Tuesday, October 16, 2007

BARAZA LA MAWAZIRI KUVUNJWA


Na Saed Kubenea
RAIS Jakaya Kikwete huenda akalivunja Baraza la Mawaziri na hata kupunguza ukubwa wake kutokana na tuhuma za ufisadi zinazoikabili serikali, habari za kibalozi zimeeleza.
Habari ambazo MwanaHALISI imezipata zinasema kuwa Rais Kikwete hana mahali pengine pa kuanzia na penye uhakika katika kukabili tuhuma za ufisadi zinazoiandama serikali yake, isipokuwa kuunda safu mpya ya uongozi katika serikali.
“Hana njia nyingine ya kujisafisha na kusafisha safu za uongozi wake; atalazimika kuwaondoa marafiki zake na labda kuwapa kazi nyingine lakini aonekane anaitika kilio cha wananchi wengi na sehemu ya jumuiya ya kimataifa,” habari zimeeleza.
Rais Kikwete alirejea nchini Jumapili iliyopita kutoka ziarani Marekani na kukuta tuhuma nyingi zikikabili utawala wake huku usimamizi wa serikali ukitota.
Kauli za mabalozi wa nchi za nje walioko Dar es Salaam, zinazotaka serikali kujibu tuhuma za ufisadi, nazo zikiwa tayari zimeiweka serikali katika mtihani mgumu.
Hatua ya kuvunjwa kwa baraza la mawaziri inafuatia kauli ya Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliyetangulia kurejea nchini na kutoa msimamo wa Kikwete kwa taifa.
Alisema watuhumiwa wote wa ufisadi serikalini watachunguzwa na wale watakaobainika watachukuliwa hatua.
Tayari rais amefanya kikao cha dharura na washauri wake wakuu katika baraza la mawaziri ili kubaini mahali pa kuanzia kuleta sura mpya kwa utawala wake ambao hivi sasa unakaribia umri wa miaka miwili.
Aidha, kuna taarifa za vikao vya dharura vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kamati Kuu inakutana leo Jumatano na Halmashauri Kuu inakutana kesho Alhamisi jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza tangu Kikwete aingie madarakani kupatikana kwa taarifa juu ya uwezekano wa kuvunja baraza la mawaziri.
Mara ya mwisho Kikwete kufanya mabadiliko madogo katika baraza hilo ilikuwa karibu na mwishoni mwa mwaka jana ambapo mmoja wa walioteuliwa alikuwa Nazir Karamagi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, kutoka Viwanda na Biashara.
Karamagi alichukua nafasi ya Dk. Ibrahim Msabaha aliyeteuliwa kuwa Waziri wa masuala ya Afrika Mashariki.
Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam na Marekani alikokuwa ziarani, zinasema hatua ya kuvunja baraza la mawaziri inaweza kutekelezwa wakati wowote kuanzia sasa.
“Kwamba Rais Kikwete atavunja baraza lake, siyo tena suala la mjadala. Mjadala ni lini atafanya hivyo,” habari zimeeleza.
“Je, afanye hivyo sasa, au asubiri hadi baada ya uchaguzi mkuu katika chama chake? Lakini yote yanategemea shinikizo alilonalo katika kutafuta sura mpya kwa utawala wake,” taarifa za ndani zimeeleza zikinukuu hata baadhi ya wasaidizi wa rais.
Chama Cha Mapinduzi, kinafanya mkutano wake mkuu wa uchaguzi Novemba hii. Hadi tunakwenda mitamboni kulikuwa bado na mvutano iwapo mkutano huo ufanyike Dodoma ambako maandalizi yanaendelea au uhamishiwe Dar es Salaam.
Pamoja na uvunjaji baraza la mawaziri ili kupata timu mpya, taarifa zinasema rais anatarajiwa kufanya mabadiliko katika uendeshaji na usimamizi wa taasisi za fedha ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Sehemu nyingine ambako mabadiliko haya yanatarajiwa kufanyika ni katika ukusanyaji kodi ambako wahusika wakuu ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Hazina ambao ni wasimamizi wa utawala na matumizi ya fedha.
Maeneo mengine yanayotarajiwa kukumbwa na mabadiliko makubwa, sambamba na baraza la mawaziri ni uendeshaji na usimamizi katika wizara za Nishati na Madini na Miundombinu.
Wizara hizi mbili ndizo zenye mikataba mingi na mikubwa ya uchimbaji madini na ujenzi, ambako kumesheheni madai makubwa ya ufisadi.
Kwa mujibu wa habari hizo, baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri watapoteza nafasi zao. Wapya watateuliwa na wengine watabadilishwa wizara.
Miongoni mwa mawaziri wanaotajwa kwamba watatupwa nje ya baraza ni Nazir Karamagi ambaye amekuwa akiandamwa na tuhuma za ufisadi kuhusiana na mkataba wa madini kati ya Serikali na kampuni ya Barrick katika mradi wa Buzwagi, wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga.
Upinzani unamtuhumu Karamagi kukaidi maoni ya Kamati ya Ushauri ya Madini ambayo ilimtaka asisaini mkataba huo hadi hapo serikali itakaporekebisha sheria na sera ili iweze kuwa na mapato zaidi.
Imebainika kuwa Karamagi alisaini kabla Kamati hiyo haijabadilisha chochote katika mkataba huo, vikiwemo Sera na Sheria ya madini; jambo ambalo linaonyesha mazingira ya rushwa.
Aidha, Karamagi alitoa kauli zisizo sahihi bungeni kwamba alikuwa katika msafara wa Rais Kikwete wakati alikwenda Uingereza kwa shabaha ya kusaini mkataba.
“Huyu bwana (Karamagi) amejiingiza mwenyewe kwenye nyavu. Hawezi kujinasua. Hata rais analiona hili,” habari za ndani ya serikali zimeeleza.
Kuhusu ukubwa wa baraza la mawaziri, habari zinasema rais hawezi kuepuka kupunguza idadi ya mawaziri ambao wanachangia ongezeko lisilo la lazima la matumizi ya serikali.
“Kila mmoja anaona kuwa wingi wa mawaziri haulingani na kazi wanazofanya. Lakini wakati huohuo, matumizi yao yanaacha pengo kubwa katika matumizi ya serikali. Rais hawezi kuacha kurekebisha hili,” mtoa habari ameeleza.
“Mifano ni mingi. Chukua huu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo. Mawaziri watatu wa nini pale? Kazi za naibu mawaziri wawili zinaweza kufanywa na wakurugenzi au wakuu wa idara,” ameeleza mtoa habari.
MwanaHALISI ina taarifa kwamba karibu nusu ya naibu mawaziri hawatarejea kazini wakati mawaziri wapatao saba watatupwa nje.

Mwisho

2 comments:

Anonymous said...

Huyu jamaa anatisha.

Anonymous said...

Litavunjwa lini? Mbona halijavunjwa mpaka sasa?