Wednesday, April 2, 2008

Makamba amemlisha nini Kikwete?



Na Saed Kubenea
JUMAMOSI iliyopita, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, alinukuliwa akitetea chama chake kwamba hakina makundi.

Alisema, “kama mtu anasema ndani ya CCM kuna makundi, muulize yeye yuko kundi lipi.”

Kauli ya Makamba ilikuja siku moja baada ya mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho, Abiud Meregesi, kunukuliwa na vyombo vya habari akisema, “makundi yanaitafuna CCM.”

Kwa hakika, makundi haya yanafahamika kwa kila mmoja, akiwamo Makamba mwenyewe. Hata Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, analifahamu fika jambo hili.

Anajua, kama sote tujuavyo, kwamba kuwapo kwa makundi ndiko kunasababisha wanachama wake kutokuwa wamoja kama ilivyokuwa zamani.

Makamba anajua kuwa makundi hayo yamezalishwa na baadhi ya wanachama na viongozi wao, hasa wale waliokuwa wanashabikia kundi la mtandao.

Hili ndilo kundi lililokiharibu chama hiki kwa kiwango kikubwa. Baadhi ya viongozi wa kundi hili, wakiwamo wale waliokuwa wanafadhili shughuli zake, hawezi kukwepa lawama.

Kwa ujumla, asili ya makundi ya sasa ndani ya CCM ni wanamtandao wa Kikwete, ambao walitafuta na sasa wamepata madaraka makubwa katika chama na serikali.

Kwa hiyo, mgawanyiko wa wana-CCM unajikita katika matokeo ya vitendo vya wafuasi wa kundi hili, ambao walifanikiwa kujenga chuki ya makundi kwa kashfa walizozusha dhidi ya washindani wa Kikwete.

Washindani wa Kikwete wakati huo walikuwa ni pamoja na Dk. Salim Ahmed Salim, Fredrick Sumaye, Pofesa Mark Mwandosya, Dk. Abdallah Kigoda, Iddi Simba na John Malecela.

Haidhuru kama alishiriki moja kwa moja au la. Kikwete anajua waliomfanyia kazi ya kuwagawa wana-CCM. Anajua pia hawakuwagawa kwa hoja za kisera au kiitikadi, bali kwa udaku na ‘kuvuana nguo’ katika vyombo vya habari.

Ajabu ni kwamba Kikwete mwenyewe ameshindwa kumaliza tofauti alizosababisha, na akawateua hata baadhi ya aliowatumia kushika nyadhifa kadhaa, jambo ambalo jamii imeliona kuwa zawadi kwa kazi yao hiyo.

Kwa mfano, wapo waandishi wa habari waliotumiwa na kundi la Kikwete kusambaza na kuhariri habari na picha za washindani wake ili kuwaharibia, huku wakijua kuwa walikuwa wanafanya makosa kitaaluma.

Waandishi walipofukuzwa kazi, Kikwete aliwachukua katika kambi yake ya kampeni, na baada ya uchaguzi aliwapa kazi nono; mmoja katika ofisi ya serikali iliyoongozwa na rafiki yake, na mwingine katika chombo cha habari kinachomilikiwa na rafiki yake.

Kwa hiyo, Kikwete aliwapa zawadi nono kwa kazi hiyo waliyofanya. Kama alifanya hivyo kwa waandishi tu, tutasemaje kwa wanasiasa wenzake ambao amewapenyeza polepole kushika nafasi nyeti katika chama na serikali?

Mazingira hayo ndiyo yamekuza ushindani dhidi yake ndani ya chama kiasi cha makundi nayo kudhamiria kutumia mbinu zilezile walizotumia watu wake, ili kukomoana au hata kumkomoa rais mwenyewe.

Bahati mbaya au nzuri kwake, Makamba alikuwa kwenye kundi la wabomoaji wa wengine – kundi ambalo limempa ulaji alionao. Hivyo, anaposema leo kwamba CCM haina makundi, wenye akili wanatazamana na kujiuliza kama anajua anachokisema na iwapo anajua anaowaambia maneno hayo.

Wanaomfahamu vema Makamba wamekuwa wanamshangaa Kikwete tangu alipompendekeza kuwa Katibu Mkuu wa CCM na kumteua kuwa mbunge. Wanadai nafasi alizopewa zinazidi uwezo wake.

Wanadiriki kusema kwamba hata kauli yake ya sasa kwamba CCM haina makundi, ni ushahidi mwingine wa uwezo mdogo kiuongozi alionao.

Katika kuthibitisha kwamba bado makundi yanakitafuna CCM, katika kikao kimojawapo cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika Dar es Salaam, Agosti mwaka jana, zipo taarifa zinazosema kwamba Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru alikwaruzana waziwazi na Kikwete.

Kilichosababisha mkwaruzano huo ni hatua ya Kingunge kujaribu kushinikiza wajumbe wa CC kukata jina la John Mwankenja, kwa madai kwamba Mwakenja ni “mtu wa Profesa Mark Mwandosya.”

Ukweli unabaki palepale, kwamba makovu yaliyotokana na uchaguzi ndani ya chama hiki bado hayajapona.

Ni Makamba aliyerejea kutoka Mvomero, mkoani Morogoro kusuluhisha makundi ya uchaguzi, na amerejea na tuhuma nyingi kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo, Suleiman Muradi.

Si vema kupuuza kauli ya Maregesi na hata madai kwamba mikasa ya kisiasa iliyomkumba ilitokana na utashi wake wa Frederick Sumaye kuwa mgombea urais.

Lakini kwa kuwa alikuwa na vijikasoro vyake, hivyo hivyo vikatumiwa na makundi yaliyompinga, vikamng’oa kwenye uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM.

Hata hatua iliyochukuliwa dhidi ya Mujuni Kataraiya, aliyekuwa katibu wa CCM wa mkoa wa Mwanza, ilitumia udhaifu wake katika usimamizi wa fedha za chama kuhalalisha nguvu ya makundi yaliyokuwa yanamuwinda kwa sababu hakumuunga mkono Kikwete kwenye kinyang’anyiro.

Ni makundi hayohayo ndiyo yalimdhalilisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Philip Mangula, ambaye alivuliwa wadhifa huo siku Kikwete alipochaguliwa tu kuwa mwenyekiti.

Mangula hakuwa kwenye kundi lake la mtandao. Zipo taarifa za kuaminika kwamba Kikwete aliombwa kumuacha Mangula angalau amalize kipindi chake mwaka jana. Hakukubali.

Makundi hayo ndiyo yalimfuata Mangula hadi Iringa alikokuwa anagombea uenyekiti wa mkoa; yakahakikisha anashindwa.

Kuna madai kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya CCM, Paul Sozigwa, aliondolewa katika nafasi yake kwa kuwa alihisiwa kuwa yeye, Mangula na Ngwilizi walikuwa wanampinga Kikwete, na walikuwa na faili lake chafu wakati wa mchakato, ambalo mwenyekiti Benjamin Mkapa ‘aliogopa’ kulisoma, hivyo halikujadiliwa!

Kikwete na kundi lao walisahau kwamba haikuwa lazima kila mmoja kumuunga mkono Kikwete, na kwamba baada ya kupitishwa, kazi yake kubwa ilikuwa ni kukijenga chama katika umoja wa awali.

Hayo yameshindikana kwa miaka mitatu sasa, na tayari nyufa kubwa zinaanza kutokea, zikiwahusisha hata wastaafu; huku Makamba akiendelea na propaganda zake zinazokuza migawanyiko badala ya kuikomesha.

Katika mazingira ya sasa, kwa haya tunayoona yanatendeka ndani ya CCM, wenye akili watamsikiliza na kumuamini Maregesi kuliko Makamba.

Wala hawatamuuliza Maregesi kundi lake ni lipi. Hawatamuuliza hata Makamba mwenyewe kwa sababu wanajua makundi yao. Hakika baadhi ya kauli za Makamba zinaleta aibu kwake na chama chake.

Mwisho

No comments: