Friday, October 5, 2007

WAISLAMU WAMELOGWA NA NANI?


Waislamu wamelogwa na nani?

Na Saed Kubenea
“VICHWA visivyosikia nitavipiga marungu.” Hiyo ni kauli ya Shekh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaban bin Simba.
Aliitoa mwaka 2002 mara baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo. Uchaguzi wa Mufti ulifanyika kutokana na kifo cha Marehemu Hemed Bin Juma bin Hemed.
Kwa hakika, kinyang’anyiro cha uchaguzi ule kilikuwa na ushindani mkali kati ya Shekh Mkuu wa sasa, Mutfi Simba na Shekh Sulemani Gorogosi.
Uchaguzi ulifanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Biashara (CBE) mjini Dodoma. Bila shaka, si wengi waliomuelewa na wala si wengi walioelewa kauli halisi ya Mufti Simba.
Wengi walikuwa gizani. Lakini sasa ikiwa ni takribani miaka mitano tangu Shekh Simba achaguliwe kushika nafasi hiyo, wengi wameanza kumuelewa.
Kwamba kauli yake ya “Vichwa visivyosikia nitavipiga marungu,” iliwalenga “wanaolivuruga” Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Wakati huo, machoni mwa wengi, BAKWATA ilionekana kama chombo kilichopotea njia. Asilimia kubwa ya waislamu walikuwa hawaikubali.
Wengi waliona baraza hilo kama chombo cha serikali na chama tawala-CCM.
Baadhi yao walikuwa wanasema waziwazi kwamba BAKWATA imeingiliwa na serikali. Kipaumbele chake hakikujulikani machoni mwa waislamu wengi.
Maswali kama, BAKWATA inakwenda wapi au Baraza litafika kweli, yalikuwa yakisikika kila kona.
Mapambano kadhaa yalianzishwa kuipinga BAKWATA na viongozi wake. Kilikuwa ni kipindi cha harakati na hatua za kuikataa BAKWATA zilifika mbali.
Wanaharakati kadhaa walihubiri ubaya wa Baraza na kile lilichokiita “ndoa yake na serikali.” Hicho ndicho chanzo au kichocheo cha “mauaji ya Mwembechai.”
Kulikuwa na hata madai kwamba baadhi ya waislamu walipanga mapinduzi dhidi ya uongozi wa Baraza.
Mihadhara na makongamano vilifanyika usiku na mchana. Kila pembe ya nchi waislamu walisimama kulaani Baraza na kuituhumu serikali kwamba inawalinda viongozi wake.
Misikiti kadhaa ilianzisha harakati kwa madai kwamba BAKWATA imeshindwa kuutetea uislamu na waislamu kwa ujumla.
Wanaharakati mbalimbali walichipuka; wengine wakiwa na dhamira ya kweli na wengine wakiwa waganga njaa.
Baadhi yao wanafahamika hata kwa majina na matendo yao. Wote hawa walikuwa na madai yanayofanana kwamba BAKWATA imemezwa na serikali na imeshindwa kuutetea Uislamu.
Hata hivyo, watu makini waliyadharau madai hayo baada ya kuwapima watoa madai na matendo yao.
Wengi walijua tangu awali kwamba BAKWATA haikuingiliwa na serikali wala waumini wa dini nyingine; imeingiliwa na waislamu wenyewe.
Ni wale waliokuwa wanaitumia BAKWATA kujinufaisha. Baadhi yao wangalipo hadi sasa, lakini wengi wameondolewa.
Hakuna aliyejua au hata kufikiri kwamba Mufti Simba angeweza kuwang’oa ndani ya BAKWATA; baadhi ya viongozi walionekana kuwa kikwanzo kwa maendeleo ya uislamu.
Watu kama Ali Mubaraka, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA, Mussa Hemed, Naibu Katibu Mkuu Dini, Abas Kihemba na wengineo tayari walikuwa wameweka mizizi yao ndani ya baraza hilo.
Wapo waliondoka wenyewe baada ya kuona mambo yanakwenda kombo, lakini wapo wengi pia ambao wameondoka kwa kung’olewa na kimbuga cha Mufti Simba.
Kwa hakika, Shekh Simba amekuwa simba kweli. Amejitahidi kurudisha hadhi na heshima ya baraza hilo mbele ya jamii. Amefanikiwa japo si kwa kiasi kikubwa kurudisha umoja na mshikamano miongoni mwa waislamu.
Tayari sasa baadhi ya waislamu wanalikubali baraza lao. Wengi sasa wanajua kwamba adui yao mkubwa si serikali, wala madhehebu mengine, bali waislamu wenzao.
Na hili linathibitika sasa wakati mgogoro unaofukuta kati ya mfanyabiashara Yusuf Manji anayemiliki kampuni ya Quality Group na baadhi ya waislamu wakiongozwa na mwanaharakati mahiri, Shekh Khalifa Khamisi.
Kiwanja kinachogombewa ni Na. 311/1 kilichopo Kitalu T Chang’ombe, Dar es Salaam.
Taarifa zinasema kiwanja hicho kilimilikishwa kwa kampuni ya Quality Group na baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa BAKWATA, ambao tayari Mufti amewashughulikia.
Hadi sasa, haijulikani ni kiasi gani wale “wasaliti” walilipwa kwa kazi hiyo.
Linalofahamika ni kwamba watendaji hao, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Abass Kihemba, walifukuzwa kazi kwa madai ya kukiuka maadili ya kazi yao.
Hicho ndicho chanzo au kichocheo cha harakati na malalamiko ya sasa yanayoongozwa na Shekh Khalifa Khamisi.
Lakini kwamba aliyemilikishwa na waliomilikisha, wote ni waislamu, ni jambo linalodhihirisha kuwa BAKWATA na uislamu havivurugwi na serikali, bali na waislamu wenyewe.
BAKWATA ni moja ya taasisi ya kidini nchini iliyopata bahati ya kumiliki mali na vitegauchumi vikubwa.
Mwaka 1968 ilimilikishwa na serikali mali za iliyokuwa Taasisi ya Waislamu ya Afrika Mashariki (East Afrika Muslim).
BAKWATA ilirithi majumba, pamoja na vitegauchumi mbalimbali kwa dhamira kuendeleza uislamu.
Bahati mbaya hayo hayakufanyika. Kila mmoja anafahamu kwamba kama BAKWATA ingetumia mali na rasilimali zake vizuri, leo ingekuwa mbali kimaendeleo.
Kama raslimali zake zingetumika vizuri, waislamu wangekuwa juu. Wangepata elimu bila kutegemea msaada mkubwa kutoka kwa serikali. Na hata malalamiko yanayoenezwa sasa kwamba serikali imewasahau waislamu yasingesikika.
Lakini bahati mbaya ni kwamba waliopewa dhamana ya kusimamia mali na rasilimali za waislamu ndiyo haohao waliogeuka na kuzitafuna.
Wakati madhehebu mengine yako katika mbio kali za maendeleo, bado BAKWATA inatambaa.
Angalia madhehebu mengine yanamiliki Hospitari za rufaa (Bugando-Mwanza na KCMC-Moshi), BAKWATA imeishia kumiliki zahanati.
Wakati madhehebu mengine yanamiliki vyuo vikuu, kwa mfano Chuo Kikuu cha Tumaini mkoani Iringa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine – Nyegezi, Mwanza, BAKWATA imeishia kumiliki sekondari.
Kibaya zaidi, hata hizo sekondari na shule za msingi ilizonazo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu.
Nyingine hazina vitendea kazi, vikiwamo vitabu vya ziada na kiada; na nyingi zinaongoza kwa matokeo mabaya katika mitihani ya taifa.
Hata chuo kikuu pekee cha Morogoro (Muslim University of Morogoro), ambacho kilianzishwa miaka miwili iliyopita kwa msaada wa serikali, tayari kinayumba.
Chuo kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu na ucheleweshaji mishahara kwa wafanyakazi.
Hakina mitaala ya kutosha na wala hakina vitendea kazi vingine muhimu. Kwa kweli ni “bora chuo” na wala si chuo bora.
Yapo madai kwamba hata mandhari ya chuo kwa sasa hayavutii kama kilivyokuwa wakati kikiwa chini ya Shirika la Umeme TANESCO.


Mwisho

No comments: