Thursday, March 13, 2008

Nani ataweza ‘kumwokoa’ Kikwete?

MwanaHALISI, Machi 12, 19, 2008
Na Saed Kubenea

JUMAPILI iliyopita, nilipokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms), kutoka kwa Saguda Mahela, aliyejitambulisha kwangu kuwa ni msomaji wa gazeti la MwanaHALISI, akinipa pole kutokana na kutishiwa maisha.
Alisema, “Poleni ndugu zangu. Nawaomba msife moyo. Endeleeni na kupigania taifa letu…Leo hii, Baba wa taifa akifufuka, atakuwa na marafiki wachache sana. Wengi aliowaachia madaraka, wamekuwa wanafiki za wazandiki.”
Mahela anasema ameguswa sana na taarifa niliyoitoa kwa wananchi Ijumaa iliyopita, kwamba chombo chao kinasakamwa na watumishi wake wanatishiwa kuangamizwa.
Jambo moja ni wazi, nalo ni kwamba kilio hiki si cha MwanaHALISI peke yake. Ni dhahiri wanaotishia gazeti hili wanatishia magazeti na vyombo vingine vya habari. Wanaotaka kunyamazisha gazeti hili wanataka kunyamazisha vyombo vyote vya habari na wananchi pia.
Wanaoendesha vitisho wanadhamiria jambo moja tu; wanataka kupora haki zetu za kikatiba na haki ya kukusanya na kusambaza habari.
Lakini pia wanaotaka kutunyamazisha wanataka tuache kumwambia Rais Kikwete kwamba waliomzunguka hawafai na kwamba wanateketeza taifa.
Kama aliowateua kumsaidia wamekataa kumwambia ukweli, kwa nini wananchi wasimwambie kupitia MwanaHALISI?
Binafsi, sikutarajia kama taifa hili linaweza kufika hapa. Kwamba, ndani yetu wanaweza kutokea watu wasioheshimu hata mchango wa wazazi wetu, waliojitolea mhanga katika kupigania uhuru wa taifa letu.
Kwamba, kumbe wapo watu miongoni mwetu waliojipa madaraka na hata mamlaka ya kupora uhuru wetu.
Ni ukweli usio na shaka kwamba iwapo vyombo vyote vya habari na waandishi wa habari, watakubali kuwekwa mfukoni mwa watawala, taifa hili litaangamia.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba si Chama Cha Mapinduzi (CCM), wala Baraza la Mawaziri, au vyombo vya usalama, vinavyoweza kuwa na ubavu wa kumueleza rais bayana kwamba hapa umekosea.
Tayari Baraza la Mawaziri lililopita limedhihirisha hilo. Lilipoteza kabisa uwezo wake wa kumsaidia rais kutimiza majukumu yake.
Hili linatibitishwa na Kamati teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kufua umeme wa dharula, kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC).
Kamati ya Bunge, ilibaini kuwepo ukiukwaji mkubwa na wa makusudi wa maagizo ya Baraza la Mawaziri uliokuwa unafanywa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliyefukuzwa na bunge.
Kamati haikuona, katika uchunguzi wake, jitihada za aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati, Dk. Ibrahim Msabaha kumzuia Lowassa kukiuka sheria na taratibu za nchi.
Si hivyo tu, Dk. Msabaha mwenyewe hakusema mbele ya Kamati teule na umma kwa ujumla, kwamba alimueleza rais Kikwete kuwa yeye Lowassa alipindisha maagizo yaliyopitishwa chini ya uenyekiti wake (rais).
Badala yake, Dk. Msabaha analalama kwamba hakuhusika na kadhia hiyo. Anasema “amefanywa kondoo wa kafara.”
Kauli hii ya Dk. Msabaha, ambaye inaelezwa kwamba anajua mengi kuhusu mkataba huo, inadhihirisha kuwa ndani ya serikali, Kikwete yuko pekee yake. Wasaidizi wake, ama hawapo, au wameamua kuasi.
Je, ni kweli kwamba Dk. Msabaha hakufahamu njama za Lowassa za kuvunja maamuzi halali ya baraza la mawaziri? Je, hakujua kwamba alikuwa na wajibu kumueleza rais juu ya hatua hiyo ya Lowassa?
Bila shaka alijua, maana Dk. Msabaha anafahamika kwamba ni mtu makini na msomi wa kiwango cha juu mno. Anajua taratibu za kuendesha serikali, kwa sababu amekuwamo ndani ya serikali kwa muda mrefu.
Kama yote hayo aliyafahamu, lakini akashindwa kumueleza rais, badala yake “akaitonya sikio” Kamati teule ya Bunge juu ya ubabe wa Lowassa, Kikwete anaweza wapi kusimama na kusema anao wasaidizi imara katika serikali yake?
Na dhambi ya kunyamazia ufisadi haiwezi kumpata Msabaha pekee yake, bali karibu mawaziri wote waliokuwamo katika baraza la mawaziri lililopita.
Mawaziri hawa walikuwa wanajua jinsi Lowassa alivyokuwa anaendesha serikali kama vile anaongoza kijiwe cha kahawa.
Ukiondoa udhaifu wa mawaziri, kuna udhaifu mwingine mkubwa katika vyombo vya ulinzi na usalama. Ni wazi kwamba vyombo hivi vimeshindwa kumshauri vema rais.
Kwa mfano, vyombo hivi haviwezi kujitapa kwamba vilimshauri vema rais wakati wa kuunda baraza la mawaziri, au katika uteuzi wa baadhi ya watu ndani ya serikali.
Kama vilimshauri na Kikwete akaamua kuachana na ushauri huo, basi ni lazima kuna jambo. Ama Kikwete amegundua udhaifu wa vyombo vyake katika kusimamia ukweli, ama na yeye anaweza kuwa “bwana haambiliki.”
Lakini inavyoonekana, kuna matatizo katika uongozi wa vyombo hivi. Maana ukiangalia baadhi ya walioteuliwa (tumejadili hili katika makala zilizopita), utabaini pasipo shaka kwamba taasisi hizi hazijafanya kazi yake kama inavyotakiwa.
Kama hiyo haitoshi, vyombo vya usalama vilishindwa hata kusema, kwamba kampuni ya Richmond haikuwa imesajiliwa Tanzania, wala Marekani. Kutokana na hali hiyo, watu makini lazima watatilia mashaka uwezo wa vyombo hivi katika kumsaidia rais vema.
Katika chama chake, hali ni hiyohiyo. Ndani ya Kamati Kuu (CC) hadi Halmashauri Kuu (NEC), wengi waliochaguliwa ni watu wa “wako mtiifu.”
Wakati wa uhai wake, akiwa madarakani na hata baada ya kuondoka, Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alivitumia vikao vya chama kutengeneza serikali. Vikao vilitawaliwa na mijadala mikali na ya wazi.
Kupitia vikao hivyo, ndipo uaminifu wa viongozi wa chama na serikali ulipopimwa. Ndimo mahali ambamo watu walisutwa kwelikweli. Waliopatikana na tuhuma, hawakucheleweshwa. Walilazimishwa kujiuzulu.
Humo ndimo makada mashuhuri akiwamo rais aliyekuwa madarakani, Aboud Jumbe Mwinyi, waling’olewa kutokana na kile kilichoitwa, “kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar.”
Si hivyo tu, ni katika vikao hivyo, aliyekuwa Waziri Kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zazibar, Seif Shariff Hamad, alifukuzwa katika chama.
Ni katika vikao hivyo pia, Horace Kolimba aliitwa kuhojiwa. Mlolongo ni mrefu mno.
Lakini kwa sasa, haitarajiwi hilo kutokea kutokana na ukweli kwamba CCM sasa si tena chama cha siasa. Hata wanachama wanasema CCM hivi sasa ni “dodoki.” Hakuna tena miiko ya uongozi katika chama. Uaminifu na uadilifu si tena sifa ya mtu kupata uongozi.
Kila uchaguzi unapowadia, wagombea wanashindana kuvuna kwa kura kutokana na kiwango cha pesa cha kila mgombea.
Katika mfumo wa sasa, ukichanganya ule wa mwenyekiti kuwa “mungu mtu” ndani ya chama chake, na upande mwingine kutokuwa na wenye uwezo wa kushauri na nia ya kujenga nchi yao, basi taifa linakwenda harijojo.
Mwenye uwezo wa kulielekeza taifa kutoka hapa lilipo anastahili nguvu nyingine ya ziada. Nguvu ya kusimama mwenyewe bila kutegemea fadhila za mwenyekiti, wala fedha za wanaojiita wafanyabiashara “waliokinunua” chama na baadhi ya viongozi wake.
Taarifa zinasema, kwamba viongozi wanaoweza kujipima kwa viatu vya Nyerere hivi sasa ndani ya Kamati Kuu ya CCM ni John Samwel Malecela, Samwel Sitta, Abdulrahman Kinana, Anne Makinda na rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassani Mwinyi.
Wapo wanaosema, kama vikao hivi vingekuwa imara kama zamani, hata suala la Richmond lisingewahi kufika bungeni. Lowassa angeadhibiwa na chama mapema kabla mambo hayajafika mbali.
Kwa hakika, ingekuwa CCM ya zamani, Lowassa asingeishia kujiuzulu uwaziri mkuu pekee, chama kingemtaka ajiuzulu nafasi zote alizonazo.
Wajumbe wangesimama bila aibu na kusema, “bwana huyu amekisaliti chama chetu. Amemsaliti rais wetu. Amewasaliti Watanzania waliotuamini na kutukabidhi madaraka.”
Tunajadili nani anaweza kumsaidia Kikwete. Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, hawezi kusema na hata akisema, hakuna anayeweza kuyatilia maanani maneno yake kwani Mkapa ni sehemu ya matatizo yote yanayokabili nchi sasa.
Mikataba yote kuanzia ule wa Net Group Solution, EPA na mkataba wa kupakua na kupakia mizigo bandarini kupitia kitengo cha makontena (TICS), imefungwa wakati wa Mkapa.
Kutokana na hali hiyo, mahali pekee ambapo Kikwete anaweza kupata salama ni kupitia vikao vya Bunge.
Kwa kupitia Bunge, ndipo mawaziri wanaweza kunyoosheana vidole. Huko ndiko mikataba michafu kama ya TICS, IPTL, EPA, Songas, uuzaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), inaweza kujadiliwa na ufumbuzi ukapatikana.
Kupitia Bunge, ndipo wananchi wanaweza kujua kwa uhakika, ni nani mmiliki wa Kagoda? Ni Rostam Aziz, au mfanyabiashara Yusuf Manji?
Huko ndiko dhamira ‘nzuri’ ya Kikwete inaweza kuonekana. Huko ndiko Lowassa, Nazir Karamagi na Msabaha wengine, wanaweza kuibuka na kutokomezwa.
Lakini kwa hali ilivyo sasa, ni vigumu kwa Kikwete kujikwamua kutoka katika mikono ya marafiki zake, waliojikita serikalini kwa ajili ya biashara.
Na huko si kwamba wanafanya biashara halali; hapana. Baadhi yao ni wakwapuaji wakubwa wa uchumi wa nchi. Wengine wanatajwa hata kuwamo katika kundi la kufoji nyaraka na kukwepa kodi.
Kisa? Wakati wa kampeni za Kikwete walifadhili chama chake. Sasa watu makini, wanajiuliza, nani atamuokoa Kikwete?

Mwisho

No comments: