Tuesday, March 4, 2008

Sakatal la Richmond:

Bunge lilipaswa kwenda mbele zaidi

· Lowassa, Rostam hawawezi kujinasua
· Ushahidi wa Salva, Shoo wawatia kitanzi

WIKI iliyopita tulimalizia uchambuzi wa kauli za Edward Lowassa akijitetea kuwa “ameponzwa na wasaidizi wake” katika kashfa ya mkataba wa kitapeli wa kufua umeme wa dharula kati ya serikali na kampuni ya Richmond. Leo, Mwandishi Wetu, SAED KUBENEA, anaangalia, pamoja na mambo mengine, iwapo Kamati teule ya Bunge iliyochunguza mkataba huo ilitosha kuishia hapo ilipoishia.

NI wachache sana, wasiokubali kwamba Kamati teule ya Bunge, iliyochunguza mkataba wa kuzalisha umeme wa dharula kati ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) na kampuni ya Richmond Development Company (LLC), ilifanya kazi inayostahili pongezi.
Kila anayelitakia mema taifa hili, anakubali kwamba Kamati teule iliyokuwa chini ya mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ilifanya kazi vema.
Kwa waliokuwa wanafuatilia kazi za kamati hii, wanajua jinsi ilivyokuwa inatenda kazi zake. Ilifanya kazi katika mazingira magumu sana kutokana na hatua ya baadhi ya watendaji wa serikali kuamua kuitenga na muda mchache ulitolewa na Bunge kukamilisha kazi yake.
Kutokana na hali hiyo, wengi walitarajia kuwa kamati isingefanikiwa kutimiza majukumu yake kama umma ulivyotarajia.
Wapo watendaji wa serikali ambao katika kutimiza azima yao ya kuhujumu kazi za kamati, walifikia hatua ya kuficha nyaraka muhimu kwa lengo la kutaka ukweli usifahamike.
Kwa lengo la kutaka umma usifahamu kuwa Richmond haikuwa kampuni, bali lilikuwa ni genge la wezi waliojikusanya ili kuchota fedha za umma.
Kwa lengo la kuficha ukweli kuwa Richmond haikusajiliwa, si hapa Tanzania tu, bali hata huko Marekani, ambapo watetezi wake walikuwa wanajitapa kwamba ndiko ilikotokea.
Kwa lengo la kuficha ukweli kuwa hata mabenki ya Marekani, ambako tulihubiriwa kuwa ndiko nyumbani kwa Richmond, yaligoma kutoa barua ya dhamana (LC) ili kutekeleza mkataba wake kwa maelezo kwamba haziifahamu hiyo kampuni.
Waliokataa kushirikiana na tume teule ya Bunge na kuficha nyaraka, hawakutaka ifahamike kuwa serikali, kwa shinikizo, au ushauri wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ilishinikiza benki ya CRDB kubeba jukumu hilo ambalo tayari lilikataliwa na benki za Marekani.
Walionyima tume ushirikiano hawakutaka ifahamike kuwa, pamoja na mapungufu yote yaliyofahamika, kutokana na vilio vya vyombo vya habari na baadhi ya waandishi wa habari kuhusu “uwezo, hadhi na heshima ya Richmond,” bado serikali iling’ang’ania ‘kuibeba’ na hata kuamuru kuhamisha mkataba wake kwenda kwa dada yake Dowans.
Ni haohao ambao hawakutaka ifahamike kwamba serikali imeruhusu Richmond kuhamisha mkataba wake na kuuongezea muda mkataba huo hadi miaka miwili, wakati dharula ya umeme ikiwa imemalizika!
Hakika walitaka umma usifahamu kuwa baadhi ya watendaji serikalini waliamua kuficha hata nyaraka, ama kwa utashi wao, au kwa kuelekezwa na “mabwana zao,” ili wahusika katika sakata la Richmond wasiweze kujulikana hadharani.
Bila shaka, hicho ndicho chanzo, au kichocheo kilichomsukuma makamu mwenyekiti wa Kamati teule, Injinia Stella Manyanya, kutaka kuangaliwa upya kwa kauli ya “wako mtiifu,” kwa hoja kwamba inatumika vibaya.
Manyanya anasema, baadhi ya watendaji katika ofisi za serikali, wamefikia hatua ya kutii kila jambo yakiwamo yale yasiyostahili.
Hata hivyo, pamoja na matatizo yote hayo, na ukweli kwamba kazi ya Kamati haikuwa kuhukumu, bali kuchunguza mwenendo wa mkataba huo, lakini Bunge na Kamati yake hawawezi kukwepa lawama kwamba hawakulifikisha jambo hili mahali palipotarajiwa na mamlaka kuu ya nchi ambayo ni wananchi.
Lilikuwa ni jukumu la Bunge, baada ya kuona kamati yake imeishia kutoa taarifa, kuchukua hatua zaidi mbele.
Kwa bahati mbaya Bunge letu halikuona umuhimu wa kufanya hivyo. Halikukubali kufanya kazi ya kutoa maagizo na maelekezo, na hatimaye kuunda chombo cha kusimamia utekezaji wa mapendekezo yake.
Badala yake, Bunge likaishia kukubali mapendekezo ya kamati, kuanzia yale ya awali hadi ya nyongeza.
Kutokana na hali ilivyo ndani ya serikali, lilikuwa ni jukumu la Bunge kubeba dhamana ya kufuatilia, kusimamia na kushinikiza watendaji serikalini kutekeleza kama serikali yenyewe iliyoahidi.
Kwa kufanya hivyo, watendaji waliojikita serikalini na kujigeuza ‘miungu watu,’ angalau wangeogopa kwamba serikali ingewajibika mbele ya Bunge.
Hivyo mapendekezo ya Bunge yangeweza kutekelezwa kikamilifu, tofauti na hofu iliyopo sasa, ambapo utekelezaji wa ahadi hizo, utategemea dhamira iliyopo kwa watendaji wakuu serikalini, Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Kama Kikwete atageuka kutoka “Tumaini lililopotea” na kurudi katika “Tumaini lililorejea,” huku Pinda akaamua ‘kujipinda kwelikweli,’ basi angalau matumaini ya Watanzania yanaweza kurejea.
Lakini katika hali ya sasa, hakuna mwenye matumaini. Wengi tunaona kuwa mwisho wa siku ukifika, Pinda na Kikwete, watabaki wapweke.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wengi wa watendaji wanaotakiwa kuchukuliwa hatua, baadhi yao ndiyo watuhumiwa wakuu katika sakata hili.
Mfano hai, ni Mwanasheria Mkuu wa serikali, Johnson Mwamyika. Je, Mwanyika anapata nguvu wapi ya kumuwajibisha Maria Kejo, anayetuhumiwa kusaidia Richmond kutumbikiza serikali katika utapeli huu?
Kamati teule inaagiza Kejo achukuliwe hatua za kinidhamu, papo hapo kamati inataka Mwanyika awajibishwe.
Ni dhahiri kwa wanaomfahamu vema Kejo, hawawezi kuamini kuwa mama huyu alifanya haya kwa bahati mbaya.
Mmoja wa maofisa waandamizi serikalini, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Patrick Rutabazibwa, anathibitisha katika hati yake ya kiapo kuwa Kejo si mwadilifu kwa taifa lake.
Ni Kejo aliyetaka kumuhonga Rutabazibwa ili akubali kupitisha mkataba wa kinyonyaji wa IPTL. Rutabazibwa aligoma kuhongwa. Hata hivyo, mkataba wa IPTL ulisainiwa baada ya wahusika kumkiuka.
Au, wapi anaposimamia Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, ili aweze kuwajibisha watendaji wake wanne waliotuhumiwa kuisafisha Richmond?
Ni Hosea aliyetoa taarifa ya kuisafisha Richmond na kudai kwamba haikuleta hasara yoyote kwa serikali wakati leo hii kila kitu kiko wazi kwamba ni Richmond ambayo ni kitanzi cha watumia umeme nchini.
Nani ataamini serikali hapa, wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel ole Naiko, amefikia hatua hata ya kuupotosha umma kuhusu suala la Richmond, hadi Spika wa Bunge, Samwel Sitta, anachanganyikiwa asijue la kufanya?
Je, yuko wapi mwajiri wa Naiko, ambaye ana ubavu wa kumwajibisha kwa kauli zake za uchochezi ambazo zinataka kuliingiza taifa katika vita ya kikabila?
Nani aliyemtuma Naiko, hadi kufikia hatua ya kusema kwamba Kamati ililenga Wamasai, wakati kati ya wote waliotakiwa kuwajibishwa, mwenye asili ya Ummasai ni mmoja tu?
Kwa ujumla, uadilifu wa serikali unatiliwa mashaka. Hoja hii inapata nguvu zaidi leo, wakati wananchi wanaposikia kauli za kebehi na dharau, zinazotolewa na baadhi ya watumishi wa serikali, au taasisi zake kwa Bunge.
Ulikuwa wajibu wa Bunge kujipa jukumu la kusimama imara na kuhakikisha watumishi wa serikali walioshiriki katika kuliingiza taifa hasara, wanalipa hasara hiyo wao wenyewe, kama sheria ya utumishi wa umma inavyotamka.
Je, katika hali hii, nani atakayemvika paka kengele? Bila shaka hakuna. Sana sana, serikali itaishia kuwajibisha watendaji wake, lakini haitawasukuma mahakamani.
Ukiacha hilo, kuna hili la mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ambaye anasema hana uhusiano wowote, na wala hajui kampuni ya Richmond.
Katika utetezi wake kwa njia ya maandishi wakati wa mjadala bungeni, Rostam alijitetea kwamba Kamati teule ilikuwa na muda wa kutosha wa zaidi ya siku 45 za kumuita; lakini haikufanya hivyo, badala yake imemsingizia kumiliki kampuni ya Dowans.
Kamati ya Bunge inasema, kushindwa Rostam kutoa ushahidi kumechangia kushindwa kujulikana kwa vitu muhimu sana. Kwa mfano, kamati imeshindwa kujua “uhusiano wa kindugu” kati ya kampuni ya Caspian na Dowans ambapo barua pepe (imeili) na sanduku la barua zinazotumiwa na makampuni hayo ni zilezile.
Rostam anajitetea kwamba si barua pepe tu, hata wafanyakazi wa ofisi yake wanaweza kufanya kazi Dowans, lakini kwamba yeye akawa bado hajawa mmiliki wa kampuni hiyo.
Hata hivyo, hakuna asiyemfahamu kwamba Rostam anawafahamu vema Dowans. Kutokana na Rostam kuwa rafiki wa karibu wa Rais Jakaya Kikwete na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), asingekubali anuani yake kutumiwa na kampuni asiyoifahamu.
Kwa vyovyote iwavyo, rafiki wa rais hatakubali kuchafuliwa. Rostam anajua kuwa iwapo atakubali kushirikiana na kampuni za kitapeli, hatachafuka yeye peke yake, bali hata swahiba wake Kikwete.
Hivyo basi, Rostam sharti awe anajua nani mmiliki wa Dowans; anatoka wapi na uwezo wake kifedha ukoje.
Anajua jinsi walivyopata mkataba wa Richmond, maana hata mwanasheria wa Richmond anasema hadi sasa hakumbuki kuwapo majadiliano kati ya mteja wake na Dowans ya kuhamisha mkataba huo.
Kutokana na hali hiyo, hakuna ubishi kwamba katika kuhamisha na hata kufanikisha mkataba huu, kuna mkono mrefu wa mmoja wa vigogo ndani ya serikali, au nje yake.
Na hili linapata nguvu zaidi kutokana na kuwapo ushahidi wa mtu muhimu sana, na ambao hauwezi kutiliwa mashaka. Huu ni ushahidi wa mkurugenzi wa mawasiliano, Ikulu, Salva Rweyemamu.
Salva anakiri akiwa chini ya kiapo kuwa aliyemtambulisha kwa Mohammed Gire wa Richmond ni “rafiki yake wa siku nyingi,” Rostam Aziz.
Vipi Rostam ajitokeze leo na kukana rafiki yake huyo waliyetoka naye mbali? Vipi Rostam aseme haifahamu Richmond/ Dowans, wakati hata Gideon Shoo, swahiba mwingine wa karibu na Rostam anathibitisha kuwa aliyewatambulisha kwa Gire ni yeye Rostam?
Akitoa ushahidi wake mbele ya kamati na chini ya kiapo, 19 Desemba, 2007 Shoo anasema, “Kwa sababu hii kazi imekuja through Rostam Aziz, who is a friend. Sasa mimi sikuzungumza na Rostam moja kwa moja, but I think he spoke to Salva…”
Shoo ni mwandishi wa habari wa kusomea. Katika kesi ya Reginald Mengi na Adam Malima, ushahidi wake ulitajwa kuwa ulisaidia sana kamati kufanikisha majukumu yake.
Na kwa kuwa Rostam, Shoo na Salva ni marafiki, lazima ushahidi wao ukubalike zaidi. Shoo, Salva na Rostam, wanapendana sana. Hakuna kati yao, mwenye ubavu wa kumficha jambo mwenzake.
Lakini kinachoonekana hapa, ni mzigo ambao Rostam ameamua kujitwisha katika kutafuta kujinasua na tope hili la Richmond.
Bali jambo moja ni wazi. Hadi hapa, na ukweli uliokwishapatikana, serikali inaweza kuvunja mkataba wake na Richmond na dada yake Dowans na isiathirike kwa lolote.
Tayari wataalamu wa sheria za mikataba wanasema, kama mtu amethibitisha kuwa hana uwezo wa kufanya kazi aliyoomba, mkataba huo huwa batili, na kwamba hasara zinaangukia huko ziliko.
Kwa maneno mengine, kama mkataba huu utavunjwa, serikali itanufuika na mashine zilizopo, huku Richmond na dada yake Dowans, wakinufuika na pesa walizokwishalipwa.
Je, kwa nini serikali inaendelea kuwa na kigugumizi? Inataka watu waamini kuwa ni kweli Dowans na Richmond ni makampuni ya mfukoni ya wapangaji wa Ikulu? Isifike huko. Serikali ichukue hatua.

MwanaHALISI- Machi5-12, 2008.

mwisho

No comments: