Thursday, November 29, 2007

MONGELLA ATAFUNA MAMILIONI

Na Saed Kubenea

RAIS wa Bunge la Afrika, Gertrude Mongella, anatuhumiwa kutenda makosa ya kukosa uaminifu, wizi na utoaji ajira kinyume cha taratibu, imefahamika.
Kuhusu wizi, Mongella anatuhumiwa kutafuna zaidi ya dola za Kimarekani 138,000 sawa na shilingi 180milioni za Tanzania, mali ya Bunge la Afrika – Pan African Parliament (PAP).
Taarifa za kuaminika kutoka mkutano wa wakuu wa Umoja wa nchi za Afrika (AU), uliofanyika Ghana mwezi uliopita zinasema viongozi wa nchi hizo walitoa agizo kwa Mongella “kurudisha fedha hizo mara moja.”
Taarifa zinasema agizo hilo kali lilitolewa katika kikao ambacho Rais Jakaya Kikwete alihudhuria.
Kuhusu kukosa uaminifu, Mongella anatuhumiwa kulipwa mamilioni ya shilingi na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kazi za Bunge la Afrika, lakini papohapo akawa analipwa na bunge la Afrika kwa kazi ileile ambayo Bunge la Jamhuri limemlipa.
Katika tuhuma ya utoaji ajira, Mongella anatuhumiwa kuajiri jamaa zake ndani Sekretarieti ya Bunge hilo, kinyume cha taratibu. Imeelezwa kuwa mmoja wa waajiriwa wake ni mkwe wake.
Sekretarieti ya Bunge la Afrika tayari imeanza uchunguzi kuhusu tuhuma za ajira. Uchunguzi kuhusu tuhuma za kulipwa katika mabunge yote mawili, tayari umekamilika.
Taarifa za hivi karibuni zimeeleza kuwa mkwe wa Mongella, ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, amesharejea nchini baada ya uchunguzi kuanza.
Mbunge mmoja mashuhuri katika Bunge la Afrika alithibitisha kurejea nyumbani kwa mkwe huyo wa Mongella, lakini alisema hamkumbiki vizuri jina lake.
“Ndiyo. Na hivi ninavyozungumza na wewe, tayari mhusika amesharejea nchini. Amefanya hivyo siku chache baada ya uchunguzi kuanza,” alifafanua.
Mbunge huyo wa Ukerewe, mkoani Mwanza, anatuhumiwa pia kujilipa dola za Marekani 800 kwa kila siku anazofanya kazi katika bunge la Afrika, huku akiwalipa jamaa zake aliowaajiri dola za Marekani 400 kwa siku.
Katibu wa Bunge la Jamhuri, Damian Foka, alithibitishia MwanaHALISI juzi Jumatatu, kwamba “amezisikia” tuhuma hizo dhidi ya Mongella.
Hata hivyo, Foka alisema ofisi yake haijajulishwa rasmi na ofisi ya Bunge la Afrika au ofisi ya Katibu Mkuu wa AU juu ya hatua za kuchukua.
“Nililisikia jambo hili nilipokuwa Afrika Kusini. Lakini nilipomuuliza mwenyewe (Mongella), alisema ni uwongo mtupu. Alisema, ‘wananisingizia hawa. Wananizushia tu jamani,’ ” alisema Foka akimnukuu Mongella.
Foka alikiri kwamba Bunge la Tanzania limekuwa likimlipa Mongella fedha zote anazostahili wakati akifanya kazi za Bunge la Afrika.
Alisema kwa kufanya hivyo, ofisi yake haikuwa inakiuka taratibu, bali ilikuwa inatimiza wajibu wake na makubaliano na Bunge la Afrika.
“Wakati Bunge hili linaanza, tuliombwa na viongozi wa AU tuwalipie wabunge wanaoingia katika bunge hilo gharama zote wanazostahili,” alisema Foka.
Alisema kwa sauti ya upole, “Nami nimekuwa nikitimiza wajibu huo. Nilikuwa nikiwalipa wabunge wetu, akiwamo mama Mongella, stahili zao zote.”
“Kama kuna mtu amelipwa mara mbili, wanaostahili kuulizwa ama ni mama Mongella mwenyewe, au waliomlipa. Maana nijuavyo mimi mama Mongella na wenzake wote wanaotoka Tanzania tayari walishalipwa na mabunge yao,” alisema.
Taarifa kutoka Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika, zinasema bunge la SADC lilijulishwa juu ya tuhuma zinazomkabili Mongella, na hatua ambazo zimechukuliwa hadi sasa.
“Ni kweli kwamba mama Mongella anatuhumiwa kwa makosa ya udanganyifu, wizi na upendeleo katika utoaji ajira. Jambo hili lililetwa katika Bunge la SADC kama taarifa,” alisema mbunge huyo ambaye hakupenda kutajwa jina.
Tayari ukaguzi umefanyika na ripoti ya ukaguzi imekabidhiwa kwa Sektarieti ya Afrika. Kampuni iliyofanya ukaguzi ni KP GM ya Nairobi, Kenya.
“Kinachosubiriwa sasa ni kukabidhiwa kwa wakuu wa nchi husika. Unaweza kupata habari zaidi iwapo utawasiliana na Janguo (Athumani Janguo). Yeye anaweza kujua yalipofikia hadi sasa,” alisema.
Athumani Janguo Janguo ni mbunge wa Kisarawe, mkoani Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja wa wabunge wa Tanzania katika bunge la AU.
Mkutano wa Bunge la SADC ulifanyika nchini Malawi 20 Oktoba mwaka huu.
MwanaHALISI ilipowasiliana na Athumani Janguo alisema, “Siyafahamu kwa undani. Kama suala hilo lililetwa ni baada ya mimi kuondoka. Mimi nilirejea nyumbani mapema kutokana na matatizo ya msiba.”
Mbunge mwingine katika bunge hilo, James Wanyancha (Serengeti-CCM), alikubali kwamba mama Mongella anakabiliwa na tuhuma hizo.
Hata hivyo, Wanyancha alilitaka MwanaHALISI kutoandika habari hizo kwa madai kwamba zitaharibu sifa ya Tanzania machoni mwa jamii ya kimataifa.
“Ni kweli, lakini ndugu yangu uwe mzalendo. Haya mambo yatamharibia mama na tunaweza hata kupoteza huu urais katika bunge hili,” alisema Wanyancha kwa hali ya msononeko.
Alisema, “ Mongella si peke yake aliyelipwa mara mbili. Weka maslahi ya taifa mbele… angalia tuendako.”
MwanaHALISI lilipowasiliana na Mongella, juzi Jumatatu, saa 3:12 asubuhi kuhusiana na tuhuma hizo, alisema kwamba hawezi kuzungumza kwa vile yupo katika gari anakwenda Morogoro.
“Niko njiani nakwenda Morogoro. Siwezi kuzungumza na wewe,” alisema Mongella, mara baada ya kutakiwa kusema lolote juu ya tuhuma zilizoelekezwa kwake.
MwanaHALISI haikuchoka kumtafuta Mongella. Iliwasiliana naye tena saa 10:17 jioni, lakini alisema hawezi kuzungumza na waandishi wa habari bila kuwa na ahadi nao.
“Huwezi kujua niko wapi? Ninyi ni watu wa ajabu sana. Naweza kuwa na watu muhimu na mkutano muhimu. Siwezi kuzungumza. Nenda ofisi ya Bunge ukaweke ahadi ya kukutana na mimi,” alisema Mongella.
Hata gazeti hili lilipomsisitizia kwamba ni vema atoe kauli, Mongella aliendelea kung’ang’ania, “Nimeshakwambia nenda ofisi za bunge. Huelewi?”
Mongella ni mmoja wanawake mashuhuri nchini. Mwaka 1995 alikuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake duniani uliofanyika Beijing nchini China.


Makala haya yamechapishwa katika gazeti la MwanaHALISI la 28 Novemba, 2007.

Mwisho


Makala haya

2 comments:

Anonymous said...

Mama Mongella, acha hayo. Du. Ufisadi mpaka ulaya?

Anonymous said...

Mama Mongella acha hayo. Ufisadi mpaka nje ya nchi? Unaona unavyoliabisha taifa?