Friday, October 5, 2007

MAKAMBA ASHINDWA KUMFUTA KIGODA


Makamba ashindwa kumfuta Kigoda

Na Saed Kubenea

KWA uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukataa kumlinda Katibu Mkuu wake wa zamani, Philip Mangula katika kinyang’anyiro cha uongozi mkoani Iringa, ni ishara tosha kwamba ulikuwa umemchoka.
Uongozi wa sasa wa CCM umemchukulia Mangula kama mmoja wa wanachama wa kawaida, na wengine wanasema huenda uliandaa mazingira ya maangamizi yake kisiasa.
Mangula alibwagwa na Diwani wa Makambako, Deo Sanga, maarufu kwa jina la Jah People.
Vyama ambavyo vinathamini na kuenzi viongozi wake waliovitumikia, ama huwalinda au huwashauri wasigombee ili chama kiendelee kuheshima.
“Mangula amethibitishiwa kuwa hatakiwi. Ni kama amefukuzwa katika chama. Madai kwamba ni demokrasia ndani ya chama ni kichaka cha kuficha njama zao,” amenieleza mmoja wa viongozi wa CCM wilaya ya Kinondoni jjini Dar es Salaam.
Alisema ukiona chama kimeanza kutupa nje makada wake, ujue kwamba kimeingiliwa na kinaelekea kwenye maangamizi.
Kada mwingine aliyetupwa nje ya uongozi wa chama chake ni Dk. Juma Ngasongwa; mwalimu wa siasa wakati huo Chuo Kikuu cha CCM Kivukoni na baadaye mwalimu Chuo Kikuu cha Kilimo, Sokoine, Morogoro.
Ngasongwa amebwagwa na mfanyabiashara Azizi Aboud. Huyu ni tajiri mwendesha mabasi ya abiria, kiwanda cha mafuta ya kula na viwanda vingine.
Pamoja na makada hao mashuhuri, ni wanachama maarufu ambao wameangushwa na wenye fedha au waliofadhiliwa na viongozi wakuu.
Wanachama wa kweli wa CCM bado wanajuliza na huenda wasitulie hadi wapewe sababu ya kuwatelekeza makada wa chama.
Katika mataifa yenye mfumo wa vyama, Katibu Mkuu wa chama ni mtu muhimu sana. Hata baada ya kuacha madaraka hubaki kuwa mtu wa heshima na muhimu kwa chama chake.
Ilionekana mapema kwamba Mangula alikuwa anafukuzwa kwenye chama mara baada ya Jakaya Kikwete kuchukua uenyekiti CCM na kuvunja Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Kuondolewa kwake kwenye kazi hiyo au kuchanganywa tu na wengine kwa madai kuwa ajitafutie nafasi kwa kugombea, ni kuweka utaratibu wa kutelekeza watumishi wa CCM utakaowakumba hata walioko madarakani hivi sasa.
Katibu Mkuu wa sasa wa chama hicho, Yusuf Makamba sharti aanze kuweka maji wakati anaona wenzake wananyolewa. Wakimchoka watamtupa na hata kumzibia fursa za kupata nafasi nyingine ya uongozi.
Kuanguka kwa Mangula kunasemekana kutokana uthabiti wake wakati wa kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005 ambapo alitaka taarifa ya Kamati ya Maadili ya CCM isomwe mbele ya Kamati Kuu.
Taarifa hiyo ilikuwa na maelezo juu ya wagombea urais wote wa chama hicho kuhusu mwenendo wao. Taarifa zinasema Jakaya Kikwete ndiye alikuwa amekaliwa kooni na kamati hiyo.
Lakini Mangula bado ana umri wa kushiriki siasa katika vyama vingine vya siasa kama angetaka kufanya hivyo na kama hajakata tamaa kabisa.
Yeye anasema hakushindwa katika uchaguzi huru na haki, bali ameshindwa katika uchaguzi uliotawaliwa na hila, rushwa, hadaa, na ghiliba.
Anafika mbali zaidi na kutahadharisha kwamba, kwa hali inavyokwenda, muda si mrefu kiongozi wa CCM atapatikana kwa njia ya mnada.
Haijulikani viongozi wa chama chake wameyachukulia kwa uzito kiasi gani madai hayo. Lakini bila shaka kwa wanavyofahamika, wameyapuuza.
Hata hivyo, sasa wengi wanajiuliza: Uchaguzi huu umekisaidia CCM, au umekipeleka kusikojulikana?
Maswali ni mengi na magumu. Hii ni kwa kuwa kila mahali kuna malalamiko ya wizi wa kura, kutoa rushwa, kupendelewa na mengine mengi.
Wapo wengine wengi wenye mashaka kwamba CCM kimeanza kuwakimbia wenye chama na kukumbatia matajiri. Wapo wanaodai kwamba chama kimemezwa na mtandao.
Kwa tathimini ya haraka ni kwamba, uchaguzi huu umefanya CCM kuzama kwa kasi katika mtaro. Chama kimehama kutoka kwa wakulima na wafanyakazi na kuwa chama cha matajiri wenye fedha nyingi.
Ni kweli, katika baadhi ya maeneo uchaguzi umekwenda vizuri, lakini katika maeneo mengine, kuna malamiko lukuki.
Hali ni mbaya zaidi katika mkoa wa Kilimanjaro, ambapo mmoja wa wagombea alikataa matokeo akidai kwamba Waziri Mkuu Edward Lowassa, alielekeza upigaji kura.
Tayari mgombea huyo, Sammy Ngassa, amekataa kusaini matokeo na kukata rufaa kupinga matokeo hayo katika ngazi za juu za chama chake.
Lakini ukiacha hilo, kila kona ya nchi kuna malalamiko ya kuwapo kwa vitendo vya rushwa, hadaa, ghiliba na matumizi mabaya ya madaraka.
Vitendo hivyo vimefanywa hadharani; baadhi ya wagombea tayari wamelalamika. Wapo waliolalamika kwa siri na wengine kwa uwazi.
Katikati ya yote hayo, baadhi ya wagombea ambao tuliwatabiria ushindi wameshinda. Kwa mfano, mwenyekiti wa Mkoa wa Kagera, Constancia Buhiye, ni mmoja wa waliotabiriwa ushindi.
Katika mfululizo wa uchambuzi wangu nilisema ni Constancia Buhiye, aliyekuwa akipewa nafasi ya kuwatoa jasho Alhaji Ahmed Lugusha na Alhaji Adam Khalid Kahahuza. Hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Katika mkoa wa Ruvuma, nilisema kwamba Geofrey Mhagama amechoka na atashindwa. Ndivyo iliyotokea.
Lakini nilitabiri kwa kuangalia mwenendo wa siasa kwamba Janesta Mhagama atapata ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Ndivyo ilivyotokea. Vivyo hivyo kwa Nsilo Swai wa Kilimanjaro.
Utabiri huo wa kisayansi umedhihirika pia katika mikoa ya Singida, Lindi, Pwani, Mtwara, Kigoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Tanga na Kilimanjaro.
Bali ukweli ni kwamba uchaguzi wa CCM umeingiza sura nyingi mpya ambapo wengi hawakushinda kwa kuwa ni makada au walikuwa wanakijua chama, au hata kwa uaminifu na uadilifu wao.
Sura nyingi mpya zimetokana na kuungwa mkono na baadhi ya vigogo serikalini na katika chama; au walikuwa na fedha za kununulia kura au fadhila.
Ni wanachama wachache sana walioshinda kutokana na uwezo wao binafsi usiohusishwa na fedha au kubebwa.
Bahati mbaya ni kwamba wengi walioshinda kwa hila hawana hata uwezo wa kushindana kwa hoja na diwani wa upinzani, achilia mbali mbunge.
Baadhi ni walanguzi waliojikita katika chama ili kukidhi matakwa yao. Wengine ni wale waliokwishazunguka vyama vyote vya siasa kama George Guninita na Haji Sunday Manara.
Guninita amepata uenyekiti wa mkoa wa Dar es Salaam na Manara amekuwa Katibu Mwenezi mkoani humo.
Huku CCM imekumba wafanyabiashara wakubwa bila kujali imani yao na uthabiti wa uanachama wao. Huku kimezoa hata waliokwishakitukana na kukibeza.
Swali zito na kubwa ni hili: CCM kitaweza vipi kusalimika katika “mchanganyiko maalum” huku kikiachana na makada wake wa siku nyingi kwa sababu dhaifu?
Hata wanachama wake walioshinda, kama Profesa Mark Mwandosya aliyenyakua ujumbe wa NEC, Mbeya wamepita kwa mbinde.
Mwandosya alikuwa anapambana na mbunge wa kuteuliwa Tomy Mwang’onda, ambaye taarifa zimesema wakati wote amejinadi kuwa ametumwa na Rais Kikwete kuchukua nafasi hiyo.
Hakuna awezaye kutabiri kwamba Mwandosya ataweza kuwa na nia na moyo wa kutumika kama awali baada ya kuchoshwa na hata kujeruhiwa hapa na pale kisiasa kupitia kampeni za uchaguzi huu.
Mwandosya ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Alikuwa mmoja wa wanachama wa waliotaka kupitishwa na chama hicho kuwania urais mwaka 2000.
Mwang’onda ambaye ni mtoto wa mkurugenzi wa zamani wa usalama wa taifa nchini, Colnel Abson, amelazimika kusubiri hadi Mwandosya anastaafu naye awe anakomaa kisiasa.
Mwingine ambaye ni kada wa CCM aliyepita kwenye tundu la sindano, ni George Mkuchika, Mbunge wa Newala ambaye ametetea nafasi yake ya ujumbe wa NEC Mtwara.
Mkuchika alitarajiwa kushindwa kwa kuwa tangu awali alikataa kuingia kwenye mtandao wa Kikwete; ingawa wanao wafahamu wanajua kuwa walikuwa marafiki.
Ni msimamo huohuo uliomtuma Mkuchika kuingia kinyang’anyiro bila woga na kama mwanasiasa anayethubutu.
Hata hivyo, uchaguzi huu unazidi kuonyesha kwamba bado kuna vita kubwa ndani ya CCM kati ya kundi la mtandao na lile ambalo liko nje ya mtandao.
Mbali na Mkuchika na Mwandosya, aliyekuwa amezwe na mtandao ni Dk. Abdallah Kigoda ambaye naye ameukwaa ujumbe wa NEC mkoa wa Tanga.
Juhudi za Katibu Mkuu wa CCM, ambazo wafuatiliaji wa siasa za CCM wanasema zililenga kuziba mlango wa Kigoda, zimeshindwa na yeye kaibuka mshindi.
Dk. Kigoda, mbunge wa Handeni, ni mmoja wa wanachama wa CCM waliojitosa kuwania urais.
Mbali na kile kinachoitwa njama za kumwangusha katika uchaguzi ndani ya chama, Kigoda amechomolewa haraka katika uongozi wa serikali ya Kikwete.
Wakati wazoefu katika siasa za CCM Bara wanafunga majeraha ya uchaguzi, kule Zanzibar nako si shwari. Machachari ya Ali Juma Shamhuna yamezimwa.
Shamhuna, Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, alikuwa anagombea ujumbe wa NEC kupitia mkoa wa Kaskazini Unguja.
Shamhuna ni mmoja wa wanasiasa kinyonga. Katika madaraka yupo tayari hata kuasi ili mradi afanikishe adhima yake.
Ni Shamhuna aliyehama kambi ya Komandoo Dk. Salimin Amour na kujiunga na kambi ya Rais Amani Abeid Karume ambako baadaye alipewa uwaziri na kuanza kuisakama kambi ya Salmin.
Kwa kipigo cha sasa cha Shamhuna, matumaini yake ya kutaka kuwa rais wa Zanzibar sasa yamejikwaa.

kubenea@yahoo.co.uk
0784-440 073

No comments: