Wednesday, February 20, 2008

Lowassa alang'oka hivi



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KULIKUWA na vikao mbalimbali. Hivi vya “kumwokoa” Lowassa na vile vya “kumwangamiza,” mithili ya mashabiki wa kandanda.

Ndani na nje ya kumbi za Bunge, minyukano na mivutano kati ya wafuasi wa Lowassa na wapinzani wake, ilikuwa ni ya wazi kabisa.

Kila upande ulijitahidi kuweka mkakati wake. Wakati “wafuasi” wa Lowassa walijitahidi kuzima hoja ya Kamati, wapinzani wake walijipanga kuhakikisha ripoti ya Kamati inawasilishwa na inajadiliwa.

Kosa kubwa ambalo wafuasi wa Lowassa walifanya, ni kuwatosa Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha kabla ya mjadala kuanza.

Wafuasi wa Lowassa, waliongozwa na Katibu Mkuu wa CCM Yusuph Makamba, mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, mbunge wa Songea Mjini Emmanuel Nchimbi na mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Wengine walikuwa Mbunge wa Nyamagana, Laurance Masha na mbunge wa Kigoma mjini, Peter Selukamba. Wote hao walipita huku na kule kushawishi wabunge kukubaliana na hoja ya kuzima ripoti ya Kamati Teule ya Bunge.

Wakati hilo likifanyika, wapinzani wao waliwatumia Karamagi na Msahaba, ili kuhakikisha Lowassa anaangamia.

Ni wapinzani wa Lowassa walioshinikiza Karamagi na Msabaha kung’ang’ania kuwa kuna mipango ya kutaka “kuwatoa kafara kwa ajili ya Lowassa. ”

Hivyo Karamagi na Msabaha wakatakiwa kusema “kila kitu” kilichotokea katika mchakato wa zabuni ya Richmond ili kujiondoa katika tope.

“Pamoja na kwamba hata wao wasingesalimika, lakini ukweli angalau ungejulikana. Ni tishio hilo, lililomsukuma Lowassa kuachia ngazi mapema,” mbunge mmoja kutoka kambi iliyokuwa inampinga Lowassa aliliambia MwanaHALISI.

Kuna taarifa kwamba kambi ya Lowassa haikufahamu mkakati huo mapema. Ndiyo maana Selukamba alisimama bungeni kutaka Bunge lisijadili taarifa ya kamati kwa madai kwamba Lowassa hakuhojiwa.

Wapo wanaoweza kusema kwamba Lowassa alijua kitakachotokea, ndiyo maana aliamua kujiuzulu kabla ya mjadala kuanza.

Lakini ukweli ni kwamba, Lowassa hakujua mapema. Angejua, ni dhahiri asingesubiri mjadala uanze.

Akiwa amepewa nafasi ya kuwa mzungumzaji wa kwanza, Lowassa alishindwa kulieleza Bunge kile ambacho alitarajiwa kukieleza katika Kamati Teule, hasa kuhusiana na madai yake kwamba Kamati haikumpa nafasi ya kujitetea.

Badala yake, Lowassa alilalama na kushutumu kamati kwa kusema, “…nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili,” akidai kuwa hakuhojiwa na Kamati.

Kauli ya Lowassa ilifadhaisha watu wengi makini. Walijiuliza, “Kama huyu analalama, kwa nini hakutumia nafasi hiyo kujitetea bungeni?”

Wakati hayo yakitokea, wapinzani wa Lowassa walijenga hoja imara kujibu mapigo ya mashabiki wa Lowassa na hata Lowassa mwenyewe.

Hoja ya Selukamba, ilivunjwa kwa ustadi mkubwa na mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, mbunge wa Karatu Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka na mbunge wa Nzega, Lucas Selelii.

Akijibu hoja ya Lowassa, Selelii kwanza alimtaka Lowassa kuthibitisha baadhi ya madai yake dhidi ya Kamati.

Alitishia asipofanya hivyo basi atatumia Ibara ya 63 (8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kuliomba Bunge limchukulie hatua.

Kuhusu hoja kwamba barua ya Lowassa ya utetezi haikuwasilishwa kwenye Kamati, Selelii alisema walipokea barua hiyo 28 Januari 2008, wakati Kamati ilishawasilisha taarifa yake kwa Spika wa Bunge.

“Kama mchezo huo (akiwa na maana ya kughushi) unafanyika sehemu nyingine, kwa kamati teule hii iliyoongozwa na mwanasheria aliyebobea, wajumbe makini wenye nia njema na taifa hili na sektarieti yenye usiri mkubwa na uaminifu wa hali ya juu, mchezo huo usingewezekana,” alisema Selelii.

Hoja ya Selelii iliungwa mkono na Kilango ambaye alikuwa akichangia kwa uchungu, alimshutumu waziwazi Lowassa kwa kutaka kulipotosha Bunge.

Aliwashutumu viongozi wa serikali kwa hatua ya kusaini mkataba huo na kulitia aibu taifa.

“…ndugu zangu, Karamagi, Msabaha, Lowassa na Mwanasheria Mkuu wa serikali, yote haya yaliyosemwa ni ukweli mtupu, hakuna udaku hapa,” alisema Kilango.

Hilo la magazeti ya udaku lilikuwa limesemwa na Lowassa pale alipopewa nafasi ya kwanza kujadili hoja. Alisema Kamati imechukua taarifa kutoka “magazeti ya udaku.”

Hoja ya Kilango ilifanana kwa kiwango kikubwa na hoja ya Sendeka, ambaye alisema kila kilichozungumzwa ni cha ukweli.

Sendeka alifika mbali zaidi na kutaka wahusika wafikishwe mahakamani na wafilisiwe.

Hakuishia hapo. Sendeka alitaka hata Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), hasa kiongozi wake mkuu, Edward Hosea, awajibike kutokana na kulidanganya taifa kuhusu kampuni ya Richmond.

Kutokana na hali hiyo, uwezekano wa Lowassa kujinasua katika kitanzi kilichotabiriwa na MwanaHALISI jana yake, ulikuwa haupo.

Tayari ilishaonekana kuwa uwezekano wa Lowassa kujiokoa na kuokoa wenzake, ulikuwa finyu sana.

Bali kwa hakika, Lowassa ametafunwa na mengi na kuandamwa na mengi. Baadhi ni ya bayana na mengine inawezekana amepakaziwa ili kuhalalisha azima ya kumuondoa.

Kwa mfano, kulikuwa na hata madai ya Lowassa kutaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Lakini kilichokuwa wazi, Lowassa ametafunwa na makundi ndani ya chama chake. Kila mwenye akili tumamu anajua jinsi makundi ya mtandao asilia, mtandao matumaini na anti-mtandao, yalivyokitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Na Lowassa ni zao la makundi katika chama chake. Kupatikana kwa wingu la Richmond kulisaidia kukuza mitafaruku miongoni mwa makundi na mateka wa kwanza akawa Lowassa.

Ni minyukano ndani ya CCM iliyosababisha Lowassa atungwe jicho mapema na haraka, kwani kuna wengine wengi ambao wangeanguka naye haraka.

Kwa mfano, tungeona wengi waking’olewa akiwamo Andrew Chenge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daud Ballali na Yusuf Manji mwenye tuhuma lukuki kuhusiana na biashara tata iliyoshirikisha Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

“Lowassa ametafunwa na mengi. Kuna hili la madai ya kutaka kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Lakini pia alikuwa na mvutano na Spika wa Bunge, Samwel Sitta,” kilisema chanzo kimoja cha habari ndani ya CCM.

Kilichotokea Dodoma, 7 Februari 2008 tayari kilikuwa kimebashiriwa na gazeti hili toleo la 6-12 Februari 2008.

Hata kilichofuatia hakikuwa kigeni. Gazeti hili liliwahi kuandika, tena mara nne, kwamba Rais Kikwete angefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.

mwisho

No comments: