Tuesday, October 16, 2007

KIFO CHA CCM KIWAZI

KATIKA ukurasa wa kwanza wa gazeti hili, kuna habari kwamba Mwenyekiti wa Chama Cha Mpinduzi (CCM) na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amekibinafsisha chama chake kwa matajiri.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku.
Butiku anasema, mpango wa Mkapa kukibinafsha CCM ulikuwa unajulikana kwa wajumbe wote wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC) ya
chama hicho.
Haya si madai madogo. Ni madai makubwa mno. Hii ni kutokana na ukweli kwamba malalamiko ya matumizi makubwa ya fedha, yametawala ndani ya CCM kwa miaka mingi sasa.
Kiini cha fedha hizo, ama kimekuwa uchotaji kutoka serikalini au kwa matajiri, au kwa njia zozote zile hata za kihalifu.
Ni nani asiyejua kwamba hata kesi za wauza madawa, wauza magogo nchi nje, na kesi nyingine kubwa za mabilioni ya Shilingi, hata zitakapokuwa zimefikishwa polisi, hazijulikani mwisho wake.
Nani ataamini kwamba matumizi ya viongozi wa chama, ambayo vyanzo vyake vya fedha havijulikani, hayawezi kutokana na njia hizo chafu za kuangamiza chama kilichoko madarakani sasa, kwa zaidi ya miaka 45.
Kilio cha Butiku ni kilio cha wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, na ni kilio cha wananchi kwa jumla. Ni kilio cha wananchi wote kwa sababu, wanaotoa fedha chafu, kwa matumizi machafu, ndiyo wanaotengeneza sera ambazo taifa zima linapaswa kuzifuata.
Anayetunza mcheza ngoma, ndiye achaguaye wimbo. Vivyo hivyo, kwa wanaolundika mamilioni ya Shilingi katika chama tawala.
Huu ni msiba wa CCM, wanachama wake na taifa kwa ujumla. Hili ni donda ndugu ambalo sharti ling’olewe hata ikibidi kukata mikono au miguu leo hii.
Na kwa kuwa viongozi wa CCM wa sasa wanalalamika kwamba hawana uwezo wa kufuatilia rushwa na ufisadi, ni jukumu sasa la wazalendo kujitokeza, ama kuelekeza jinsi ya kutoka katika matope haya, au kuiweka CCM upandeni na wenye kupenda nchi yao wakaiongoza.

ends

No comments: