Thursday, February 14, 2008

Ikulu: Richmond ya Rostam


Ikulu: Richmond anaijua Rostam
· Ndiye aliyeileta nchini
· Lowassa alimuingiza

Na Saed Kubenea

KAMPUNI ya Richmond Devolvement Company (RDC), ni mali ya mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, imefahamika.
Taarifa za kuaminika zinamtaja Rostam kuwa kinara mkuu katika Richmond; waziri mkuu “aliyeng’olewa na Bunge,” Edward Lowassa, ‘aliingizwa na mwanasiasa huyo.’
Taarifa kutoka ndani ya Kamati ya Bunge iliyochunguza mkataba kati ya serikali na Richmond zinasema kwamba Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Salva Rweyemamu, ndiye aliyethibitishia Kamati kuhusu kuhusika kwa Rostam na Richmond.
Akizungumza 18 Desemba, 2007 katika kikao cha Kumi na Tano cha Kamati ya Bunge saa 10:23 jioni, Rweyamamu alilithibitishia Bunge kwamba anafahamu kampuni ya Richmond tangu Desemba 2006.
“...Mwaka jana, tuliombwa na watu wa Richmond, tuwasaidie katika ku-menage media katika matatizo yao kama yalivyokuwa na kwa kweli kazi hiyo tuliianza bila mkataba, tukaifanya,” alisema.
Alisema wakati huo ofisi za kampuni hiyo zilikuwa katika jengo la Mkadamu House jijini Dar es Salaam; alitukutanishwa na Gire kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo.
“Mheshimiwa mwenyekiti… our main contact person alikuwa ni mtu mmoja anayeitwa Gire nafikiri ni Mohamed, sina uhakika na jina la kwanza,” Salva alikiambia kikao cha Kamati ya Bunge.
Alisema, “Gire ndiye alikuwa representative wa Richmond hapa Dar es Salaam. … Gire alipewa namba yangu na rafiki yangu Rostam, I have that feeling. Kwa hiyo, baada ya hapo nikawa na-deal na Gire throughout."
Katika ushahidi wake huo uliochapishwa kuanzia ukurasa 955 hadi 964 katika kitabu cha Hansard za Bunge Sehemu ya Tatu, Salva anakiri kwamba Richmond ilikuwa ni kampuni ya kitapeli.
Ushahidi huo wa mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu unathibitisha madai kwamba Richmond haikuwa kampuni ya Marekani, bali kikundi cha watu wa hapa nchini kilichokuwa na lengo la kukamua uchumi wa nchi.
Vilevile ushahidi huo unathibitisha kwamba wakubwa ndani ya serikali, akiwamo waziri mkuu aliyejiuzulu, Lowassa, alijua kila jambo kuhusu Richmond.
“Huu ni ushahidi mkubwa sana na ambao hauwezi kupuuzwa hata kidogo. Kwanza, ni kwa sababu, Salva ni swahiba mkubwa wa Rostam na ni mtu wa ikulu. Ushahidi wake, lazima uwe na ukweli,” alisema mbunge mmoja wa CCM, juzi mjini Dodoma.
Wakati Salva akizungumza hayo, Rostam alikanusha kuifahamua kampuni hiyo, lakini alikiri kwamba alimtambulisha Salva kwa Gire.
“Mimi nawafahamu Dowans, si Richmond. Hawa nawafahamu kwa sababu kampuni yangu ya Caspian inafanya kazi pale,” alisema Rostam mjini Dodoma.
Ushahidi wa Salva katika kamati unavunja minong’ono kwamba Kamati ya Mwakyembe iliwazushia Rostam na Lowassa kuhusu kuifahamu kampuni ya Richmond.
Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu mkataba kati ya serikali na kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond, iliwasilishwa bungeni Jumatano iliyopita na ilianza kujadiliwa Alhamisi, ambapo vigogo watatu wa ngazi ya juu katika serikali waliamua kuachia ngazi.
Vigogo walioachia ngazi ni Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mtangulizi wake, Dk. Ibrahim Msabaha.
Kabla ya kuingia ikulu, Salva alifanya kazi katika kampuni G&S iliyokuwa inajihusisha na ushauri wa habari.
Huko alikuwa pamoja na mwandishi wa habari mwandamizi Gedion Shoo, ambaye kwa mujibu wa Salva bado anaendelea na kazi hiyo mpaka sasa.
“Hivi ninavyozungumza, sifahamu kama G&S wanaendelea na kazi hiyo, kwa sababu formally siko ndani ya G&S, nilijitoa baada ya kuanza shughuli yangu mpya. Siwezi kufanya kazi zote mbili,” anafafanua Salva.
Akibanwa na mjumbe wa Kamati Injinia Stela Manyanya, Salva alisema, “…on one side, the company was not delivering on the other side, unapewa wewe jukumu la kuiambia media kusema hapa, hii delivery itakuja tu subirini wakati huo nchi iko kwenye matatizo makubwa sana. Matatizo ya giza.”
Taarifa zinasema kujiuzulu kwa mawaziri hao kunafuatia shinikizo kubwa lililotokea ndani ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Imeelezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa CC, walikuja juu, wakitaja majina na kushinikiza kwamba wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi unaohusu Richmond na Akaunti ya Fedha za Nje (EPA) waachie ofisi za umma “na bila mjadala.”
Imefahamika kwamba wajumbe waliokuwa wakishinikiza waliongozwa na Abdulrahaman Kinana na makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela.
Bunge katika kikao chake kilichopita, liliunda Kamati teule kuchunguza mkataba kati ya serikali na kampuni ya Richmond.
Kamati hiyo iliongozwa na mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe.

mwisho

No comments: