratibu wa kutoa siri za vikao kwa watu wa nje ya chama hauonyeshi kulinda mapenzi na hadhi ya mtu kwa chama chake.

Alisema, “Kama unakipenda chama, tambua hilo. Huu utaratibu wa kutoa siri za vikao vyako kwa mtu siye, si mapenzi kwa chama chako.”

Gazeti la MwanaHALISI limekuwa likiandika taarifa mbalimbali za vyama, ikiwemo CCM na wakati wote limekuwa likizingatia kupata taarifa kutoka vyanzo sahihi.

Habari ambazo taarifa inalalamikia zinahusu upatikanaji wa taarifa kutoka kikao cha rais na wajumbe watatu, John Malecela, Yusuph Makamba na Ali Ameir Mohamed, ikulu Dodoma.

Kikao hicho kilihusu maamuzi ya Kamati ya Uongozi ya wabunge wa CCM juu ya mkataba wa uzalishaji umeme wa Richmond, na hatua ambayo watuhumiwa wakuu walipaswa kuchukua.

Mwisho

1 comment:

Anonymous said...

Saed kubenea sasa hivi unaboer mtu wangu, mbona gazeti lenu haliko updated kwenye mtandao? yaani kila nikifungua nipate news motomoto hakuna kitu kunani lakini? mafisadi wamekunyamazisha nini? kaza buti tupe mpya mwanahalisi ndio gazeti makini la tanzania.