Saturday, October 6, 2007

SERIKALI ITOKE USINGIZINI

Serikali itoke usingizini

JUMAMOSI iliyopita Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilibrod Slaa, alifuzu siasa za uwazi na kutoa somo kwa watawala na watawaliwa.
Dk. Slaa, msomi na mweledi wa mambo mengi, alipanda jukwaani, jjini Dar es Salaam, na bila woga wala aibu, akataja majina ya watu 11 waliomo katika nafasi za uongozi na kuwatuhumu kufanya vitendo vya “ufisadi.”
Alisema ana ushahidi. Akakomba hazina yake ya kile ambacho bila shaka aliandaa kwa muda mrefu. Akapaza sauti. Akakumbuka siyo wote ambao watafurahia atakachosema. Akawaomba wananchi wamsimame naye.
Katika orodha yake kuna rais mstaafu, rais aliyeko madarakani, mawaziri, makatibu wakuu, gavana wa benki, wafanyabiashara na wanasheria.
Kinga pekee ya kiongozi huyu, aliyekuwa akiongea kwa niaba ya ushirika wa vyama vya upinzani na umma wa Watanzania, ni ukweli. Na ukweli hauwezi kumsaliti.
Tunamfahamu Dk Slaa kuwa kiongozi makini; si mtu wa kukurupuka; si mpayukaji. Ni mwerevu na mwenye uwezo wa kujenga hoja na kubomoa hoja.
Tuaamini kwamba amefikia uamuzi wa kujenga hoja hadharani kwa sababu moja tu: Yeye, wenzake katika upinzani na umma wa Watanzania, wamechoka mtindo wa walioko madarakani wa kuzidi kulindana na kulea uoza.
Alichofanya ni kutaja majina na kutuhumu. Alichofanikiwa ni kuanika. Alichoibua ni mjadala. Alichochochea ni uzalendo na moyo wa kuthubutu. Ametenda wajibu wake.
Dk. Slaa, kwa taarifa alizoweka wazi, atawezesha wengi kuelewa kwamba umasikini wa nchi hii na watu wake, kumbe chanzo chake ni hapahapa. Chanzo chake ni baadhi ya watu wake. Chanzo chake ni sera na mipango ya walioko kileleni.
Kuingia mikataba mibovu ni kununua umasikini, tena kwa makusudi, na kuutawanya kwa wananchi huku walioununua wakineemeka kileleni kutokana na posho ziendanazo na makubaliano.
Kuruhusu watu wachache wakatumbua fedha na raslimali za nchi ni kupalilia umasikini, udhalili wa maisha na maangamizi ya jamii kiuchumi, kijamii na hata kisaikolojia.
Je, walioko madarakani wanaweza, angalau mara hii, kujifunza kwamba inafikia wakati watu wanachoka hila, dhuluma, uwongo na uzandiki, na wanataka mabadiliko?
Dk. Slaa na kambi nzima ya upinzani wameamua kupasua jipu. Ni kweli linaweza kuwa limetoa harufu mbaya. Lakini ni harufu mbaya ya jipu lenye usaha na siyo harufu ya mpasuaji.
Basi na serikali ikomae. Ijifunze, ama kupasua majipu au kukaa na wanaoyapasua ili kutafuta dawa yasiote tena.
Alichofanya Dk. Slaa na kambi yake kisaidie kila mmoja kupiga moyo konde. Serikali itoke usingizini. Iwepo kazini wakati wote. Mlinzi anayesababisha mali ya tajiri kuibiwa, anastahili kufukuzwa kazi.

No comments: