Tuesday, February 26, 2008

rICHMOND: Lowassa anaweweseka?


MwanaHALISI 27 fEBRUARI-MACHI 4, 2008

Na Saed Kubenea
WAZIRI Mkuu “aliyeng’olewa na Bunge,” Edward Lowassa, ameanza kujitetea akisema hakupokea rushwa yoyote kutoka kampuni ya Richmond Development Company.
Lowassa anasema kilichotokea ni kwamba aliponzwa na watendaji walio chini yake; na kwamba binafasi hakuhusika na mchakato mzima ulioipa ushindi wa zabuni Richmond.
Anasema, “Sikuhusika katika mchakato wa zabuni ulioipa ushindi Richmond. Mimi niliponzwa na wasaidizi wangu. Hawa ndiyo walioniangusha. Nimewajibika kwa niaba yao,” Lowassa amewaambia wafuasi wake na wananchi kwa ujumla.
Lowassa anasema kazi ya kufanya uchambuzi wa kuchagua mzabuni, haikufanywa na yeye, bali ilifanywa na Kamati Maalum ya Serikali (GNT).
Hakuna ubishi kwamba utetezi huu mpya wa Lowassa ambao unatolewa siku 21 baada ya kujiuzulu na nje ya Bunge, unahitaji kuhojiwa.
Je, Lowassa kwa nini hakueleza haya ndani ya Bunge; badala yake amekimbilia kuyasemea TvT?
Na alipewa nafasi bungeni, alishindwa kulieleza Bunge kile ambacho amekieleza TvT na kwenye mkutano wa hadhara, kijijini kwake, katika jimbo la Monduli?
Inawezekana kabisa, Lowassa hakusema bungeni yale aliyosema Monduli na TvT kwa kuwa alijua wabunge wangeyapinga kwa kuwa wanajua ukweli mzima wa suala hili.
Ndiyo maana wala hakujihangaisha kujibu hoja za Kamati teule iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, iliyoonyesha mazingira ya kuhusika kwake.
Vilevile, Lowassa alijua kuwa Bunge lingekataa utetezi wake. Matokeo yake, angebanwa na kanuni zinazotaka mbunge kutosema uwongo bungeni.
Inawezekana pia kwamba Lowassa alishindwa kusema hayo bungeni, kwa hofu kwamba Nazir Karamgi na Dk. Msabaha walikuwamo ndani ya Bunge, na hivyo wangeweza kusema ukweli wa yote yaliyotokea.
Lakini ukiacha hilo, hata utetezi wenyewe wa Lowassa bado una mashaka.
Kwanza, Lowassa anakubali kuwa Kamati ya Maalum ya serikali iliyoshughulikia zabuni ya Richmond iliundwa kwa maelekezo na maagizo yake.
Lowassa ambaye leo anakana kuhusika na Richmond, ndiye anasadikiwa kutoa amri na hata kutisha wasaidizi wake, akitaka Kamati “Ibebe Richmond” na kuipa kazi iliyoomba.
Vilevile, ni Lowassa ambaye anatajwa kushinikiza upokonywaji Bodi ya Tenda ya Tanesco kazi ya kutafuta mzabuni, baada ya Bodi hiyo kukataa kuipa kazi ya kufua umeme wa dharula kampuni ya Richmond.
Ni Lowassa yuleyule anayetajwa kushinikiza kupunguzwa kwa vigezo ili kufanikisha azima ya kuipa kazi kampuni hiyo ya kitapeli.
Lowassa na wenzake walijua, pasipo na shaka kuwa Richmond ni kampuni isiyokuwa na hadhi, sifa, wala uwezo wa kufanya kazi iliyotaka kupewa.
Hili linathibitishwa na barua ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha kwenda kwa Lowassa, ambayo watetezi na wafuasi wa Lowassa wanaitumia kutaka kumsafisha.
Barua hiyo yenye Kumb. Na. CDB 286/397/01 ya 17 Juni, 2006 inasema, “…Nakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Majadiliano ya Serikali (GNT) ya kuteua Richmond na naomba kuwasilisha kwako, kwa uamuzi na maelekezo.”
Hii inathibitisha madai ya siku nyingi kwamba aliyeiteua Richmond kuingia mkataba na Tanesco, hakuwa Dk. Msabaha, alikuwa Lowassa.
Ni wazi kwamba Lowassa alitumia ustadi mkubwa kuiteua Richmond, kwani alitumia kichaka cha Kamati yake ya Majadiliano.
Barua ya Dk. Msabaha inaonyesha na kuthibitisha ukweli kwamba Lowassa alikuwa mstari wa mbele katika kusimamia, kupitisha, kuagiza na hata kuamuru Kamati kuipa zabuni Richmond.
Si barua ya Dk. Msabaha pekee, ambayo inathibitisha ukweli huo, bali hata barua iliyotoka ndani ya ofisi ya Lowassa mwenyewe inaliweka wazi jambo hili.
Msaidizi Mkuu wa Lowassa, ole Kuyan, katika barua yake kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anasema, “…Endelea kusaini mkataba kati ya Richmond na serikali, maana Waziri Mkuu, Edward Lowassa tayari ameridhika kwamba Richmond ipewe mkataba.”
Kauli kwamba Waziri Mkuu Lowassa “ameridhika” inafunga mjadala na inadhirisha kwamba Lowassa alijua kila hatua katika kufanikisha mkataba huu.
Aidha, kauli ya Kuyan, kwamba Waziri Mkuu ameridhika na hivyo mkataba kati ya serikali na Richmond usainiwe, inaonyesha wazi kuwa Lowassa ndiye aliyekuwa anasimamia jambo hili.
Kwa upande mwingine, hoja ya Lowassa kwamba aliwahi kumuonya Dk. Msabaha kuhusu “Ubabaishaji wa Richmond,” na “kutaka kuvunja mkataba huo mara mbili, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kuzuiwa na wanasheria,” haina uzito wala mantiki.
Sababu ni mbili: Kwanza, hakuna hata mwanasheria mmoja nchini na nje ya nchi, ambaye angeshauri serikali kubaki katika mkataba wa Richmond, kama Lowassa angesema ukweli kwamba Richmond haipo kwa mujibu wa sheria.
Hii ina maana haipo katika orodha ya kampuni za Marekani, wala katika orodha ya Wakala wa Msajili wa Kampuni (BRELA) nchini Tanzania.
Lilikuwa ni jukumu la Lowassa kuwaeleza kinaga ubaga wanasheria kwamba, si hapa Tanzania wala Marekani, ambako Richmond imesajiliwa.
Halikuwa jukumu la wanasheria kujua kama Richmond ni kampuni hewa. Hilo lilikuwa jukumu la Lowassa na serikali yake.
Kwani wanasheria ni kama madaktari; jukumu la kueleza maradhi linabaki kwa mgonjwa mwenyewe. Na mficha maradhi, umauti humfichua.
Lowassa hakuchukua jukumu hilo. Hakusema ukweli kwa wanasheria kuwa Richmond haipo kisheria. Kwamba Richmond ni kampuni ya mfukoni. Kwamba haina uwezo wala heshima ya kufanya kazi na serikali.
Kwa hakika, kama yote haya yangejulikana wazi kwa wanasheria, lazima wangeshauri serikali kuvunja mkataba, tena mara moja.
Kwa kuwa Richmond haikuwa imesajiliwa, wanasheria wanajua kuwa hakuna mtu ambaye angekwenda mahakamani na kudai yeye ni mmiliki wa Richmond.
Je, angeanzia wapi? Angetumia nyaraka gani kuthibitisha madai yake? Angesema nini mbele ya sheria? Wapi hasa angeshika?
Kutokana na hali hiyo, Lowassa asitake kukwepa jukumu lake la kikatiba la kutumia vyombo vya serikali kufanya uchunguzi na kujua uhalali wa kuwapo kwa Richmond.
Serikalai ilipaswa kujua nani mmiliki wa Richmond. Yuko wapi? Uwezo wake kifedha ni upi? Je, si tapeli lililokubuhu ambalo lilitaka kuingiza taifa mkengeni kama ilivyotokea?
Lilikuwa ni moja ya majukumu ya ofisi ya Lowassa kwenda BRELA, na kupekua mafaili ili kubaini ukweli wa madai ya wananchi na vyombo vya habari vilivyokuwa vinapaza sauti vikisema, Richmond haikuwa kampuni, bali kilikuwa kikundi cha watu waliojikusanya ili kuchota hazina ya taifa.
Lakini pamoja na kwamba Lowassa alijua ukweli huo, aliamua kukaa kimya. Hili alilifanya ili kupata mahali pakutokea, pale ukweli utakapodhihiri.
Maana hata pale ilipodhihirika kuwa Richmond haikuwa na uwezo wa kifedha, na kwamba mabenki ya Marekani yamekataa kutoa barua ya dhamana (LC), bado serikali iliamrisha au ilishauri au ilishawishi benki ya CRDB kubeba jukumu hilo.
Je, mbona Lowassa hataki kulisema hili, badala yake anaendelea kung’ang’ania wanasheria akidai wamemshauri vibaya?
Ni Lowassa ambaye alijiapiza na kusema, “Richmond ni watu makini,” na kwamba umeme utaingia katika Gridi ya Taifa ndani ya mwezi mmoja.
Ni uwongo huo uliomuambukiza Rais Jakaya Kikwete, hadi kufikia kuchukua hatua ya kuwadanganya wananchi na jumuiya ya kimataifa juu ya ujio wa umeme wa Richmond.
Wanaokumbuka vema wanajua kuwa alikuwa ni Lowassa ambaye alihubiri wananchi kutojadili Richmond kwa madai kwamba, “mabwawa ya kuzalisha umeme tayari yamejaa maji,” na hivyo hakuna tena tatizo la umeme nchini.
Ukiondoa hilo, kuna hili analolieneza kuwa yeye ni bingwa wa kuvunja mikataba nchini. Mfano anaotoa ni mkataba kati ya serikali na kampuni ya City Water.
Sasa swali tunajiuliza: Kama kauli ya Lowassa ina ukweli, kwa nini alishindwa kuvunja mkataba huu wa Richmond?
Mbona huu ndiyo ulikuwa wazi zaidi, ambapo hata ‘juha’ alifahamu kuwa Richmond ilikuwa kampuni ya kitapeli?
Kudai kuwa serikali na Lowassa hawakujua kuwa Richmond lilikuwa genge la walaghai, na hivyo kuwaachia matapeli wa kila rangi kufanya watakavyo, ni kuidharaulisha serikali kwa viwango vya juu mno.
Katika taarifa yake kwa Shirika la Habari la Associated Press (AP) la Marekani, anayetajwa kuwa mmiliki wa Richmond Mahammed Gire anasema, “Si sisi, wala yeyote kati ya watumishi wetu, hakuna aliyepokea sarafu nyekundu au kulipwa chochote, kutoka serikali ya Tanzania au kwa ofisa yeyote wa kampuni yetu.”
Anasema, “Badala yake tumekuwa tukishuhudia kauli za uongo na madai potofu juu yetu,” inasema taarifa ya kampuni hiyo.
Je, Waziri Mkuu Lowassa hana wasaidizi? Kwa nini alishindwa kuwasiliana na Mohammed Gire, aliyetajwa kuwa mmiliki wa Richmond na kujua ukweli wa jambo hili?
Je, kama yote haya aliyajua, lakini alishindwa kuyasimamia kwa dhati, kwa nini watu wanajihangaisha kutaka kumsafisha?
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ikulu, Salva Rwenyemamu amethibitisha kuwa anamfahamu aliyekuwa anadaiwa kuwa “mwenye” Richmond, mtu mmoja aitwaye Gire.
Salva anakiri kuwa alitambulishwa kwa mtu huyo na Rostam Aziz ambaye alikiri pia kuwa ni rafiki yake. Vipi Lowassa alishindwa kuwasiliana na rafiki yake sana, Rostam Aziz kuhusu suala hili?
Kutokana na maelezo hayo ya Salva ambayo hayawezi kutiliwa mashaka, ni wazi kuwa Rostam anaijua vema kampuni ya Richmond.
Na kwa kuwa Lowassa na Rostam ni chanda na pete, hakuna mwenye ubavu wa kumficha mwenzake jambo.
Hivyo haiingii akilini kwamba Rostam angeweza kumdanganya Lowassa juu ya Richmond, hadi Lowassa aharibikiwe kwa kiwango hiki.
Kwa kiongozi kama Lowassa kukubali kuidhinisha mamilioni yote hayo ya shilingi kwa kampuni hewa, ni lazima kuna jambo limejificha.

(Wiki ijayo, katika safu hii, tutajadili: je, Kamati ya Bunge, ilitosha kuishia hapo ilipoishia? Bunge halikustahili kutoa maelekezo zaidi kwa serikali?)

Mwisho

1 comment:

Anonymous said...

safi Said