Wednesday, February 20, 2008

JK alimtosa LowassaKikwete alimtosa LowassaRAIS Jakaya Kikwete aliafiki kutoswa kwa waziri mkuu wake, Edward Lowassa, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema Rais Kikwete aliweka wazi msimamo wake wa kutaka Lowassa kung’oka wakati “wafuasi” wa Lowassa wakiwa katika hatua za mwisho za kumwokoa na jinamizi la Richmond.

“Ndiyo kulikuwa na juhudi kubwa za kutaka kumuokoa Lowassa. Lakini baada ya msimamo wa ‘bwana mkubwa’ kujulikana, wote walisalimu amri,” kimeeleza chanzo cha habari cha gazeti hili.

Msimamo wa Kikwete ulijulikana pale alipokutana na wajumbe watatu wa Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao walitumwa kwake kumweleza maamuzi ya kamati hiyo kuhusu ripoti juu ya Richmond.

Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM ilikutana baada ya mkutano wa wabunge wote wa chama hicho kushindwa kufikia maamuzi.

Kushindwa kufikia maamuzi kulitokana na mambo mawili makuu: kutokuwepo kwa Lowassa kujieleza na kuwepo kwa mvutano miongoni mwa wajumbe, hawa wakitaka Lowassa “ajiuzulu” na wengine wakisema “asijiuzulu.”

Ni katika hatua hii, Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM iliamua kufanya kikao chake na kupitisha maamuzi ambayo walipeleka kwa Rais Kikwete.

Waliokwenda kumwona rais ni Yusuph Makamba, katibu wa kamati ya wabunge wa CCM, Ali Ameir Mohammed na mbunge wa Mtera, John Malecela.

Wajumbe hao watatu walikuwa wanawakilisha Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM.

Wajumbe wa kamati hiyo ni wajumbe wote wa Kamati Kuu (CC), Katibu wa wabunge wa CCM, Mwenyekiti (Waziri Mkuu), wenye viti wa kamati za bunge wanaotoka CCM.

Lakini katika kikao hiki Lowassa alitolewa nje ili ajadiliwe na baada ya hapo aliitwa ndani.

Mjumbe mmoja wa kikao cha wabunge alithibitishia gazeti hili kwamba, ndani ya kikao kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya wajumbe waliokuwa wanamtetea Lowassa na wale waliokuwa wanampinga.

Katika kikao hicho, mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, alisimama imara kuhakikisha Lowassa anachia ngazi.
“Tunataka mkija kesho asubuhi mje na Lowassa akiwa tayari amejiuzulu. Vinginevyo, sisi kama Bunge, tutamfukuza ili kuiokoa serikali isiabike na kumtoa rais wetu katika tope la Richmond,” alisema mbunge mmoja wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa Viktoria, akimnukuu Sendeka.
Mbunge huyo alisema kwamba, inawezekana ni kauli ya Sendeka iliyomwamsha Malecela na kubaini hatari ya chama na serikali kugawanyika, iwapo kamati ya uongozi ingeng’ang’ania kumlinda Lowassa.
Ni katika Kamati ya Uongozi, Malecela alitoa ushauri wa Lowassa kuachia ngazi, ambao hata hivyo, ulipingwa vikali na baadhi ya wajumbe wakiongozwa na Emmanuel Nchimbi na Andrew Chenge.

Juhudi za Lowassa kujinasua dakika za mwisho, zilikuwa zimechukua sura mpya kwa kumwita Dodoma, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba aliyekuwa Kiteto, Arusha akiendesha kampeni za uchaguzi mdogo.

Aidha, mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz aliingia mjini Dodoma, Jumanne 5 Februari, siku moja kabla ya ripoti ya Tume kuwasilishwa, akitokea nje ya nchi, kwa lengo la kuzima harufu ya jinamizi la Richmond.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, Makamba aliingia mjini Dodoma usiku wa manane wa Jumanne, akisindikizwa na polisi.

Hata hivyo, kilele cha juhudi zote za kumwokoa Lowassa asizame, na zile za kutaka kulinda chama na hadhi ya serikali, kiliwadia pale rais alipokutana na kamati ya wajambe watatu wa Kamati ya Uongozi ya CCM.

Taarifa zinasema msimamo wa Kikwete wa kuafiki kutoswa kwa Lowassa ulitokana na hoja zilizojengwa na Malecela, baada ya kuona kile kilichoitwa “hatari” ya kusambaratisha chama na taifa.

Awali Kamati ya Uongozi ya wabunge wa CCM iliwapa wajumbe wake watatu ujumbe wa kupeleka kwa rais uliotaka Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha “watoswe,” wakati huohuo “kuisema sana” serikali lakini kumtetea Lowassa kwa nguvu zote.

Mbele ya Rais Kikwete, mjumbe aliyewasilisha hoja ya kutoswa kwa mawaziri wawili na kulindwa kwa Lowassa, alikuwa Makamba. Mjumbe mwingine, Ali Ameir Mohamed, aliitikia na kukubali kuwa hayo ndiyo yalikuwa maazimio ya Kamati ya Uongozi.

Ndipo Rais Kikwete alimgeukia Malecela aliyekuwa amekaa mkao wa mashaka na kumuuliza, iwapo hayo yaliyosemwa na wenzake ndiyo walikuwa wamekubaliana na kuagizwa.

Habari za ndani zinasema Malecela alikubali kuwa hayo ndiyo waliyoagizwa, bali yeye alikuwa na mawazo tofauti.

Alimwambia rais kuwa mawazo yake ni kwamba, ama Edward (Lowassa) abebe mawaziri wake wote, waje mbele yako na kujiuzulu ili wakupe nafasi ya kuunda serikali mpya, au asubiri kufukuzwa na bunge.

Ilikuwa baada ya kauli ya Malecela, rais akirejea madai ya baadhi ya wabunge kuwa Lowassa hakupata nafasi ya kujieleza, aliwaambia wajumbe kwamba warudi na kumpa Lowassa nafasi ya kujieleza.

Hapa Kamati Teule ya Bunge ilikuwa imemaliza kazi yake ya kuchunguza na bunge lilikuwa limebakiwa na kazi ya kufanya maamuzi.

Kwahiyo kwa kauli ya rais ambayo ilionyesha kukubaliana na Malecela, na taarifa za ndani zilizosema rais alitamka pia kwamba kulikuwa na kazi kubwa ya kufanya kuliko taarifa alizopelekewa, rais alionyesha nia ya kufanya mabadiliko makubwa serikalini.

Kwa vyovyote vile, kama rais angependa Lowassa abakie serikalini, angechukua ushauri uliowasilishwa na Makamba.

Lakini hatua aliyochukua, ya kukubali kujiuzulu kwa Lowassa na kuvunja baraza la mawaziri, ilionyesha kuafiki mabadiliko kinyume na matakwa ya kamati ya uongozi ya CCM.

Wachunguzi wa mambo ya kisasa wanasema Kikwete alisoma nyakati badala ya kung’ang’ania ushauri ambao usingempa fursa ya kufanya mabadiliko muwafaka aliyohitaji katika utawala wake.

Alisema hatua hiyo ingefikiwa, basi rais, serikali na chama vingeabishwa. Aidha, serikali ingeweza kuingia katika matatizo makubwa kiuongozi, alisema.

“Unajua mzee huyu alishaona mbali. Aliona hatari ya chama kupasuka na Lowassa kuzama katika historia chafu,” kimesema chanzo cha habari.

Malecela alitoa ushauri mara tatu kwa Lowassa kujiuzulu. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye mkutano wa Kamati ya Uongozi wakati Lowassa akiwa ametolewa nje ili ajadiliwe.

Mara ya pili ilikuwa baada ya Lowassa kurejea kwenye kikao na mbele yake; na mara ya tatu ilikuwa mbele ya rais.

Malecela alinukuliwa na mpasha habari akisema, “Ili kuondoa majungu, ninaurudia msimamo wangu mbele yako (Lowassa)… Katika hili una njia mbili tu: Ama ubebe mawaziri wako wote uende mbele ya rais ujiuzulu, au usubiri Bunge likufukuze.”

Taarifa zinasema baada ya kauli ya Malecela na Kikwete, kilichokuwa kimebakia ni ama kushinikiza Bunge lisijadili “Ripoti ya Mwakyembe,” au Lowassa kukubali kujiuzulu.

Bunge katika Mkutano wake wa Tisa, liliunda Kamati Teule kuchunguza mkataba kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Kamati hiyo iliongozwa na mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe. Kufuatia uchunguzi huo, Lowassa alijuzulu pamoja na mawaziri wawili.
Bunge limeitaka serikali kutekeleza mapendekezo yote ya kamati teule na tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameaunda kamati ya utekelezaji wake.

mwisho

No comments: