Tuesday, January 29, 2008

Zakia Meghji, anamdanganya nani?

Zakia Meghji anamdanganya nani?

Na Saed Kubenea

WAZIRI wa Fedha, Zakia Meghji, amejidhalilisha. Hakujidhalilisha yeye peke yake; amedhalilisha hata serikali anayoitumikia.
Ni kutokana na hatua yake ya kuwaandikia wakaguzi wa hesabu akisema dola za Marekani 30.7 milioni zilizolipwa kwa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, zililipwa kwa ajili ya matumizi nyeti ya serikali.
Septemba 15, mwaka 2006, Meghji aliwaandikia maodita wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini akisema ni serikali iliyolipa Kagoda.
“Kama unavyofahamu vema, mamlaka ya serikali huwa na siri, vilevile haja ya kugharamia matumizi ya busara.
“Kwa hiyo... malipo ya dola 30,732,658.82 za Marekani yaliyofanywa na BoT kwa Kagoda Agriculture Limited, yaliidhinishwa na serikali kugharamia matumizi yake nyeti na ilikuwa lazima kuchukua hatua hii ya kudumisha usiri huu.”
Hakuishia hapo. Alisema, “Hatua iliyochukuliwa na serikali katika mazingira hayo, inaendana na matakwa ya sheria za Tanzania.”
Hakuna ubishi kuwa hatua ya Meghji ya kukubali kuandika barua ya kuisafisha Kagoda bila ya kwanza kuelewa ukweli wake, inapunguza hadhi na heshima yake kwa umma na kwa yule aliyemteua.
Meghji ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kamati Kuu (CC). Hawezi kuibuka leo na kusema kwamba alidanganywa na Daudi Ballali (aliyekuwa Gavana wa BoT) juu ya matumizi ya fedha hizo.
Ndani ya CC ndiko mipango ya siri ya serikali na CCM hupangwa. Huko ndiko inadaiwa pia kuwa hata wizi wa kura hujadiliwa na kuandaliwa.
Hivyo basi, ilitarajiwa na wengi kuwa Meghji angekuwa makini. Hii inatokana na ukweli kwamba ni yeye anayeaminika zaidi kwa mteule wake, Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa zinazosambazwa na wafuasi wa kundi la mtandao zinamtaja Meghji kuwa ni mmoja wa “mawaziri vipenzi” kwa Kikwete.
Taarifa zinafika mbali zaidi. Zinadai kuwa chaguo la kwanza la Kikwete katika kuteua mgombea mwenza katika uchaguzi wa mwaka 2005, lilikuwa Meghji. Haya yanasemwa wazi na bila ya kificho.
Ni vigingi vya wazee, wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, Benjamin Mkapa, vilivyozuia Meghji kushika nafasi hiyo.
Ndani ya Kamati Kuu, Mkapa na wenzake wanadaiwa kupinga mpango wa Kikwete wa kumtaka Meghji kuwa mgombea mwenza.
Walitaka na walisisitiza kuwa nafasi hiyo iendelee kushikwa na Dk. Ali Mohammed Shein.
Hoja ilijengwa ikisema kuwa uzoefu wa Dk. Shein utaweza kumsaidia Kikwete katika kujenga serikali imara na iliyo bora.
Kwamba kumuacha Dk. Shein nje ya uongozi, kutaiongezea serikali mzigo mwingine, kwa vile itailazimu kumhudumia kama kiongozi mstaafu, wakati bado anazo nguvu za kutumikia taifa.
Hata “uzanzibari” wa Meghji ulijadiliwa. Baadhi walidai kuwa Meghji amekuwa mno mtu wa bara na haonekani tena kuwakilisha Zanzibar.
Kama haya ni ya kweli, basi Mkapa na wenzake waliona mbali zaidi. Leo hii, Kikwete angekuwa na mzigo mwingine mkubwa wa kumbeba makamu wake.
Tayari mawaziri kadhaa wameonekana kupwaya. Wengine badala ya kutumikia wananchi, wanazitumia nafasi walizopewa kujitajirisha.
Mifano ya mawaziri na wasaidizi wa aina hiyo ni mingi. Wengi wao, badala ya kumsaidia Kikwete wanazidi kumtokomeza. Meghji ni mmoja wao.
Tayari tumeona “makamu wa rais aliyetarajiwa” akishindwa kusimamia Wizara ya Fedha.
Hatua yake ya kukiri hadharani kuwa alidanganywa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, juu ya matumizi ya mabilioni ya shilingi, inaonyesha jinsi asivyo makini.
Katika barua yake hiyo, Meghji wala hakujihangaisha kueleza matumizi ya fedha hizo, na hakutaja hizo shughuli “nyeti za serikali” alizodai kuwa ndiko fedha zilitumika.
Badala yake, anang’ang’ania kusema kuwa barua hiyo iliandikwa na Ballali na yeye aliweka saini yake tu. Kwa maana nyingine, waziri anakuwa muhuri wa kuidhinisha hata asiyoyaelewa!
Kauli hiyo inaonyesha hakujishughulisha kuisoma barua aliyopewa kuisaini, akiamini tu alichoelekeza kifanywe au barua yake ya pili inayokana ile ya kwanza, ni “feki.”
Hata baadhi ya maneno yaliyomo katika barua yake ya awali, yanaonekana wazi kupingana na yale yaliyomo katika barua ya pili.
Kwa mfano, katika ibara ya pili ya barua hiyo, Meghji anasema, “Kwa hivyo basi, kama nilivyozungumza nanyi kwa kirefu, malipo ya Dola 30,732,658.82 kwa Kagoda na BoT yaliamriwa na serikali na kutumika na serikali kugharamia matumizi nyeti ya serikali.”
Kwa maneno hayo, inaonyesha moja kwa moja kuwa hoja ya awali ya Meghji kwamba alidanganywa au “alichomekewa” na Gavana Ballali, haina mashiko.
Barua yake inadhihirisha kuwa suala la “matumizi nyeti ya serikali” katika malipo ya fedha hizo halikuwa geni kwake.
Kwa hakika, Meghji alishiriki katika mjadala huo kwa kina na analifahamu jambo hilo kwa mapana yake. Alivyo mweleedi, haikubaliki kuwa hakujua alichokuwa akikifanya.
Jambo hili linaleta hisia kwamba alikuwa anafanya jambo ambalo alikuwa analifahamu vema.
Kama ombi la kuandika barua hiyo lingetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, au Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman, au Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, angalau lingeeleweka.
Lakini hatua yake ya kukubali ombi la Ballali kuandika barua na yeye kukubali kuisaini, inazidi kumuingiza katika lindi la tuhuma za ufisadi.
Meghji haraka angejiuliza: “Hivi Ballali na usalama wa taifa wapi na wapi?”
Ukiacha hilo, katika barua hiyo, Meghji anasema katika ibara ya tatu kuwa hakuna malipo mengine ya fedha yaliyoidhinishwa kutoka BoT katika kipindi cha kuanzia Julai Mosi, mwaka 2005 hadi 30 Juni, mwaka 2006.
Haijafahamika lengo la Meghji la kuingiza maneno hayo katika barua yake lilikuwa nini hasa, lakini tutasema lililenga kuilinda Kagoda na makampuni mengine yaliyoshiriki kuangamiza uchumi wa nchi.
Je, ni kweli hakukuwa na malipo mengine katika kipindi hicho? Au alikuwa anamaanisha hakukuwapo malipo mengine yanayohusu “matumizi nyeti ya serikali?” Hii ni hoja nyingine isiyopata majibu ya Meghji.
Kama ni hivyo, kwa nini hoja ya “matumizi nyeti” ihusishwe na malipo ya Kagoda tu, na siyo malipo yaliyofanywa kwa makampuni mengine yaliyokwishathibitishwa na wakaguzi kuwa yameghushi nyaraka?
Au, kuna ukweli kwamba Meghji alikuwa anajua nani analipwa katika Kagoda na hivyo hakuona sababu ya kuzuia malipo hayo?
Kama si hivyo, kipi basi kilimsukuma Meghji kuchukua hatua hiyo ya nguvu ya kuikingia Kagoda kifua?
Alichotakiwa Meghji, ni kusikiliza hoja ya Ballali. Kisha kuwasiliana na Ikulu (kupitia Katibu Mkuu au hata Rais mwenyewe), Idara ya Usalama wa Taifa (Intelligence), Mkuu wa Majeshi (CDF) ili kujiridhisha na maelezo ya gavana.
Meghji anadai kwamba wakati Ballali ‘anamchomekea’ juu ya uhalali wa matumizi ya fedha hizo, Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja hakuwapo nchini, ndiyo maana alishindwa kuhakiki ukweli wa madai ya Ballali.
Hii ni hoja dhaifu sana. Je, kama alikuwa hajui alichokuwa anataka kufanya, kulikuwa na uharaka gani wa yeye kusaini barua hiyo bila ya kwanza kuwasiliana na Mgonja?
Je, huko alikokuwa Mgonja ni mbali gani katika dunia ya leo ya simu za mkononi au barua pepe kiasi cha kutopatikana ili amuondolee mashaka Meghji?
Kama yote hayo yalimkwaza Meghji kupata mawasiliano, anataka kusema kuwa Ofisi ya Mgonja ilifungwa na wasaidizi wa wake hawakuwepo?
Kama haikufungwa, nyaraka hazikuwapo? Je, Mgonja si anao manaibu katibu wa kumsaidia kazi? Hawakuwepo? Mbona Meghji hakuwasiliana na wasaidizi hawa wa Mgonja kutafuta ukweli?
Au Meghji alikuwa bado anafanya kazi kwa mazoea katika serikali mpya iliyokataa mtindo huo?
Kama angewasiliana na Mgonja au wasaidizi wake, angeweza kujua kwa uhakika kama Ballali alikuwa mkweli au alikuwa anadanganya.
Lakini kubeba maandishi ya Ballali kama yalivyo, kunamuonesha jinsi asivyo makini katika mambo nyeti kama vile walivyoshawishi wapinzani wake.
Mwaka 2006 Meghji aliwahi kuandika barua kwa mashirika ya fedha ya kimataifa juu ya kuwapo kwa ongezeko la bei ya umeme nchini lakini baada ya vyombo vya habari kuripoti suala hilo, alikana kufanya hivyo.
Lakini alipoonyeshwa barua yake iliyopatikana katika mtandao, alibaki kutafuna maneno.
Ni Meghji anayedaiwa kuhusika katika kufoji ripoti ya ukaguzi ya hesabu za BoT ya mwaka 2005-2006.
Ametajwa kuhusika na ugawaji holela wa vitalu vya uwindaji wakati akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii; hata familia yake ilitajwa kumiliki baadhi ya vitalu vilivyopatikana kwa mgongo wake.
Kwamba Meghji hakuandika barua hiyo, na badala yake alisaini tu barua iliyoandikwa na ofisa wake, ni jambo linaloelezeka.
Wakati Meghji anasema mabilioni ya shilingi yaligharamia “kazi ya siri ya serikali,” Gavana Ballali aliwaambia maodita haohao kuwa fedha hizo zilitumika kulipa madeni ya kampuni mbalimbali za kimataifa zilizokuwa zikiidai serikali ya Tanzania.
Kama Meghji alikuwa na nia njema, alipaswa kutilia mashaka kauli ya Ballali na kufuatilia hatua kwa hatua kile alichoelezwa.
Hii inatokana na ukweli kwamba fedha zilizokuwa zinatajwa ni nyingi; ni fedha za walipa kodi na washirika wa maendeleo.
Lakini pili, kubwa zaidi, ni: Balali (kama kweli alimueleza Meghji hivyo), mbona hakumuonyesha Meghji barua kutoka serikalini iliyomuagiza kuchota fedha hizo na kuipa Kagoda?
Je, Meghji hakuona umuhimu wa kuonyeshwa barua hii? Au anataka kutuaminisha kuwa serikali inatenda kazi zake kwa maagizo ya mdomoni?
Lakini Waswahili husema, maandiko matakatifu yalibashiri tangu awali kuwa hakuna lililofichika ambalo haliwezi kufichuliwa.
Kagoda imefichuka. Tayari imefahamika kuwa haikuwa kampuni, bali genge la wahuni waliojikusanya kwa lengo la kufilisi nchi.
Kwa hakika, kama uongo huu haukuwa umepangwa kwa pamoja kati ya Ballali na Meghji, basi Meghji alitakiwa kusoma nyaraka zote zinazohusu kampuni ya Kagoda.
Huko angegundua jinsi wajanja hawa walivyofanikiwa kucheza karata zao na kuchota mabilioni ya fedha kama kufumba na kufumbua.
Katika kipindi kifupi, Kagoda iliweza kuingia mkataba wa dola 30 milioni na wadai mbalimbali nchini Ujerumani, Italia, Yugoslavia, Uingereza, Ufaransa, Marekani na Japan.
Meghji angeona jinsi kampuni hiyo ilivyosajiliwa kitapeli kwa muda mfupi, huku ikiwa haina anuani inayofahamika.
Angeona hata mahali panapotajwa kuwa ofisi za Kagoda, pasivyotambulika kwa serikali yenyewe.
Jambo moja la wazi hapa ni kuwa Meghji hana sababu tena ya kuendelea kung’ang’ania ofisi za umma wakati ameshadhihirisha kuwa hana uwezo wa kushika nafasi hiyo.
Na laiti angekuwa anazingatia uwajibikaji unaosisitizwa kila wakati, tayari angekuwa amejiuzulu.
Hata hivyo, kinachoshangaza wengi ni hatua ya Kikwete ya kushindwa kumuwajibisha, au hata kumfukuza.
Kwa Kikwete kushindwa kufanya hivyo, naye anaweza kujikuta anakuwa sehemu ya tatizo. Ni vema rais abadilike. Atangulize maslahi ya umma.
Vinginevyo, itafikirika kwamba rais aliamua, kwa makusudi, kuweka waziri wa fedha mbumbumbu ili wakubwa waweze kuchota fedha watakavyo.
Hakika utetezi wa Meghji ni kama kuchotea maji kwenye pakacha. Hauingii akilini.

Mwisho

No comments: