Wednesday, February 20, 2008

Kikwete lilia taisa, si Lowassa

JK lilia taifa, si Lowassa


RAIS Jakaya Kikwete anajaribu kubadili upepo wa kisiasa. Anasema kilichosambaratisha baraza lake la mawaziri, baada ya Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu ni ajali ya kisiasa.
Kwamba Lowassa amepata ajali ya kisiasa ndiyo maana akajiuzulu.
Kikwete alitoa kauli hiyo, alipokuwa akihutubia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam wiki iliyopita.
Tunajua kwamba Lowassa hakuwa Waziri Mkuu tu kwa rais Kikwete, bali rafiki wa karibu.
Viongozi hawa wametoka mbali kisiasa, wameishi katika harakati mbalimbali na hata kupanga mikakati ya kushika madaraka ya dola. Hatimaye walifanikiwa.
Kwa maana hiyo tunajua rais anaweza kuwa na uchungu kwa haya yaliyomfika rafiki yake.
Inaweza ni kutokana na kuanguka kwa kishindo kibaya.
Pamoja na yote hayo, tunaomba kauli zinazotamkwa hadharani ziwe za kiungwana katika suala hili.
Hakuna ubishi kwamba Lowassa alilazimika kuwajibika kwa kuachia ngazi. Lakini mwenyewe alisema ndani ya Bunge kwamba ameachia ngazi kwa sababu nongwa imekuwa ni uwaziri mkuu.
Lowassa alishindwa kukiri kwamba katika usimamizi wake wa kazi alijikuta ametumbukia kwenye sakata la Richmond, ambalo limeigharimu taifa mabilioni ya shilingi.
Lowassa hakutolewa kafara. Lowassa aliwajibika kwa matendo na maamuzi yake kama kiongozi wa nchi.
Alijikuta hana pa kutokea kwa sababu katika uwanja wa siasa za uwazi na ukweli au tuseme panapostawi demokrasia, Lowassa alikuwa hana njia nyingine ya kufanya isipokuwa, kuachia ofisi ya umma.
Kwa kiwango cha tuhuma ambazo zimewaandama viongozi waandamizi wa serikali ya awamu ya nne, ilikuwa ni jambo la kushangaza Kikwete kupata kigugumizi cha kushindwa kuvunja baraza la mawaziri.
Ndiyo maana sisi tunasema kwamba kama Kikwete anaonyesha mbele ya umma kuwa Lowassa ameonewa, anaweza kusababisha hisia mbaya kutoka kwa wananchi.
Kiongozi mkuu wa dola yanapotokea matetemeko makubwa kabisa ya kisiasa kama hili la Richmond, busara na hekima inapaswa kuongoza.
Kutoa kauli na matamko yanayokinzana na ukweli, kunaweza kusababisha kiongozi mkuu kutoeleweka vema.
Ni vema Kikwete akafahamu hana sababu ya kumlilia Lowassa, bali anapaswa kulilia Taifa hili linalohujumiwa na wasaidizi wake aliowateua.
mwisho

2 comments:

Anonymous said...

Look here

Anonymous said...

Sorry. Look please here