Monday, October 1, 2007

KIKWETE HAJAMTUMA LOWASSA
Na Saed Kubenea

NIMESOMA kwa makini makala ya Kondo Fuzuge, mmoja wa wachangiaji makala katika gazeti hili, iliyochapishwa katika toleo la MwanaHALISI la wiki iliyopita.
Makala hiyo ilibeba kichwa cha habari kisemacho, “Utendaji wa Lowassa wamkwamisha Kikwete,” ambamo anasema utendaji kazi wa Lowassa ni wa woga au wa kukimbia lawama.
Anasema kila mahali ambapo Lowassa amepata fursa ya kuhutubia mkutano wa ndani au wa hadhara, amesikika akitangulia kusema kwamba ama ametumwa, ameagizwa au ameelekezwa na Rais Jakaya Kikwete kusema yale anayosema.
Hakuna anayemfahamu Lowasa ambaye atabisha kuhusu tabia anayojadili Fuzuge. Hakika ni nadra sana Lowassa kusema bila kudai kwamba ametumwa na Rais Kikwete.
Mifano ipo. Hata katika mambo ya msingi ambayo yameonyeshwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama vile ujenzi wa shule za sekondari na kupambana na umasikini, bado Lowassa atadai ameagizwa na Rais Kikwete.
Bali kwa uzoefu na kadri ninavyomwelewa Rais Kikwete, hawezi kuwa anamwagiza Lowassa kila jambo. Hii ni kwa sababu zifuatazo.
Kwanza, Kikwete anapenda kila mtu afanye kazi aliyopewa kwa mujibu wa maelekezo ya ofisi husika; kanuni, masharti na sheria inayotawala.
Kama Kikwete hawezi kuamini kuwa waziri mkuu anaelewa na ana uwezo wa kufikiri na kutenda bila kuagizwa, hali itakuwaje kwa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na hata Afisa Tawala wilayani?
Ni hivi majuzi tu Kikwete alisisitiza hilo. Katika semina iliyofanyika katika hoteli ya Kunduchi, Dar es Salaam, Kikwete aliwataka viongozi wa wilaya na mikoa kutimiza majukumu yao bila woga; sembuse waziri mkuu.
Kwa msingi huo, hakuna anayeweza kukubali kwamba mambo yote anayofanya Lowassa yametokana na maagizo ya Kikwete; ingawa Kikwete anaweza kuwa na msimamo uleule juu ya yanayotendeka.
Pili, Kikwete hawezi kumtuma Lowassa kuwashambulia wakuu wa wilaya hadharani na kuwaumbua mbele ya wananchi. Hiyo si tabia yake katika TANU na sasa CCM.
Tatu, Kikwete hawezi kumtuma Lowassa kuyakana yaliyofanyika katika awamu iliyopita kwa madai kwamba serikali yake haihusiki nayo.
Katika Tanzania, Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, wanaweza kuchukuliwa kama “mtawala mmoja.”
Kwamba mmoja kamaliza muda wake na kuondoka, hakubadili siasa, sera na mwelekeo wa chama kilekile - CCM. Ndio maana hizi zinaitwa “awamu” tu na siyo tawala za watu tofauti.
Ndiyo maaana hata Kikwete amewahi kusema kwamba serikali yake “haitatazama mambo yaliyopita,” na kufanya uviziaji na ulipizaji visasi, kama ilivyotokea katika nchi jirani za Zambia na Malawi.
Lakini Lowassa, mara baada ya kurejea nchini kutoka Thailand, alikokwenda kutafuta mvua ya “Sumbawanga,” aliwaambia waandishi wa habari kwamba matatizo ya umeme yaliyopo nchini hayakusababishwa na serikali ya sasa, bali yalitokana na serikali iliyopita.
Ninaapa kwamba Kikwete hawezi kumwagiza hili. Hawezi kwa sababu anajua kuwa Lowassa ni Mtanzania, amekuwa akiishi hapa na amekuwa serikalini.
Aidha, Kikwete anajua kwamba mvua ya “Sumbawanga” inaweza kupatikana hatahapa nchini. Hivyo basi, asingeweza kuruhusu mamilioni ya shilingi kutokomea katika mradi ambao huenda ungekuwa mithili ya Richmond au IPTL.
Nne, Kikwete hakumwagiza Lowassa “aagize” kipindupindu kitokomee ndani ya siku saba kutoka jiji la Dar es Salaam. Naapa Kikwete hawezi kutoa amri hiyo au ya aina hiyo kwani anajua mazingira ya jiji hili.
Kikwete anajua kwamba kwa mazingira ya Dar es Salaam, kipindupindu ndio kitafanya jiji hili kuwa makao yake makuu; kitazaa na kujukuu hapahapa.
Tano, Kikwete hawezi kumwagiza Lowassa atoe agizo kwa wananchi kwamba waache kujadili nishati ya umeme na kampuni ya Richmond iliyoshindwa kuleta umeme wa dharura.
Hii ni kwa kuwa licha ya Kikwete kujua kwamba mjadala wa wazi na hata wa siri ni haki ya wananchi wake, anaelewa fika pia kwamba wananchi wameathirika sana kutokana na ukosefu wa umeme.
Aidha, Kikwete anajua kuwa mawaziri wake wa Wizara ya Nishati na Madini, wakiwa wanawasiliana na Lowassa, walimdanganya kuhusu umeme wa Richmond na kumfedhehesha kitaifa na kimataifa.
Sita, Kikwete hakumwambia Lowassa amweleze Reginald Mengi aondoe madai yake dhidi ya mbunge wa Mkuranga, Adam Malima, jambo ambalo Lowassa hajakana mpaka sasa. Hakutumwa na Kikwete!
Saba, Lowassa hataki kujiangalia upya. Hataki kufanana na wale anaowaongoza. Yeye ni amri, vitisho na maagizo kila mahali. Kila anapopita anagombana na watendaji wake, au anamgombanisha rais na wananchi.
Naapa kwamba Rais Kikwete hajamwagiza Lowassa kuwa na tabia hiyo. Hajamtuma!
Mwandishi Fuzuge anahitimisha: “Kwa hiyo, Lowassa anataka kueleweka kwamba anayoyafanya siyo yake, kwa maana kuwa hakuyataka yeye, hakuyafikiria yeye, hakuyaagiza yeye. Kwa ufupi anataka ifahamike kuwa yeye ni mjumbe tu na mjumbe halaumiwi.”
Nakubaliana na Fuzuge. Sikubaliani na Lowassa; na bila shaka Waziri Mkuu Edward Lowassa ana jambo analotaka kuzulia Rais. Tusubiri.

Mwisho

No comments: