Monday, October 1, 2007

SAKATA LA ZITTO:

Karamagi amuingiza Kikwete

Serikali yazidi kuanikwa

· Karamagi alisaini mkataba akiwa peke yake
· Ajaribu kumwingiza Rais Kikwete
· Masilingi, Mwakyembe, wambana mbavu
· Mudhihiri alalamika, “Ninatumiwa lakini…”


Na Saed Kubenea

SAKATA la Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi la kusainia mkataba wa madini nje ya nchi, liliibua mtafaruku mkubwa ndani ya Kamati ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limeelezwa.
Wabunge wengi waliopata fursa ya kuchangia, walimbana Karamagi aeleze hasa kilichotokea kuhusiana na kusaini mkataba.
Kikao cha wabunge wa CCM kilifanyika siku mbili baada ya Bunge kumsimamisha Zitto Kabwe kuhudhuria mikutano ya Bunge hadi Januari mwakani. Kabwe ni mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Taarifa kutoka ndani ya kikao zinasema alipoanza kujieleza, Karamagi alionekana kama anayetaka kumhusisha Rais Kikwete, lakini ghafla akakaa kimya.
Hiyo ilikuwa baada ya kuulizwa iwapo Rais Kikwete alikuwa anajua jambo hilo. Hata hivyo baadhi ya wabunge walishikilia kutaka kujua nafasi ya rais katika sakata hilo.
MwanaHALISI limeambiwa kuwa awali, Karamagi alikieleza kikao kuwa alimuanga Rais Kikwete kwamba anakwenda kukutana na wamiliki wa kampuni hiyo.
Hapo ndipo palizua kasheshe. Wabunge walihoji, mara hii kwa kutoa macho, “Je rais alijuajie kama Karamagi alikuwa anakwenda kusaini mkataba wakati alimuanga anakwenda kukutana tu na wamiliki?”
Taarifa zinasema alikuwa ni, Dk. Harisson Mwakyembe, mbunge wa Kyera na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji, aliyesimama na kumtaka Waziri Karamagi kusema ukweli juu ya sakata zima lilivyokuwa.
Gazeti hili limedokezwa kwamba Mwakyembe alisema mbele yawabunge wenzake kuwa Karamagi hajawahi kuiambia kamati yake juu ya kusaini mkataba na yeye, Karamagi hakuzungumzia suala hilo hata katika bajeti ya wizara yake.
“Nje tumelimaliza. Ndani atueleze ilikuwaje? Mimi ni Makamu Mwenyekiti (Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji). Ndani ya kamati yetu hatujui hili. Hajatueleza,” amenukuliwa Mwakyembe akisema.
Taarifa zinasema Mwakyembe alihoji hata uamuzi wa kusainia mkataba huo hotelini badala ya ubalozini.
Alisema hata kama mkataba huo ulisainiwa hotelini kwa bahati mbaya, lakini mbona kuna taarifa kwamba hakukuwa na hata ofisa mmoja wa ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, wakati wa utiaji saini.
Chanzo chetu cha habari kinasema kauli ya Mwakyembe ilitanguliwa na malalamimiko ya Mudhihir Mudhihir, mbunge wa Mchinga, ambaye alimlalamikia Karamagi akisema, “Si mtu mwenye shukurani.”
“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi nimekuwa kinga kwa muda mrefu. Nimekuwa nikilinda chama chetu. Lakini hakuna shukurani. Huu ni uungwana kweli,” alisema mtoa habari akimnukuu Mudhihir.
Chanzo chetu cha habari kinasema Mudhihir alilalama, “Nimechoka kutumika. Huyu Bwana Karamagi kabla ya sijasimama bungeni kumtetea, alikuwa ananipigia simu mara kadhaa na hata kunitembelea nyumbani kwangu.
“Lakini sasa hata nikimpigia simu hapokei. Jamani huu ni uungwana?” aliuliza Mudhihir.
Ni Mudhihir aliyewasilisha hoja ya kumbana Zitto hadi bunge kufikia uamuzi wa kumsimamisha vikao vya bunge hadi Januari mwakani kwa madai ya “kusema uwongo” dhidi ya Karamagi.
Zitto atakuwa akipata nusu mshahara kwa mwezi kwa kipindi chote.
Taarifa za ndani ya kikao cha wabunge wa CCM zinasema, aliyepinga adhabu ya Zitto waziwazi, ni Wilson Masilingi, Mbunge wa Muleba Kusini. Alisema adhabu iliyotolewa haikuwa sahihi.
Masilingi alitoa msimamo huo baada ya makubaliano ya kikao kuwa iundwe “tume” ambayo itapita kwenye vyombo vya habari kutetea hoja ya bunge ya kumfungia Zitto.
MwanaHALISI inazo habari kwamba tume hiyo iliundwa na tayari imeanza kazi. Tume iko chini ya uenyekiti wa Naibu Spika, Anna Makinda.
Habari zinasema wajumbe wengine ni, Wilson Masilingi, Manju Msabya (Kigoma Kusini), Adam Malima (Mkuranga) na Mudhihir Mudhiri (Mchinga).
Hata hivyo, kwa mujibu wa habari hizo, Masilingi alisema kazi ya kuzuia moto wa wananchi itakuwa ngumu kutokana na suala zima kutawaliwa na utata.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wenyewe siujui. Yanayozungumzwa yana wingu zito. Nikiulizwa na waandishi wa habari je, umewahi kuuona huo mkataba unaoutetea, nitasemaje?” alisema mtoa habari akimnukuu Masilingi.
Aliongeza, “Suala limekwenda katika hali ya usiri. Hakuna uwazi, hakuna tunachokijua. Ni usiri juu ya usiri.”
Masilingi ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliwahi pia kuwa Waziri wa Utawala Bora, katika serikali ya Benjamin Mkapa.
Akionyesha kupinga adhabu dhidi ya Zitto, Masilingi alisema, “Kwanza, kilichokuwa mbele ya Bunge ilikuwa ni hoja ya kuunda kamati teule ya Bunge ya kuchunguza mkataba huu. Huwezi kuamua hoja juu ya hoja.”
“Hapa ilikuwa ama kuunda kamati teule au kuliachia suala hili. Lakini badala ya kupiga kura kukata uamuzi wa kuunda kamati, tunapiga kura kumfungia mbunge. Hili si sahihi,” amenukuliwa Masilingi akinasihi wenzake kistaarabu.
Taarifa toka kikaoni zinasema mbunge wa Kahama ambako ndiko uliko mradi huo, James Lembeli, alililamika kwamba hajawahi kuelezwa na Karamagi juu ya kuwapo kwa mradi huo.
Wapo pia baadhi ya wabunge walioonyesha mashaka yao juu ya busara iliyotumika.
Wengi walihoji iwapo suala la mfanyabiashara Reginald Mengi na mbunge wa Mkuranga, Adam Malima liliudiwa tume ya bunge, kwa nini hili limeshindwa kuundiwa tume.
Wachunguzi wa mambo wanasema ni uamuzi wa Kamati ya CCM wa kuunda tume ndio ulisababisha Katibu wa Bunge Damian Foka, kutoa taarifa kwa vyombo vya habari akizuia wananchi na asasi za kijamii kulalamikia maamuzi ya bunge juu ya Zitto.
Lakini kilichowaacha hoi wajumbe wengi, yalikuwa ni majibu ya Karamagi kwa madai ya Mudhihir.
Karamagi alisema ameshindwa kupokea simu za Mudhihir kwa kuwa amebanwa na kazi za kuandaa nyaraka za kikao cha Baraza la Mawaziri, mtoa habari amelieleza gazeti hili.
Majibu haya, hata hivyo, hayakuwafurahisha wabunge wengi. Mmoja wao amenukuliwa akisema “Ni kawaida ya baadhi ya mawaziri kujitia kiburi na hata kubadilisha simu.”
Zitto aliwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza hatua ya waziri Karamagi kusainia mkataba nje ya nchi.
Katika majibu yake bungeni, Karamagi alidai kwamba serikali isingeweza kuacha nafasi ya kusaini mkataba ipotee, ikiwa na maana kwamba wawekezaji huenda wangebadilisha mawazo.
Hoja hiyo, badala ya kuzima moto iliuwasha na kuibua maswali mengine mengi.
Je, ni serikali iliyowaomba wawekezaji hawa kuja nchini na sasa wanaweka masharti kuwa watawekeza tu ikiwa mkataba utasainiwa kabla ya mwisho wa Machi?
Lakini si wawekezaji wenyewe ni Barrick Gold Mines ambao wapo nchini tayari?
Je, si walikuwa wanajua kuwa serikali inapitia upya taratibu za mikataba? Je, walitaka waingie mkataba mpya kwa utaratibu wa zamani?
Je, hata hii juhudi ya serikali "kuwashawishi" wawekezaji hawa kubadilisha vipengele kadhaa vya mikataba hiyo, si itagonga mwamba?
Kwa nini ripoti ya mazingira haikutiliwa maanani? Je, iwapo ikigundulika baadaye kuwa mradi huo ni hatari kwa mazingira, serikali itajinasua vipi kama siyo kwa gharama kubwa au kushindwa hata kuchukua hatua yoyote?
Je, kwa nini Karamagi hakuweza kutoa taarifa yoyote kwa Kamati ya Buge ya Biashara na Uwekezaji juu ya mradi huo tangu Februari iliposaini mkataba hadi alipobanwa mbavu?
MwanaHALISI linaendelea kufuatilia mfumuko wa taarifa juu ya suala hili nyeti.

Mwisho.

No comments: