Thursday, March 20, 2008

Masikini mama yetu Tanzania!

Na Yusuf Aboud
MTU akiugua ugonjwa wa kansa na akachelewa kutibiwa hadi ugonjwa ukasambaa mwilini, hukabiliwa na hatari ya kufa, labda itokee miujiza ya Mwenyezi Mungu.

Hivi ndivyo ilivyo nchi mama yetu, Tanzania.

Ufisadi uliopo ni sawa na ugonjwa wa kansa ambao “ulishamvaa” mama yetu kiasi kwamba ana muda mfupi mno wa kuishi baada ya kuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa muda mrefu.

Ugonjwa wa “kansa ya ufisadi” umeshambulia zamani kwenye vichwa vya wasomi wetu, ukashambulia viungo vingine kama vile “vigogo na magogo” (wafanyabiashara na watu mashuhuri) halafu makapi (wananchi wanaumia sana). Swali nani aliyesalimika?

Ufisadi haujaanza leo. Ulikuwepo baada ya ibilisi (shetani) kudanganya binadamu wa mwanzo (Adamu na Eva) kuwa watakapokula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya, eti watafanana na Mungu. Ulikuwa ni ufisadi wa hali ya juu.

Kinyume chake, walipoukubali ufisadi (udanganyifu, uasi) wakala matunda waliyokatazwa kula, kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu wa ki Mungu, walijikuta wakipata aibu kubwa na tangu hapo ufisadi umeendelea kuwatesa wanadamu.

Watanzania wa leo wanabwatuka, wanabwabwaja “ufisadi ufisadi” na wamesahau mambo ya msingi ambayo wangeyalalamikia ili kusaidia waondokane na umasikini. Kwa wingu la ufisadi, wamefunikwa na matokeo yake hawaoni waendako.

Kama hujui ulikotoka na ulipo, hufiki uendako. Ni hatari na inatisha. Suala hapa ni maendeleo kwa Watanzania wote na si familia moja au kikundi cha watu. Keki ya taifa inapaswa kugaiwa kwa wote.

Fedha za kusaidia wajasiriamali, maarufu kama “mabilioni ya JK” zimefikia wangapi na wangapi wamenufaika? Masharti yake yakoje. Mbona masikini walioko vijijini wanalalamika hawajaziona bali wanasikia walionufaika zaidi ni wafanyabiashara?

Hili ndio jambo la kulipigia kelele badala ya ufisadi ambao kwa ulivyojijenga, kuulalamikia ni kama kutwanga maji kwenye kinu.

Ni ufisadi wa aina ngapi uliibuliwa na zikachukuliwa hatua madhubuti kushughulikia wahusika? Tuanze na ununuzi wa rada ya kijeshi iliyofungwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu JK Nyerere. Nani ameadabishwa?

Hivi tunachosubiri ni kukamilika uchunguzi ulioanzishwa na Serikali ya Uingereza. Hata Rais Jakaya Kikwete alipoulizwa, alisema anasubiri huko, maana anashangaa taifa tajiri kudhulumu taifa masikini.

Karibuni ukaibuka ufisadi kuhusu mkataba wa Richmond wa kutuletea umeme wakati tunauhitaji baada ya taifa kukumbwa na ukame uliodhoofisha upatikanaji wa maji ya kuzalisha umeme. Tumeona tu viongozi kujiuzulu, na ile hasara iliyotokana na mkataba huo, imerudishwaje?

Tatizo la mabilioni ya shilingi kuchotwa Benki Kuu yetu (BoT) kwa jina la Lord Rajipal kwa ajili ya kuagiza meli za kusaidia usafiri Watanzania. Meli zilizokuja zilikuwa mbovu na mradi ukafa kibudu. Nani alichukuliwa hatua?

Kuna hili sakata jipya la akaunti ya madeni ya nje ndani ya BoT. Wajanja wameshirikiana na viongozi wetu na kuchota Sh. 133 bilioni wakijitia wanaidai serikali. Wako wapi walioshikwa hadi sasa? Hakuna isipokuwa ubabaishaji tu.

Kuna wenzetu waliokuwa machimboni Bulyanhulu, Kahama walifukiwa lakini haikuwa lolote mpaka leo, licha ya Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kuja juu na kuibana serikali na kuwa na picha ya kuonyesha tukio.

Ingekuwa nchi nyingine, tungejua moja na haraka. Wao wanajali raia wazo, wanahangaika wanapopata shida, iwe ndani au nje ya nchi yao.

Lakini mama yetu Tanzania kwa kuwa hajapona kansa ya ufisadi, akipigwa tu usoni manoti anaishia, anaacha kufuatilia maovu.

Mijitu tuliyoikumbatia inakomba rasilimali zetu inavyotaka. Hata kama wabunge wanakasirika, haiwi lolote maana mawaziri na watendaji wengine wa serikali walishaambukizwa ugonjwa wa kansa ya ufisadi.

Tunaona viongozi wa dini wakiombea wagonjwa wa vifua, vichomi na wengineo lakini wamesahau kumuombea mama Tanzania. Hawahawa walifanya maombi maalumu kutaka ije mvua ya kujaza mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme. Walifanikiwa lakini kwa hili la ufisadi, wamekwama.

Eee Mwenyezi Mungu, liokoe taifa letu, kama kuna wezi wanaofuja mali za taifa wadhihirishe, waokoe na waache ufisadi ili nchi yetu ipone.

No comments: