Friday, October 5, 2007

WATAFUNA NCHI HAWA HAPA


STORY hii ilitoka katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 63, mwaka huu.
Na Saed Kubenea
RAIS Jakaya Kikwete na rais mstaafu Benjamin Mkapa ni miongoni mwa viongozi 11 ambao wapinzani wametaja kuwa wamefilisi nchi kwa kile kilichoitwa “vitendo vya ufisadi.”
“Ama wameruhusu, au wameidhinisha, au wamenyamazia, ufujaji wa mamilioni ya fedha za umma,” viongozi wa upinzani wameeleza jijini Dar es Salaam.
Pamoja na Kikwete na Mkapa, ni Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Gavana wa Benki Kuu (BoT) Daudi Balali, mawaziri Basil Mramba, Andrew Chenge na Nazir Karamagi.
Wengine ni Mweka Hazina wa CCM, Rostam Aziz, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Gray Mgonja, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Patrick Rutabanzibwa na Wakili maarufu Nimrod Mkono ambaye sasa ni mbunge wa Musoma Vijijini.
Hii ni mara ya kwanza kwa upinzani kuanika majina ya wale wanaoitwa “vigogo” na kuwahusisha na ufujaji wa fedha na shitaka kali la kufilisi nchi.
Mbele ya umati mkubwa, kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, viongozi walisoma jina moja baada ya jingine na kulitolea maelezo juu ya kila mmoja anavyohusika.
“Hii sasa ni mahakama ya umma. Tena wameleta kumi na mmoja kama first eleven ya kandanda. Hapa wana maana kuna timu B na C na D…” alisema mzee Seleman Kahugwa, shabiki maarufu wa moja ya timu kubwa jijini.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilibrod Slaa na mwanasheria wa chama hicho Tundu Lissu ndio walitangaza majina ya “watuhumiwa” Jumamosi iliyopita.

Benjamin William Mkapa: Kwa mujibu wa upinzani, ufisadi mkubwa ulitendeka chini ya utawala wake. Kwa msingi huo Mkapa “anawajibika moja kwa moja, ama kwa kubariki au kunyamazia” ufisadi huo.
“Zaidi ya hayo, kuna ushahidi unaoonyesha kwamba wakati akiwa madarakani alishiriki moja kwa moja, au kwa kutumia ndugu na/au washirika wa karibu wa familia yake, katika ufisadi mkubwa na uliolipotezea taifa fedha nyingi,” upinzani umeeleza.
Inadaiwa kuwa Mkapa alitumia wadhifa wake kuhakikisha kwamba kampuni iitwayo Tanpower Resources Limited inamilikishwa asilimia 85 ya hisa za kampuni ya Kiwira Coal Mines Ltd inayochimba mkaa wa mawe huko Kiwira, Mkoani Mbeya. Hisa zilizobaki asilimia 15 zinamilikiwa na serikali.
Tanpower Resources inatajwa kama kampuni iliyoanzishwa kwa ajili ya kuinufaisha familia ya Mkapa na washirika wake wa karibu na kwamba taarifa zilizoko Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), zinaonyesha wakurugenzi wa kampuni hiyo ni Anna Mkapa, Nicholas Mkapa, Joseph Mbuna, Daniel Yona na Joseph Mapundi.
Ripoti ya Dk. Slaa inasema Anna ni mke wa Mkapa, Nicholas ni mtoto wake, Mbuna ni wakili wa kujitegemea na baba mkwe wa Nicholas, Yona ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati Mkapa akiwa rais.
Hivi sasa Tanpower Resources ina mkataba wa kuuza umeme kwa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO).
“Mkataba huo utanufaisha kampuni ya Kiwira Coal Mines Ltd., na Mkapa, familia na washirika wake wa karibu kwa kiasi cha dola za Marekani 271 milioni kwa wakati wote wa mkataba huo,” imeelezwa.

Jakaya Mrisho Kikwete: Anatajwa kuhusika na kusaini “mikataba mibovu” ya madini na makampuni ya kimataifa, iliyosababisha upotevu wa utajiri mkubwa na kuifanya serikali ishindwe kuhudumia vizuri wananchi wake.
Inadaiwa Kikwete aliingia mkataba na kampuni ya SAMAX Limited iliyopewa leseni ya kuchimba dhahabu katika eneo la Lusu, wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora, mradi ulioleta mateso kwa maelfu ya wachimbaji wadogo baada ya kuondolewa kwenye makazi yao kwa nguvu.
SAMAX iliuza mradi wake Ashanti Goldfields ya Ghana kwa kiasi cha dola za Marekani 253 milioni. Nao Ashanti waliuza mgodi huo kwa kampuni ya Resolute Limited ambao ndio wanamiliki mgodi wa Golden Pride ulioko Lusu, Nzega uliofunguliwa Novemba 1998.
Kikwete anadaiwa pia kuingia mkataba na kampuni ya Kahama Mining Corporation Ltd (KMCL) ambayo ni kampuni tanzu ya Sutton Resources ya Canada.
Mara zote wananchi waliswagwa nje ili kupisha wawekezaji na hawakulipwa fidia kwa mali zao. Takriban wananchi 400,000 waliokuwa wakiishi na kuchimba dhahabu katika eneo la Bulyanhulu, Kahama waliachwa bila makazi.
Baadaye Sutton iliuza KMCL na Bulyanhulu kwa kampuni ya dhahabu ya Barrick Gold Corporation ya Toronto, Canada kwa dola 280 milioni. Leo hii Bulyanhulu ni moja ya migodi tajiri kwa dhahabu katika Bara la Afrika.

Edward Lowassa: Ametajwa kuhusika na kashfa ya kampuni ya City Water iliyopewa uendeshaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) mwaka 2002.
Mwanasheria Tundu Lissu aliyefafanua dai hilo alisema kwa ufupi, anajua “kilichomo katika mkataba na kwanini anamtuhumu Lowassa kuwa mhusika katika kadhia hiyo.”
Lissu ni mmoja wa mawakili wa serikali katika shauri la City Water kwenye Mahakama ya Kimataifa nchini Uholanzi ambayo inashughulikia usuluhishi wa mgogoro unaotokana na kukatishwa kwa mkataba wa City Water.
Kabla ya kukatishwa mkataba, Citywater walikwishasababisha hasara ya dola 12.5 milioni hivyo kuthibitisha onyo lililotolewa na Benki ya Dunia mapema juu ya uwezo duni wa kampuni hizo.
Lowassa anatajwa pia kwa kuhusika kwake na kashfa ya kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC) iliyopewa zabuni ya kuzalisha megawati 100 za umeme wa dharura mwaka jana.

Nazir Karamagi: Anahusishwa na mkataba wa madini kati ya Serikali na kampuni ya Barrick katika mradi wa Buzwagi, wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga.
Karamagi anatuhumiwa kukaidi maoni ya Kamati ya Ushauri ya Madini ambayo ilimtaka asisaini mkataba wa Buzwagi hadi hapo serikali itakaporekebisha sheria na sera ili ipate mapato zaidi.
Imebainika Karamagi alisaini kabla Kamati hiyo haijabadilisha chochote katika mkataba huo, vikiwemo Sera na Sheria ya madini; jambo ambalo linaonyesha mazingira ya rushwa.
Aidha, Karamagi alitoa kauli zisizo sahihi bungeni kwamba alikuwa katika msafara wa Rais Kikwete wakati alikwenda Uingereza kwa shabaha ya kusaini mkataba.
Mara zote katika wasilisho, Dk. Slaa na Tundu Lissu walisisitiza kwamba viongozi hao “wanastahili
kuitwa wahalifu kwa kuwa wamekiuka Katiba ya nchi.”

Gavana Daudi Balali: Ametajwa kama mhujumu taifa kwa kuidhinisha na kufumbia macho ufujaji wa mali za umma unaofikia Sh. 522, 459,255,000 kupitia mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya BoT jijini Dar es Salaam na Gulioni huko Zanzibar.
Upinzani unamtuhumu Balali kuhusika katika kashfa nyingi. Kuna kashfa ya hongo ya dola 5 milioni kutoka kampuni ya Skanska Jensen ya Sweden iliyosababaisha kampuni hiyo kupigwa marufuku kushiriki zabuni ya ujenzi wa majengo ya BoT.
Lakini kampuni ya Group 5 ya Afrika Kusini inayotajwa kama kampuni tanzu ya Skanska Jensen, ndiyo ilipewa zabuni hiyo.
Kuna madai ya Balali kuidhinisha na/au kuruhusu na/au kunyamazia malipo ya dola za Marekani 118,396,460.36 zilizopelekwa katika akaunti isiyojulikana ya Benki ya Nebank Ltd ya Afrika ya Kusini kama malipo ya madeni ya kampuni muflisi ya Meremeta Ltd., iliyokuwa inachimba dhahabu Buhemba, wilaya ya Musoma.
Mradi wa Meremeta umejaa utata unaotokana na usajili wake na wamiliki wake halali. Nchini umekuwa ukitajwa kuwa wa Jeshi la Ulinzi uliokuwa na jukumu la kuendeleza mradi wa uunganishaji magari wa Nyumbu, Kibaha, Pwani.
Hata hivyo, taarifa ya BRELA ya Mei 31, 2005 inaonyesha Meremeta Ltd ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania kama tawi Oktoba 3, 1997 ikithibitisha kuwa hisa 50 za Maremeta Ltd zilikuwa zinamilikiwa na kampuni ya Triennex (Pty) Ltd ya Afrika Kusini na hisa 50 zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania.
Vilevile Balali anatuhumiwa kuruhusu au kuidhinisha au kunyamazia malipo ya dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kampuni ya Tangold Ltd., kwa nadai kuwa ni ugharimiaji wa “mali na madeni ya Meremeta Ltd yaliyohamishiwa kwenye kampuni mpya ya Tangold ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.”
Hata hivyo, imefahamika kuwa Tangold Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Mauritius na baadaye kuandikishwa nchini Tanzania kama tawi la kampuni ya kigeni.”
Wakurugenzi wa Tangold Limited, kwa mujibu wa taarifa zilizoko BRELA, ni pamoja na Daudi Balali. Gray S. Mgonja, Andrew J. Chenge, Patrick W.R. Rutabanzibwa na Vicent F. Mrisho.
“Kuna utata. Kifungu 7(e) cha Katiba ya Tangold Ltd, kinaruhusu hisa za wanaomiliki kampuni hiyo kuhamisha hisa zao kwa wanandoa, baba, mama, watoto, wajukuu au wakwe zao wa kike au wa kiume.
“Sasa kama ni kweli kwamba Tangold Ltd inamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100, je nani ni mke au mume au mama au mtoto au mjukuu au mkwe wa kike au wa kiume wa Serikali ya Tanzania ambaye anaweza kuhamishiwa hisa za kampuni hiyo,” wapinzani wamehoji.
Gavana Balali anatajwa kuwa aliruhusu na au kuidhinisha na au kunyamazia mkopo usio na riba wa dola za Marekani 5,512,398.55 kwa kampuni ya Mwananchi Gold Corp. Ltd., uliotolewa kati ya 2004 na Juni 30, 2006.
Kati ya fedha hizo, deni la dola 2,807,920 limedhaminiwa kwa dhahabu ghafi ambayo ingenunuliwa kutokana na fedha za mkopo zilizotolewa na Benki Kuu yenyewe.
Hii ina maana kuwa kampuni ya Mwananchi Gold haijatoa dhamana yoyote inayoeleweka kwa mabilioni ya shilingi ilizokopeshwa na Benki Kuu chini ya Gavana Balali.
Kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkazi Mkuu (CAG), hadi kufikia Desemba 2006 Mwananchi Gold Co. Ltd., ilikuwa imeshindwa kulipa hata riba ya mkopo huo kwa kiasi cha dola 62,847.91.
“Katika mazingira haya”, inasema barua ya CAG, “hatukuweza kujiridhisha kwamba deni la dola za Marekani 5,512,398.55 inalodaiwa hadi kufikia Juni 30, 2006 linaweza kulipika.”
Vipi kampuni inapewa mamilioni ya fedha za umma katika fedha za kigeni bila ya kudaiwa riba au kupewa kipindi maalum cha kulipa mkopo huo, wameshangaa wapinzani.
Kufuatana na taarifa za BRELA, Mwananchi Gold Co. Ltd., ni kampuni binafsi ambayo wanahisa wake ni Benki Kuu ya Tanzania yenye hisa 500, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) (hisa 500), Mwananchi Trust Co. Ltd (hisa 1,123) na Chimera Co. Ltd (hisa 500).
Kampuni hiyo ilisajiliwa kama kampuni binafsi Desemba 12, 2002 na mawakili wake ni kampuni ya uwakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu Associates ikiwashirikisha Francis L. Nyalali, Waziri Mkuu wa zamani Joseph Sinde Warioba na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa R. Mahalu.
Kwa mujibu wa BRELA, wakurugenzi wa Mwananchi Gold Co. Ltd ni Joseph Sinde Warioba, Gavana Daudi Balali, Col. J. Simbakalia, Vulfrida Grace Mahalu, Yusuf H. Mushi na raia wawili wa Italia, Paolo Cesari na Patrizio Magrini.
Balali pia anatajwa kuwa aliruhusu na au kuidhinisha na au kunyamazia malipo ya Sh. 131,950,750,000 kwa watu wasiojulikana wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini. Pia anadaiwa kuidhinisha malipo ya Sh. 4,228,658,000 kwa watu wasiojulikana wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini.
Nayo CAG inanukuliwa ikisema, “hatukuridhika na uhalali wa hasara ya Sh. 131.9 bilioni zinazoonekana katika taarifa za fedha hadi kufikia Juni 30, 2006.”

Andrew Chenge: Anatajwa kuhusika na ufisadi kwa kuwa kwa katika wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliwajibika kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu mambo yote ya kisheria na kutekeleza shughuli nyinginezo zenye asili ya, au kuhusiana na, sheria.
Aidha, Chenge anatajwa kuwa amehujumu taifa kwa kuwa Mkurugenzi katika kampuni ya kigeni ya Tangold Limited iliyoshiriki na/au kufaidika na malipo haramu ya dola 13,736,628.73.
Kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chenge alishiriki kuishauri vibaya au kutoishauri vizuri BoT na wizara nyingine za serikali ambazo ziliingia katika mikataba mibovu.
Vituko vya kuuza dhahabu ya thamani ya dola 2,340 bilioni na serikali kuambulia mrahaba wa bilioni 72, au mauzo ya dola 2.6 bilioni na serikali kumegewa 78 bilioni, vilifanyika kutokana na kukosekana kwa ushauri wa mwanasheria mkuu wa serikali.

Basil Pesambili Mramba: Anatajwa kwa kushinikiza kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya Washington DC, Marekani, kupewa kazi ya kukagua hesabu za makampuni ya uchimbaji dhahabu.
Chini ya mkataba wake na Serikali kampuni hiyo inalipwa asilimia 1.9 kati ya asilimia 3 za mrahaba inaolipwa Serikali na makampuni ya madini ya dhahabu.
Kufuatana na barua ya CAG, mwaka 2005/2006, Alex Stewart (Assayers) walilipwa Sh. 14,175,753,189.46 kama malipo ya ukaguzi wa hesabu za kampuni za dhahabu japokuwa hakuna ripoti za ukaguzi zilizowasilishwa na wakaguzi hao kwa mwaka huo.
Hapa kuna madai ya kuwepo rushwa kuhusiana na mkataba wa Alex Stewart (Assayers). Barua pepe inayodaiwa kuandikwa Novemba 14, 2006 na Erwin Flores ambaye ni Makamu wa Rais Mtendaji wa kampuni hiyo, inadhihirisha hivyo.
Barua hiyo inamtaja mtu mmoja mwenye jina la Bwana Basil ambaye ana wadhifa wa Waziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuwa yeye pamoja na “wenzake” wana asilimia 12.5 za hisa kwenye kampuni hiyo na kuwa analipwa na kampuni hiyo.
Mramba alipoitwa saa 11.20 jioni ya Jumatatu, kuthibitisha iwapo ni yeye aliyetajwa katika barua pepe, alijibu kwa yuko Marekani na kutaka mwandishi aongee na maofisa wake.
Alipoambiwa kuwa ni suala linalomhusu yeye binafsi, alinyamaza kwa muda na baadaye kukata simu.
Mramba amehusishwa pia na ufujaji na/au matumizi mabaya ya fedha za umma na uuzaji holela wa raslimali za taifa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa rada ya kijeshi, ununuzi wa ndege ya Rais na ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na National Micro-finance Bank (NMB).

Gray Mgonja: Anatajwa kuwa, kwa wadhifa wake pia ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania na anashikilia nafasi ya ukurugenzi katika kampuni ya kigeni ya Tangold Limited inayohusishwa na ufisadi pamoja na Gavana Balali na Chenge. Hapa anafungwa na mgongano wa maslahi.

Patrick Rutabanzibwa: Anahusishwa na hujuma kutokana na kuwa kwake Katibu Mkuu wa Nishati na Madini wakati mikataba mibovu ya madini inasainiwa, hasa kashfa kubwa ya IPTL (Independent Power Tanzania Limited).
Hivi sasa Rutabanzibwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na vilevile mkurugenzi katika kampuni ya kigeni ya Tangold ambayo tayari imehusishwa na kashfa.

Rostam Aziz: Anatajwa kutokana na mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Caspian, ambayo anamiliki, kuwa ndiye Mkurugenzi wa Kagoda Agricultural Ltd iliyosajiliwa Septemba 29, 2005 na ndani ya wiki nane ikapewa Sh. 30.8 bilioni kupitia mpango wa kufuta madeni ya taifa.
Wapinzani wanahoji kwamba mkurugenzi wa Caspian anayehusishwa na Kagoda ni mtu wa kawaida sana, jambo ambalo wanadai linaonyesha anavyotumiwa tu.

Nimrod Mkono: Anatajwa kwa kuwa barua ya CAG inabainisha kuwa Benki Kuu imekuwa ikilipa malipo makubwa kwa Mkono & Co. Advocates, hasa yale yanayohusu kesi ya Valambhia, ambamo BoT inadaiwa jumla ya Sh. 60 bilioni.
Kwa mujibu wa barua ya CAG, wanasema wapinzani, kampuni ya Mkono tayari imelipwa Sh. 8,128,375,237 fedha taslimu kwa kesi hiyo ambayo bado iko mahakamani.
Malipo hayo ni sawa na asilimia 13.5 ya deni lote inalodaiwa BoT. Hoja ya CAG ni kuwa kesi hiyo haina muda maalum wa kumalizika, hivyo inawezekana malipo ya wanasheria yakazidi kiasi cha fedha ambacho BoT inadaiwa.
Chini ya Kanuni za Malipo ya Mawakili na Uamuzi wa Gharama za Kesi za mwaka 1991, wamesema wapinzani (Tangazo la Serikali Na. 515 la 1995), kiwango cha malipo ya mawakili katika kesi ambazo fedha inayodaiwa ni zaidi ya Sh. 10 milioni, kitakuwa asilimia tatu.
Kwa kufuata masharti ya sheria hii, kampuni ya Mkono ilipaswa kulipwa Sh. 1.8 bilioni.
Kampuni ya Mkono inatajwa katika taarifa ya uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi ya makampuni ya Tanfarms Ltd., Makinyumbi Estates Ltd., Centrepoint Investments Ltd., na Arusha Farms Ltd., yanayomilikiwa na V. G. Chavda kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha za Debt Conversion Programme.
Taarifa hiyo iliyotolewa Bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, (marehemu) Edward Oyombe Ayila Novemba 1994 ilisema:
“Mhe Spika …ni vizuri nikaelezea juu ya uhusiano unaotia mashaka kati ya V. G. Chavda na mashamba yake na Subash Patel mwenye makampuni ya Deco Art, MM Motors, MM Garage, Hotel Sea Cliff, City Bureau De Change na Nimrod Mkono, wakili wa kujitegemea.
“(Mkono) ni Mkurugenzi katika makampuni ya Azania Agricultural Enterprises. Liberty Leather Shoe Ltd, Azania Eximco, n.k.”
Wapinzani wanamnukuu zaidi Ayila akiliambia Bunge: “Ni vigumu kabisa katika hali ya kawaida kwa mtu yeyote kuamini kwamba makubaliano haya na uhusiano uliojitokeza hapa haukuwa wa hila.
Wameendelea kumnukuu Ayila akisema, “Nimrod Mkono alikuwa Mkurugenzi wa kampuni ya Oxford Services Ltd. Na pia anamiliki kampuni ya Marcus Ltd., makampuni ambayo kwa pamoja yamefaidika kwa kupata jumla ya Sh. 4,477,870,279.61 chini ya utaratibu wa DCP.”
Dk. Slaa na Lissu ambao walikuwa wasemaji wakuu mkutanoni hapo waliwaomba wananchi waunge mkono upinzani na kwamba hiyo ndiyo ilikuwa shabaha ya kufichua maovu hayo.

Ends.

No comments: