Thursday, March 13, 2008

Kikwete akwama BoT

Na Saed Kubenea

TUME ya Rais Jakaya Kikwete ya kufuatilia walioiba fedha kutoka Benki Kuu (BoT) imeingia kwenye mgogoro na huenda matokeo ya kazi yake yasiwe ya maana kwa taifa.


MwanaHALISI linazo taarifa kwamba kuna mgawanyiko katika kamati. Wakati wajumbe kadhaa wanaona bora wakae na watuhumiwa na kujadili jinsi ya kurejesha fedha, wengine wanaona sharti watuhumiwa wafikishwe mahakamani ili liwe fundisho kwa ambao hawajajitokeza kurejesha fedha hizo.


Sababu nyingine ya mgawanyiko unaokaribia kuwa mtafaruku mkubwa ni pamoja na madai kuwa Tume imeshirikisha watendaji ambao wanatuhumiwa kumiliki makampuni yaliyokwapua Sh. 133 bilioni kutoka BoT.


Rais Kikwete, mapema mwaka huu, baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT, uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young, aliagiza makampuni 22 yaliyohusika katika ufisadi huo yachunguzwe.


Rais aliunda Kamati ya kufuatilia na kurudisha fedha zilizoibwa. Tume inaundwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika, Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hosea.


Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia MwanaHALISI, wajumbe wanaotaka wahusika wafikishwe mahakamani wana hoja kwamba hatua hiyo itasaidia kurahisisha upatikanaji wa fedha zilizoibwa.


Taarifa zimesema kwamba hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wengi wa watuhumiwa katika ufisadi huo wanamiliki mali nje ya nchi, na kwamba njia pekee ya kuweza kuzikamata ni kutumia mahakama.


Hata hivyo, imefahamika kuwa Kamati ya rais haina mamlaka kisheria na inachofanya ni zoezi tu la “uhusiano mwema” kati ya watuhumiwa na kamati hiyo.


Taarifa za kuaminika kutoka serikalini na ndani ya Tume, zinasema kwamba baadhi ya watuhumiwa wamekutana na Kamati na kuwekeana mikataba ya kurudisha fedha hizo.


Hata hivyo, taarifa zinasema baadhi ya mikataba hiyo ni ya muda mrefu sana, jambo ambalo limewasukuma baadhi ya wajumbe kushauri wahusika wafikishwe mahakamani mara moja ili kiwe kichocheo cha wengine kurejesha fedha katika muda mfupi.


“Ni kweli, wapo baadhi ya watuhumiwa wamesaini mkataba wa kulipa fedha hizo. Lakini wengi wameomba kurudisha katika kipindi cha mwaka mmoja hadi mitatu,” amesema mtoa habari.


Katika hali hii ya kutaka kulipa katika mwaka mmoja hadi mitatu, kuna uwezekano wa watuhumiwa kukimbia, kukwepa au hata kuchelewesha zaidi malipo, wameeleza wajumbe wa Kamati wasiopenda mikataba na watuhumiwa.


MwanaHALISI, adhuhuri jana liliwasiliana na Mwenyekiti wa Tume, Mwanyika likitaka kujua iwapo kuna watumishi katika sekretariati ya Kamati ambao ni watuhumiwa wa ufisadi BoT.


Mwanyika, ambaye alikuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa simu, alisema hana habari kuhusu kuwepo kwa mtu yeyote ambaye anatuhumiwa kwa ufisadi katika timu yake.


Alisema anachojua ni kwamba Kamati yake inaundwa na wakuu wa Polisi, TAKUKURU na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambayo ni ofisi yake. Zaidi ya hapo hajui “mtu mwingine.”


Alipong’ang’anizwa kwamba muhusika yumo katika sekretariati ya Tume na hakuteuliwa na rais, alisema hilo halijui hadi aulize wenzake kwani hadi sasa wameshughulikia makampuni tisa tu kati ya 22 yaliyokwapua mabilioni ya shilingi kutoka BoT.


Wanasheria mbalimbali waliozungumza na MwanaHALISI juu ya uwezekano wa kuwepo mfanyakazi katika sekretariati ya timu ya rais ambaye ni mtuhumiwa wa ufisadi wa BoT, wanasema “hiyo ni hatari sana.”


Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba, alisema kama ni kweli kwamba kuna mtuhumiwa wa ufisadi aliyejumuishwa katika timu inayochunguza mafisadi wenzake, basi “taifa hili limeporomoka.”


“Huo ni mgongano wa kimaslahi. Hakutakiwi kuwamo mtu wa aina hiyo. Kama waliomuweka hawajui, basi alitakiwa awaeleze,” alisema.


Mwanaharakati huyo alisema kitendo cha mtuhumiwa kuwa ndani ya sekretariati ya Tume kinafanya mchakato mzima wa kufuatilia watuhumiwa wa ufisadi katika EPA, kuwa wa kiini macho.


Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, alisema ni makosa kisheria kwa mtu mwenye maslahi binafsi kijihusisha na jambo linalochunguzwa.


Dk. Mvungi alikumbusha kwamba katika suala hilo kulikuwa na tuhuma za serikali kutumia vyombo vyake kufanya ufisadi na kuna wakati idara ya Usalama wa Taifa ( Tanzania Intelligence Services- TIS) ilitajwa.


Dk. Mvungi alimtaka Rais Kikwete kujitenganisha na mafisadi hata kama fedha zilizoibwa zilitumiwa katika kampeni iliyomwingiza madarakani.


“Vinginevyo Rais Kikwete anaweza kujiingiza katika mgogoro mkubwa. Tunamuomba, tena kwa nia njema kabisa, ajiweke katika jukwaa safi, akiweka mafisadi kuchunguza mafisadi, anaweza kudhaniwa kwamba naye yumo,” alisema Mvungi.


Wabunge watatu ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wamelieleza MwanaHALISI kwamba matarajio ya rais yaweza kuyeyuka iwapo ndani ya Kamati kutakuwa na wale wanaostahili kuchunguzwa.

Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, kinara wa timu ya upinzani iliyokuwa ya kwanza kufichua hadharani ufisadi wa BoT, ameshtushwa na taarifa za kuwepo mtumishi wa Kamati ambaye anatuhumiwa.


Dk. Slaa alikumbusha kwamba tangu awali, kambi ya upinzani haikuridhika na mchakato mzima wa uchunguzi wa suala hilo kwa sababu “waliohusika ndio wanaojichunguza.”


“Ndiyo maana tunaendelea kupiga kelele tukisema kazi haijafanyika. Tunataka serikali, na hasa Rais Kikwete, achukue hatua mara moja kushughulikia suala hili ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wote wanaohusika,” alisema.


Kiongozi mmoja mstaafu wa serikali, ameliambia MwanaHALISI kuwa ana taarifa za kuwepo mtuhumiwa katika EPA ambaye anachunguza wenzake.


“Wizi huu uliotokea BoT kinaweza kuwa kitu kidogo sana. Lakini tatizo kubwa hapa ninaloliona ni taifa letu kuanza kujenga matabaka ya watu walio juu ya sheria na walio chini. Hii ni hatari sana,” alisema kiongozi huyo.


Hata hivyo alishangazwa na hatua ya kamati ya akina Mwanyika kujadiliana na watuhumiwa wa EPA kwa lengo la kurejesha fedha zilizoibwa.


Alisema kamati hiyo kisheria haina mamlaka ya kujadiliana na watuhumiwa, achilia mbali kuamua kuwaachia huru. Alishauri wahusika wote wafikishwe mahakamani kwa kuwa kosa lililotendwa ni la jinai.


Makampuni yanayotuhumiwa kuchota mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT ni pamoja na Malegesi Law Chambers; Money Planners & Consultants; Kiloloma and Bros Enterprises; Mibale Farm na Kagoda Agriculture Limited.


Mengine ni Ndovu Soap Limited; Njake Enterprises Limited; Navycut Tabacco (T) Limited; Becon International Limited; Bina Resort Limited; Changanyikeni Residential Complex Limited na Njake Hotels and Tours Limited.


Pia yamo Bora Hotel and Apartment Limited; Liquidity Services Limited; V.B. & Associate Company Limited; Maltan Mining Company Limited; Venus Hotels Limited; B. V. Holding Limited; Kernel Limited, G & T International Limited, Excellent Services Limited na Clayton Marketing Limited.

Yote yanatajwa kufanikiwa kuiba kiasi cha shilingi 133 bilioni kutoka EPA, baadhi yao yakitumia nyaraka za kughushi; yakidai yanawakilisha wadai wa nje wa serikali.


Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa na Serikali, kupitia kwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, zimesema kuwa baadhi ya wahusika wa makampuni hayo, wameanza kurejesha fedha.


Hadi wiki iliyopita, serikali ilisema kiasi cha Sh. 50 bilioni zilikuwa tayari zimerejeshwa hadi mwishoni mwa wiki iliyopita.


Hata hivyo, taarifa mpya aliyoitoa Mwanyika wiki moja baada ya tamko la Mkullo, ilisema ingawa wahusika wanarejesha fedha, “imekuwa vigumu kuwanasa” kwa kuwa hawajulikani wenyewe hasa ni nani.


Suala hili limepokelewa kwa mshangao mkubwa kwa vile si rahisi kwa kampuni kurejesha fedha ilizoiba halafu waliorejesha fedha wasijulikane.


Taarifa zaidi zimesema kuwa wanaorejesha fedha hufanya hivyo kwa kutumia hundi wakiandika tu majina ya kampuni, kiasi kwamba inakuwa vigumu kuwagundua.


Kumekuwa na kilio kikubwa kwa umma kutaka kamati iwataje hao wanaorejesha fedha hizo na kuwakamata ili wafikishwe mahakamani badala ya kuendelea kuwaficha kwa kutumia visingizio dhaifu.

ends

No comments: