Thursday, March 20, 2008

Nani amewatuma walioanza kampeni UV-CCM?

Na Aman Rashid

KWA muda mrefu sasa, kumejengeka utamaduni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa kila unapofika uchaguzi mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), viongozi mbalimbali hata walio nje ya jumuiya, kujihusisha.
Ndio kusema kwamba uchaguzi wa jumuiya hii, kinyume na ile ya jumuiya nyingine za chama hiki, unakuwa na mvuto wa aina yake kwa jumuiya yenyewe na hata kwa chama chenyewe.
Ukweli huu umekuwa ukidhihirika kwa kuwepo jitihada na mbinu za kila kiongozi wa juu wa chama, kujaribu kushinikiza viongozi anaodhani watamsaidia kisiasa.
Hili si jambo linalojificha, linafahamika vema. Kudhihirisha hilo, mikakati miongoni mwa viongozi wanaodhani maslahi yao yanategemea matokeo ya uchaguzi wa UVCCM, imeanza.
Kwa bahati nzuri, UVCCM wamekuwa na viongozi wao wanaowataka na mara zote wamewashinda wale wa kupandikizwa na wakubwa au watu wa nje ya jumuiya hiyo.
Mwaka 1995, jumuiya hiyo ilitangaza hadharani mgombea gani wanamuunga mkono kati ya wale walioomba kuteuliwa. Hatua hiyo ilizua tafrani kubwa ndani ya chama hicho.
Nguvu ya UVCCM ndiyo iliyokuwa nguzo kubwa ya Rais Jakaya Kikwete kiasi cha kumfanya aongoze katika raundi ya kwanza ya kura, ingawa hakufikisha nusu ya kura.
Ziliporudiwa, Benjamin Mkapa alishinda, hali iliyoelezwa kuwa ilichangiwa sana na juhudi binafsi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kumuunga mkono Mkapa wakati huo akimuamini kama Mr. Clean (bwana msafi).
Sasa baada ya kuondoka kwa Mwalimu, UVCCM wamekuwa wakitamba na kuweka viongozi wanaowataka.
Kuna hisia za dhahiri kwamba ushindi wa Kikwete mwaka 2005 ndani ya CCM ulichangiwa kwa asilimia kubwa na kuungwa mkono kwake na UVCCM kama kundi imara lenye ushawishi na mikakati ya kisasa katika kampeni.
Mwaka huu jumuiya hiyo inaingia tena katika uchaguzi wake mkuu, kama zifanyavyo jumuiya nyingine za chama hiki. Wapo baadhi ya wanachama na wasio wanachama wameanza majaribio ya kutaka kupandikiza viongozi wanaowataka.
Tayari kuna minong’ono kwamba mtoto wa kiongozi mmoja mkuu ndani ya chama, ambaye ni mwanasheria, amejipa jukumu la kuwa mwenyekiti wa kamati ya kampeni ya rafiki yake mkubwa waliyesoma pamoja tangu shule ya msingi mpaka chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Kama vile hiyo haitoshi, kijana huyu mdogo amethubutu kupandishwa/kuteuliwa kushika nyadhifa za juu za jumuiya hiyo.
Hizi ni nyadhifa ninazokumbuka kupata kushikwa na watu wenye uzoefu mkubwa kama William Lukuvi, Ruth Msafiri na Amos Makala.
Wote hawa walizipata wakiwa tayari na umri wa kutosha na wamekomaa vema kisiasa.
Sasa swali linakuja jinsi ambavyo kijana huyu mdogo alivyopanda kwa haraka ndani ya miaka miwili na kushika wadhifa wa juu kabisa katika UVCCM.
Historia ya UVCCM inatukumbusha kuwa wagombea waliowahi kubebwa na vigogo na matajiri wakubwa wenye fedha nyingi, walishindwa.
Baadhi ya vijana waliokuwa na madaraka na kuonekana wana sifa za ziada katika uchaguzi wa mwaka 1998, nguvu hizo hazikuwasaidia.
Nakumbuka uchaguzi huo uliwahusisha watu kama Frank Uhahula ambaye amepata kuwa Mwenyekiti wa Taifa kwa miaka mingi wa Chipukizi, kitengo mahsusi na nguzo muhimu ya UVCCM. Alishindwa.
Hata Samson Kipepe ambaye amekuwa ndani ya jumuiya hiyo kama mtendaji kwa muda mrefu, alishindwa kwa kuwa vijana huwa wanachagua mtu wanayemtaka.
UVCCM ina historia ya pekee, kwa hiyo harakati hizi za kutaka kupanga upya safu ya uongozi wa wake, ni juhudi zitakazoshindwa kama ilivyokuwa huko nyuma.
Zipo taarifa za kuaminika sasa kwamba huyu kijana mdogo aliyepanda kwa kasi kiwadhifa, tayari amepanga nani wa kuwa katibu mkuu, naibu katibu mkuu, pamoja na makatibu wa idara; uchumi na fedha, uhamasishaji na wa chipukizi.
Haya yote yanaonyesha namna kijana huyu alivyo na ajenda ya siri na ambayo labda ametumwa na wakubwa. Inajulikana kwamba vikao vya mikakati yao vinafanyika kwenye baa ya Rose Garden.
Wachambuzi na wana historia wanakumbuka alipopewa nafasi John Guninita na Emmanuel Nchimbi hawakuwa wanaletwa na vigogo na wala watoto wao.
Hawakupangwa kama mtoto kigogo anavyoendesha mikutano mkoani Pwani, Lindi na Mtwara na kutamka bila ya woga kwamba UVCCM inamtaka nani na haimtaki nani.
Tumekuwa tukiangalia kwa makini na kufuatilia kauli na jitihada binafsi ambazo zimekuwa zikifanywa au kufanyika chini ya himizo za kijana huyu.
Huyu ni kijana ambaye kwa hali ya kawaida hakustahili kuongoza jumuiya hii katika cheo tunachoamini kuwa kama angekuwa mwenye nia njema na safi ya kuiletea UVCCM maendeleo, basi hapo alipo anaweza kufanya hayo.
Mpanga mkakati huyo, anatajwa kugombea Ujumbe wa Baraza Kuu la Taifa kupitia nafasi za Bara ili aweze kutumia kofia hiyo kumsaidia rafiki yake, kauli aliyoitoa hivi karibuni. Na anatamba kwamba rafikiye huyo “atashinda tu hapana wasiwasi.”
Inaonyesha kuwa hategemei kamwe kampeni katika mkakati wake huo. Na hiyo ni kielelezo cha kiburi na kujiamini kwake kupita kiasi. Kauli kama hii aliitoa wakati wa mchakato wa kugombea nafasi za Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Na kweli aliokuwa anawapinga, hawakupita.
Kinachoshangaza ni kuwa huyu anayesukumwa kuwa mwenyekiti kadi yake ya UVCCM haina hata miaka mitatu, ameletwa pale kama mwanasheria, akabebwa kuwa Mjumbe wa NEC, leo Naibu Katibu Mkuu na sasa anataka kuwa mwenyekiti. Wengi tunajiuliza mbona haraka haraka hivi?
Kuna nini? Tunajiuliza mbona mapema watu wanajipangia vyeo na wa kumpa? Jambo gani wanataka kutufanyia ambalo hatulijui?
Leo tunaanza kuwaogopa na kuanza kujiuliza je, hawa wanadhamira njema? Wana uwezo wa kutuongoza? Wana maadili mema? Au wametumwa? Na nani na kwa lipi?
Na kwanini watumie pesa na wanazitoa wapi? Yote haya yanatufanya tushtuke. Kwa nini watoto wa vigogo wote wawe nyuma ya mgombea mmoja? Haya yote yanatukumbusha historia yetu na kutufanya sisi watoto wa wakulima ndani ya UVCCM kuungana na kuweka kiongozi wetu wa vijana na si kiongozi wa vigogo na wa watoto wao.
Tunaamini walipita viongozi ambao ni waadilifu kama kina Kingunge Ngombale-Mwiru, Muhammed Seif Khatibu na wenye misimamo, akina Guninita, Emmanuel Nchimbi na Makala ambao leo ni faraja ya jumuiya yetu baada ya wote kubaki viongozi wenye msimamo na wanaohakikisha kuwa maslahi ya tabaka maskini, wanyonge yanasimamiwa.
Tunashangaa tunapoona leo wanapanga safu za uongozi kabla hata hatujachagua wenyeviti wa kata. Si hatari hii? Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunazuia hili lisitokee kwa gharama yoyote. UV-CCM haipandikiziwi viongozi.

*Mwandishi wa makala hii, amejitambulisha kuwa ni msomaji wa gazeti hili na mwanachama makini wa UV-CCM, anayepatikana Dar es Salaam.

No comments: