Sunday, February 10, 2008

Sakata la Richmond: LOWASSA KITANZINI

Na Saed Kubenea
MAWAZIRI watatu katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wanatarajiwa kujiuzulu wakati wowote kutokana na kashfa ya mkataba wa Richmond, MwanaHALISI limedokezwa.
Taarifa za kuaminika kutoka serikalini na ndani ya Bunge zinasema mawaziri hao watatu wanatajiuzulu katika kipindi cha mkutano huu wa Bunge.
Tayari mmoja wa mawaziri anapitapita miongoni mwa wabunge mjini Dodoma akilalama kuwa ameponzwa na Waziri Mkuu Edward Lowassa. Haijafahamika ni kwa msingi gani.
“Ndiyo wapo mawaziri watakaojiuzulu wakati wowote kuanzia sasa. Sifahamu ni lini, lakini ni katika mkutano huu wa Bunge,” kimeeleza chanzo cha habari cha gazeti hili.
Chanzo hicho kimesema, “Inawezekana wakajiuzulu kabla ya ripoti ya Dk. Mwakyembe (Dk. Harisson Mwakyembe), kuwasilishwa bungeni, au baada ya kuwasilishwa na kujadiliwa. Lakini uhakika ni kwamba watajiuzulu.”
Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu mkataba katiya serikali na kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond, inatarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika mkutano wa sasa wa bunge.
Taarifa zinasema kujiuzulu kwa mawaziri hao kunafuatia shinikizo kubwa lililotokea ndani ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Imeelezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa CC, walikuja juu, wakitaja majina na kushinikiza kwamba wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi unaohusu Richmond waachie ofisi za umma “na bila mjadala.”
Imefahamika kwamba wajumbe waliokuwa wakishinikiza waliongozwa na Abdulrahaman Kinana na makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela. Taarifa zinasema walishinikiza kwamba rais Kikwete “awaondoe” mawaziri wake iwapo hawatakubali kujiuzulu kwa hiari.
“Mjadala ulikuwa mkali. Rais alikubaliana na hoja za wajumbe. Alisema kila anayetuhumiwa ni vema akaondoka, kabla hajaondolewa,” alisema mjumbe mmoja wa CC, akimnukuu Kikwete.
Mawaziri wawili wanaotajwa kuwa na uwezekano wa kujiuzulu ni Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mtangulizi wake katika wizara hiyohiyo, Dk. Ibrahim Msabaha.
MwanaHALISI halikuweza kupata mara moja jina la waziri wa tatu anayetakiwa kujiuzulu.
Dk. Msabaha ambaye sasa ni Waziri wa Afrika Mashariki, anasulubiwa kutokana na mkataba huo kusainiwa wakati wa utawala wake.
Dk. Msabaha aliondolewa katika wizara hiyo Oktoba 2006 katika mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri.
Karamagi amebanwa ajiuzulu kutokana na tuhuma kwamba aliongeza mkataba wa kampuni ya Dowans, bila kumshirikisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Dowans ndiyo iliyonunua mkataba wa Richmond ambapo kama ilivyokuwa kwa dada yake (Richmond), ilishindwa kukamilisha kazi kwa wakati.
Wakati mawaziri wanajiandaa kujiuzulu kwa shinikizo, mmoja wa wabunge wa zamani katika CCM anasema kunaweza kuibuka mgogoro mkubwa iwapo mawaziri hao watakataa kushinikizwa na kutaka “waondoke na waliokuwa wakiwatuma.”
MwanaHALISI inazo taarifa kwamba kuna malalamiko mengi miongoni mwa watuhumiwa ambao wanadai kuwa walikuwa wakipokea amri “kutoka juu” katika kutekeleza mkataba wa serikali na Richmond.
“Iwapo watakuwa jasiri na kumtaja huyo aliyeko juu na ambaye alikuwa akiwaamuru au kuwaelekeza, basi watakuwa wamepona na yeye atalazimika kujiuzulu kwa aibu kubwa,” kimeeleza chanzo cha gazeti hili.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mkataba kati ya serikali na Richmond ulisainiwa bila kufuata taratibu, ikiwamo kutofikishwa katika kikao cha makatibu wakuu (AMTC).
Kikao hicho kinachokuwa chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, ndicho chenye jukumu la kujadili jambo lolote ambalo litatakiwa kufikishwa katika Baraza la Mawaziri.
Kutokana na hali hiyo, mkataba wa Richmond haukifikishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri, ambacho mwenyekiti wake ni rais wa Jamhuri.
Vyanzo vyetu vya habari vinasema, mkataba kati ya serikali na Richmond ulijadiliwa na Dk. Msabaha kama waziri mwenye dhamana ya umeme, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji na Waziri Mkuu Lowassa.
“Mkataba haukufikishwa katika kamati ya makatibu wakuu. Wala haukufikishwa katika Baraza la Mawaziri,” waziri mmoja mwandamizi ndani ya serikali aliliambia MwanaHALISI.
Alisema, “Wakati mkataba unasainiwa, rais Jakaya Kikwete alikuwa ziarani Marekani. Aliporudi nchini akakuta tayari kila kitu kimevurugika. Ndipo alipoamua kufuatilia ili kujua ukweli wa suala hili.”
Bunge katika kikao chake kilichopita, liliunda Kamati teule kuchunguza mkataba kati ya serikali na kampuni Richmond.
Kamati hiyo iliongozwa na mbunge wa Kyera (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe.
Taarifa za ndani ya kamati zinasema, pamoja na mambo mengine, Kamati imeridhika kwamba Richmond haikuwa kampuni yenye hadhi, uwezo, wala heshima ya kupewa kazi iliyoomba.
Inaelezwa kwamba, Kamati ya Bunge, imeridhika kwamba Richmond nchini Marekani, ni kampuni inayojishughulisha na vifaa vya ofisini, wakati nchini Tanzania inajishughulisha na utoaji huduma za intaneti.
Mjadala wa Richmond tayari umepamba moto kila pembe ya nchi, huku wabunge waking’ang’ana kutaka kuwatoa macho wote wanaohusika.
“Kama mjadala utakuwa umekwenda kwa usawa, hakuna mwenye uhakika wa kubaki. Hata Lowassa, anaweza kung’oka,” alisema mbunge mmoja wa CCM.
Katika hali inayoashiria kwamba mambo yameiva, mwishoni mwa wiki iliyopita, wabunge waligomea semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu muswada wa Sheria ya Umeme na Biashara ya Mafuta ya Petroli.
Kwa kauli moja wabunge walishinikiza kwanza waletewe ripoti ya Richmond ili waijadili kabla ya kupitisha mswada huo.
Aidha, wabunge walisikika wakisema kwamba hawana imani na uongozi wa wizara hiyo na Tanesco kwa vile “vimejaa uchafu,” na kwamba hawawezi kujadili mambo mengine hadi “wahusika wajisafishe.”
“Zile za jana (Jumapili iliyopita) zilikuwa salamu za rasharasha. Kazi kamili inakuja wakati wa kuwasilisha hoja. Safari hii hatutaki tena kutumiwa kama mihuri,” alisema mbunge mwingine wa CCM, ambaye alitaka jina lake lisitajwe gazetini.
Kujiuzulu kwa mawaziri kutapunguza shinikizo la wanachama wa CCM kwa viongozi wakuu wa chama hicho, hasa rais Kikwete ambaye amekuwa akituhumiwa kulinda mawaziri wake walioboronga.
Naye mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, akizungumzia mvutano kati ya wabunge wa CCM na mawaziri wao, alisema kwamba kama Karamagi anasoma nyakati alipaswa kujiuzulu mapema.
“Kama kujiuzulu, alitakiwa ajiuzulu tangu siku ya semina. Sura za wabunge zilionyesha wazi kuwa hawamtaki,” alisema Dk. Slaa.

No comments: