Tuesday, October 16, 2007

TUHUMA ZA UFISADI: RAIS AKIKAA KIMYA NCHI ITATEKETEA

JUMATANO iliyopita, Rais Jakaya Kikwete, alijaribu kujibu tuhuma za ufisadi ambazo kwa mwezi mmoja sasa zimetawala anga ya Tanzania.
Alikuwa katika hafla ya kuchangia ujenzi wa hosteli ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Arusha.
Alisema katika siku za hivi karibuni, kumezuka tabia ya baadhi ya wanasiasa kujifanya dola; kupeleleza, kukamata, kuendesha mashtaka na kutoa hukumu.
Alionya kwamba tabia hiyo isipokomeshwa mara moja, inaweza kuleta athari mbaya katika mustakabli wa taifa.
Kauli ya Kikwete inatokana na kauli ya Dk. Willibrod Slaa kwamba viongozi 11 wameshiriki kufilisi nchi kwa “vitendo vya ufisadi.”
“Ama wameruhusu, au wameidhinisha, au wamenyamazia, ufujaji wa mamilioni ya fedha za umma,” walisema Dk. Slaa, mbunge wa Karatu (CHADEMA) na mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Temeke, Mwembeyanga, Dar es Salaam, mwezi uliopita.
Ukiangalia kauli ya Rais Kikwete kwa makini, utabaini kwamba hakulenga kujibu tuhuma; alilenga kutisha watoa tuhuma.
Kwa vyovyote vile, umma wa Watanzania ulitarajia kwamba rais angejitokeza na kujibu tuhuma zote hizo.
Hii inatokana na ukweli kwamba miongoni mwa waliotuhumiwa yeye ni mmoja wao. Hivyo kauli yake ilikuwa inahitajika ili kubaini ukweli au uwongo wa jambo hilo.
Pili, tuhuma dhidi ya rais, ni tuhuma dhidi ya serikali. Kutokana na hali hiyo, majibu ya rais katika jambo hili, yalikuwa yanahitajika.
Lakini hivyo sivyo ilivyokuwa. Badala ya kujibu tuhuma, rais alijitumbukiza katika kujaribu kunyamazisha mjadala na kutisha watoa tuhuma.
Kwanza, nani kamwambia Kikwete kwamba wapinzani wametoa hukumu, wanapeleleza na wanashitaki?
Kilichosemwa na wapinzani ni kwamba, kuna tuhuma za ufujaji wa fedha na maliasili ya taifa. Kilichosemwa ni kwamba kuna wizi na utumbuaji ovyoovyo wa fedha za wananchi.
Hicho ndicho kilichosemwa na wapinzani. Wapinzani hawajahukumu mtu. Wametuhumu.
Ni wajibu wa watuhumiwa kujitokeza hadharani na kujibu tuhuma dhidi yao. Ni wajibu pia wa serikali kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wahusika.
Lakini badala ya kufanya hivyo, rais anakuja na majibu ya jumla kwamba serikali yake inaifanyia kazi kila taarifa; na itachukua hatua.
Haya ni majibu ya jumla sana. Hayastahili kutolewa na Rais Kikwete. Ni majibu yaliyopaswa kutolewa na mtu ambaye alikuwa nje ya utawala.
Rais amekuwa ndani ya serikali tangu wakati wa utawala wa rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassani Mwinyi. Amekuwamo pia katika serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa.
Amekuwa mbunge katika jimbo la Bagamoyo na baadaye Chalinze. Amekuwa bungeni karibu miaka 20. Kwa nafasi yake ya uwaziri na ubunge, Kikwete alipaswa kuwa na uelewa juu ya tuhuma hizi.
Kwa kujifananisha na raia wengine wa kawaida, rais ana maana, ama ya kutaka kukwepa wajibu wake, au anataka “kuwabeba” watuhumiwa.
Haingii akilini kwa mtu yoyote kwamba rais mwenye kila chombo cha kumpasha habari, hajui lolote juu ya tuhuma hizi na uzito wake kwa jamii.
Je, Kikwete hafahamu kwamba Nazir Karamagi, aliyempa dhamana ya kusimamia madini ya umma, amekwenda Uingereza kusaini mkataba wa madini wa Buzwagwi?
Je, rais hafahamu kwamba, kabla ya Karamagi hajasaini mkataba huo, Kamati ya Ushauri ya Madini, iliukataa mkataba huo ikisema kusifanyike chochote hadi sera na sheria ya madini, ifanyiwe marekebisho?
Kikwete hafahamu kwamba, pamoja na mapendekezo hayo ya kamati, Karamagi amesaini mkataba huo wakati hadi anasaini na hadi sasa hakuna kilichobadilishwa katika kanuni, taratibu na sheria?
Je, Kikwete hafahamu kwamba ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kumejaa tuhuma za ufisadi. Hafahamu kwamba kuna madai kuwa mamilioni ya fedha za Watanzania, yamechotwa kinyume cha taratibu? Je, hilo nalo halifahamu?
Kama yote hayo anafahamu, anachotaka kutoka kwa wapinzani wakifikishe vyombo vya dola ni kitu gani hasa? Je, nini ambacho vyombo vya dola havina?
Je, Kikwete hafahamu kwamba kampuni ya Richmond iliyopewa tenda ya kuleta umeme wa dharura imeshindwa kufanya hivyo?
Au hafahamu kwamba, pamoja na Richmond kuuza mkataba wake kwa dada yake Dowans, lakini hadi sasa Dowans nayo, imeshindwa kuzalisha megawati 100 za umeme kama mkataba unavyotaka?
Kilichotarajiwa kutoka kwa Rais Kikwete ni hiki: Kwanza, kuchukua hatua mara moja ya kuwasimamisha kazi watuhumiwa wote na kuviagiza vyombo vya dola kuchunguza.
Katika uchunguzi, ushahidi ukipatikana wahusika wafikishwe mahakamani. Wakisafishwa watarudishwa katika utumishi wa umma.
Pili, kujitenga na marafiki zake; kutofautisha kazi za umma na binfasi. Tatu, kusimama imara kama mkuu wa nchi, na kukemea matendo yote maovu bila kumuangalia huyu ni nani, na alitoa kiasi gani katika kampeni zake za urais.
Kuendelea kung’ang’ania watuhumiwa, na kubaki kupiga mayowe kwamba watuhumu wafikishe ushahidi kwenye vyombo vya dola, hakuwezi kuwasafisha watuhumiwa wala serikali anayoingoza.
Mbona Waziri Mkuu Edward Lowassa aliagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya wanaotuhumiwa kutafuna fedha za umma, wasifikishwe mahakamani na badala yake waletwe makao makuu “kuwekwa benchi?”
Hao wamebainika, kwa ushahidi, kuwa wamekwapua fedha, hawashitakiwi. Je, ushahidi ambao rais anataka wapinzani watoe utatumikaje na utatumiwa na nani?
Sasa Kikwete anapotaka wapinzani wapeleke ushahidi polisi, madai yao polisi, huku akimruhusu Lowassa kubakisha wakurugenzi wanaotuhunmiwa ofisini kwake, anataka kuuleza nini umma wa Watanzania?
Tusema kwamba rais anashirikiana na waziri wake mkuu kulinda wahalifu? Inawezekana ndilo litafanyika hata kama kuna ushahidi dhidi ya watuhumiwa na ufisadi?
Rais akubali iundwe tume huru kuinusuru nchi. Hapo mafisadi watajulikana, watanaswa na watachukuliwa hatua. Hata rais hatahusishwa tena katika genge hilo.
Lakini kwa mwendo wa sasa wa kukemea hata watoa tuhuma ili kuisaidia serikali kujua kinachoendelea, basi rais ataikwamisha nchi kiuchumi na mafisadi watabaki wanachelekea.

Mwisho

No comments: