Saturday, March 15, 2008

Serikali kuzidi kung'ang'aniwa

Kambi ya upinzani bungeni, sasa itaongoza Kamati tatu za Kudumu za Bunge, kutokana na mabadiliko makubwa yaliofanywa na Spika wa Bunge wa Jamhuri, Samwel Sitta ya kuboresha utendaji kazi wa Bunge.

Taarifa zilizothibitishwa na Sitta mwenyewe zinasema, wapinzani wataongoza Kamati ya Hesabu za Fedha za Serikali (PAC), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LACT) na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POC).

Wabunge wanaotarajiwa kuongoza Kamati hizo, ni Dk. Willibrod Slaa, ambaye anatarajiwa kuiongoza Kamati ya LACT, Zitto Kabwe, kamati ya POC na John Cheyo, Kamati ya PAC.

Uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo unafanyika Jumanne wiki ijayo, lakini hakuna ubishi kwamba watakaochaguliwa kuongoza kamati hizo watakuwa ni hao.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Kanuni mpya za Bunge, zinataka kamati hizo ziongozwe na wapinzani, na kutokana na mgawano wa wabunge kwenye Kamati, ni wazi kwamba Slaa, Zitto na Cheyo, ndiyo watakaochaguliwa.

“Huu utakuwa ushindi mwingine kwa wapinzani, na utakuwa mtihani mwingine mgumu kwa CCM,” amesema mchambuzi mmoja wa siasa nchini.

No comments: