Thursday, March 20, 2008

Nani ameruhusu nchi kwenda vitani?

Na Saed Kubea

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepeleka majeshi nchini Comoro ili “kumng’oa” Kanali Mohamed Bacar ambaye anadaiwa kung’ang’ania kwenye madaraka katika kisiwa cha Anjouan baada ya muda wake wa utawala kumalizika.
Askari 650 wa Tanzania tayari wamewasili nchini humo, tokea 11 Machi, 2008 kushiriki kumg’oa Kanali Bacar ambaye kipindi chake cha uongozi kimemalizika tangu Aprili 2007.
Uamuzi wa serikali kupeleka majeshi Anjouan, ulitangazwa na mawaziri Dk. Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), katika mkutano wao na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizopepeleka majeshi ni Sudan, Senegal na Libya. Majeshi hayo yamepewa jukumu la kumng’oa Kanali Bacar, kumkamata na kumfikisha mahakamani.
Muungano wa serikali ya Comoro unajumuisha serikali za visiwa vya Ngazija, Moheli na Anjouan katika muundo uliotokana na mkataba wa Fomboni wa 17 Februari 2001.
Membe anasema majeshi yanakwenda Comoro “kurejesha utawala wa kisheria na demokrasia” kisiwani Anjouan.
Kwanza lazima tuangalie uhalali wa Kanali Bacar kuwapo madarakani. Kwa mujibu wa Katiba ya Comoro, kutokana na kutokuwapo ukomo wa uongozi, mwanajeshi huyo alikuwa na haki ya kuendelea kugombea urais wa kisiwa hicho.
Hivyo hakufanya makosa zaidi ya kukiuka taratibu. Ni dhahiri jambo hili linaweza kurekebishwa bila kutumia nguvu za kijeshi. Mara nyingi sana nguvu za kijeshi husababisha madhara makubwa.
Aidha, katika uchaguzi aliouitisha, ambao nchi washirika katika vita hiyo wanaupinga, Kanali Bacar alishinda kwa zaidi ya asilimia 85. Je, AU inapingana na matakwa ya wananchi wa Anjouan?
Tujifunze Irak. Marekani ilivamia nchi hiyo mwaka 2003. Rais George Bush alijitapa kwamba vita hivyo vingechukua wiki chache sana, kutokana na alichosema “wananchi wa Irak wanaunga mkono kampeni za kumuondoa Saddam Hussein.” Vita inaendelea hadi leo.
Je, akina Membe wana uhakika gani iwapo hilo halitatokea kwa majeshi ya Tanzania, kama wanavyodai, ili kupunguza vifo na uharibifu wa nchi?
Mgogoro wa Comoro ulianza mara tu baada ya visiwa hivyo kujitawala kutoka Ufaransa mwaka 1975 na tayari serikali imepinduliwa mara 19 tangu hapo.
Hata hivyo, kuna kisiwa cha Mayotte kilichoasi tangu wakati wa uhuru baada ya kutaka kuendelea kuwa chini ya himaya ya Ufaransa, jambo ambalo hadi leo hii, mabingwa wa vita wameshindwa kulitafutia ufumbuzi.
Je, kwa nini AU haukupeleka majeshi yake hapo kukikomboa kisiwa hicho kutoka mikononi mwa utawala wa kikoloni wa Ufaransa?
Ni jambo gani linaloisukuma Tanzania na washirika wake kuivamia Anjoaun wakati wananchi wa kisiwa hicho hawajalalamika kudhulumiwa, kuteswa na kunyanyaswa na Kanali Bacar?
Kwa nini AU haijapeleka vikosi Zimbabwe kuwakomboa wananchi wanaoteseka chini ya mkono wa chuma wa Robert Mugabe?
Kwa nini Tanzania haijapeleka majeshi kuyakomboa maeneo yanayokaliwa na waasi wa Kongo (DRC) wanaoongozwa na Jenerali Laurent Nkunda?
Membe na Mwinyi wanasema kwamba watahakikisha vifo vya raia na majeshi vinakuwa vichache. Hawajasema wamepanga kuua watu wangapi katika hicho wanachokiita “kuua watu wachache.”
Lakini pia kuna hili la uhalali wa serikali kupeleka majeshi nje ya nchi kwa dhamira ya kuondoa utawala ambao haujalalamikiwa na wananchi wenyewe.
Hili si suala la kupeleka majeshi kulinda amani, kama tulivyowahi kupeleka nchini Liberia na Lebanon.
Kwa kuwa suala ni uvamizi wa kijeshi, basi angalau serikali ingepata ridhaa ya wananchi kupitia Bunge lao. Nchi haipaswi kuingizwa vitani bila ridhaa ya chombo cha wawakilishi, hata kama hilo lilishawahi kutokea huko nyuma.
Hata Marekani ilipotaka kuvamia Irak, Bunge lake la Congress lilijulishwa na baadaye likaidhinisha kwa kupiga kura.
Hata Serikali ya Japan ilifanya hivyo mwaka 2004 ilipotaka kupeleka wanajeshi wake nchini Irak kwa ajili ya kulinda amani.
Watawala wa Japan walikuwa wamefuta kabisa uwezekano wa wanajeshi wao kutumika popote nje ya nchi yao baada ya shambulio la bomu la nyuklia lililofanywa na Marekani katika mji wa Hiroshima mwaka 1945.
Pamoja na kwamba Bunge la Japan lilikubali serikali ipeleke wanajeshi nchini Irak, bado lilitaka wanajeshi hao wasishiriki katika mapambano, bali wabaki tu kuwa wahudumiaji wa shughuli za dharura za kibinadamu.
Wataalamu wa sheria Tanzania wanasema wazi kwamba hata sheria zetu na katiba yetu, haziruhusu wanajeshi kupelekwa nje ya nchi kwa lengo la kufanya uvamizi.
Lakini hilo halikufanyika, badala yake, Membe na Mwinyi wanasema, “tayari rais amelijulisha Bunge, Baraza la Mawaziri na vikao vya juu vya chama chake - Chama Cha Mapinduzi (CCM). Haifahamiki Bunge limeshiriki vipi katika uamuzi huu.
Je, kama hivyo ndivyo, ni wapi ambako Rais Jakaya Kikwete amepata madaraka na mamlaka ya kuipeleka nchi vitani?
Ni dhahiri kama serikali ingepeleka maombi yake bungeni na Bunge likaridhia uamuzi huo, angalau tungeweza kusema kwamba wananchi wameshirikishwa na wameridhika nchi iende vitani.
Hakika katika suala la nchi kwenda vitani, hakupaswi kuwepo ushirikishaji mtu mmoja au kamati moja ya bunge, bali kupata maoni mapana na ruhusa kamili ya bunge zima hasa inapokuwa kwamba Comoro haijaivamia Tanzania.
AU haikupaswa kukubali ombi la Rais Sambi la kupewa majeshi ili kumg’oa Bacar. Ingemshauri rais kuweka shinikizo kwa Kanali Bacar, kukubali kuitisha uchaguzi mwingine utakaosimamiwa na Jumuiya za Kimataifa. Na hili Kanali Bacar alilikubali.
Kwa kujua hilo, Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, amepingana na wenzake katika utumiaji nguvu za kijeshi. Anaamini kwamba mgogoro huo unaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo.
Inawezekana kabisa kwamba Kanal Bacar, ni mnafiki, katili na mzandiki wa kutupwa kama anavyodai Membe, lakini ukweli unabaki palepale kuwa bado anaungwa mkono na wananchi wake tena walio wengi.
Kama si hivyo, kwa nini rais Sambi ameshindwa kuingia Anjouan? Je, ameogopa nini? Hilo ndilo tunastahili kujengea mashaka.

Mwisho

No comments: