Tuesday, February 26, 2008

Rostam Aziz matatani

Na Saed Kubenea

MBUNGE wa Igunga, Rostam Aziz yumo matatani. Huenda akalazimishwa kujibu hoja juu ya kampuni ya Richmond katika mkutano wa Bunge wa Aprili.

MwanaHALISI linazo taarifa kwamba Rostam atalazimika kujibu, mbele ya Bunge, maswali ambayo alitakiwa kuyajibu ndani ya Kamati Teule iliyochunguza na kuthibitisha utapeli wa Richmond.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinasema mipango ya kumwandama Rostam ili atoe taarifa muhimu, kwa ajili ya hatua za baadaye, tayari imekamilika.

“Kinachohitajika hapa ni kupata taarifa zote kuhusu Richmond ambayo kila dalili zinaonyesha anaijua na huenda ni mmoja wa wamiliki wa chombo hiki hewa,” amesema mmoja wa wabunge wa CCM.

Rostam ni mtu muhimu katika mjadala mzima wa Richmond na picha yake ilisimikwa waziwazi na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu aliyesema mbunge huyo ndiye alimfahamisha kwa Gire (Mohamed?) anayedaiwa kuwa mmoja wa wakurugenzi wa Richomond.

Kwa kuanzia, baadhi ya wabunge wanataka kuwasilisha hoja binafsi bungeni, kutaka Rostam ahojiwe juu ya kuhusika kwake na kampuni ya Richmond.

“Kanuni za Bunge zinaruhusu hoja binafsi na zinaruhusu pia kuhojiwa kwa mbunge au wabunge pindi kuna hoja muhimu tena kwa maslahi ya taifa,” ameeleza mbunge huyo.

Taarifa zinasema kumwacha Rostam apete katikati ya lawama na tuhuma zinazomwelemea aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri wawili, “ni kukataa kuona ukweli.”

Baadhi ya wabunge wa CCM waliohojiwa na gazeti hili wanasema Tume Teule ya Bunge imefanya kazi yake na kutoa mwanga, na kwamba mwanga huo unaweza kuongezeka iwapo waliokataa kuhojiwa wataletwa na kuhojiwa na bunge.

Uzito na haraka ya kumhoji Rostam vinatokana na haraka ya CCM kutaka kufanya kile kinachoitwa “kujisafisha” mbele ya wanachama wake na wananchi.

“Sikiliza mwandishi; hapa kuna watu wana urafiki na rais. Wanaweza kuwa wanafanya mambo wakifikiri kuwa rais hatawagusa. Sasa hapo hatutakuwa na chama wala serikali.

“Sharti sasa tuandae mazingira mazuri kwa rais kufanya kazi yake bila woga wa kulaumiwa na rafiki zake wa sasa na wa zamani na bila upendeleo au kusingiziwa,” ameeleza mmoja wa wabunge waliohojiwa.

Iwapo hatua ya kutumia hoja binafsi kumhoji Rostam bungeni itafanikiwa, basi Bunge litakuwa limejiongezea hadhi mbele ya wananchi na serikali.

Spika wa Bunge, Samwel Sitta hakupatikana kusema lolote kuhusiana na hoja hii, bali mmoja wa wanasheria wa Bunge amethibitisha kwamba hili limo katika madaraka ya Bunge.

Aidha, habari za baadaye zimeeleza kwamba utaratibu huo wa kuwahoji viongozi watuhumiwa ndio utatumika pia kuhoji mahusiano na kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., iliyojichotea zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mbunge wa Igunga anahusishwa na kampuni ya Kagoda ambayo ilichotewa mabilioni ya shilingi wiki nne tu tangu isajiliwe kutpka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT.

Sokomoko la Kagoda hivi sasa linapamba moto kimyakimya, huku kukiwa na taarifa kutoka mafichoni aliko aliyekuwa gavana wa BoT, Daudi Ballali zikitaja majina halisi ya wahusika.

Wakati wamiliki wa Kagoda wanatajwa kuwa watu wa kawaida, John Kyomuhendo na Francis William, taarifa za ikulu zinasema mmoja wa wafanyabiashara nchini tayari amehojiwa na Tume ya rais kuhusu fedha za EPA.

MwanaHALISI inazo taarifa kwamba aliyehojiwa (jina tunalaihifadhi hadi baadaye), ni anayedaiwa “kununua kesi” ya Kagoda kutoka kwa waliokuwa wakiiendesha kwa madai kwamba wangesaidia kumlinda.

Hata hivyo, ushahidi ulioko BoT unaonyesha majina kamili ya walioweka saini kuchukua fedha kutoka EPA kuwa si John Kyomuhendo wala Francis William wanaoitwa “wakurugenzi” waanzilishi wa Kagoda.

Wiki iliyopita serikali iliwanyang’anya pasipoti baadhi ya wahusika katika kashfa ya BoT na kuwazuia kwenda nje ya nchi.

Makampuni yaliyochukua fedha BoT kupitia madeni ya EPA yametajwa kuwa ni pamoja na yale yanayomilikiwa na wanasheria mawakili wa mahakama kuu jijini Dar es Salaam.

Makampuni 22 yalichota zaidi ya shilingi bilioni 133 kutoka BoT yakidai kuwa miongoni mwa yale yaliyokuwa yakidai serikali.

“Makampuni yameundwa hapahapa Dar es Salaam na Waswahili tunaowajua. Yamesajiliwa hapahapa. Yamechota fedha hapahapa hata bila ya kuwa na uhusiano wowote na wanaoidai serikali. Hapa ndipo ufisadi ulipofikia,” ameeleza Mohamed Lwakasisi mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam.

Katikati ya Januari mwaka huu Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume kuchunguza wahusika wote katika suala la EPA na kuchukua hatua za kuwakamata na kuwawekesha mikataba ya kurejesha fesha hizo katika muda maalum.

Katika Tume hiyo kuna Mwanasheria Mkuu wa serikali Jonston Mbwambo ambaye ni mwenyekiti. Wengine ni pamoja na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema na Mkurugenzi wa TAKUKURU Edward Hosea.

Hata hivyo kumekuwa na malalamiko katika siku za karibuni kwamba Hosea hastahili kuwa katika tume hiyo kutokana na kutumiwa kuficha utapeli wa kampuni ya Richmond iliyoshindwa kuzalisha umeme wa dharula nchini.

Mwisho

No comments: