Thursday, March 20, 2008

Dk. Nchimbi: Tulia tu!



Na Ndimara Tegambwage

KAMA kuna kiongozi mwenye bahati kubwa ni Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Lakini Nchimbi anataka kuharibu bahati yake. Anataka kujaribu mahakamani na siyo kwenye siasa ambako amefaulu.

Wiki iliyopita alivamia gazeti la Tanzania Daima na kuwatangazia kuwa thamani yake ni Shilingi Bilioni Moja. Nyingi au kidogo?

Aliwaambia kwamba wamemkashifu, hivyo wamwombe radhi, wafute kauli, wamjaze mifuko shilingi bilioni moja, vinginevyo atawaburuza mahakamani.

Nimeona mhariri amemkomalia Nchimbi akisema kwamba hafanyi lolote kati ya yote hayo. Hii ina maana gani? Kwamba Nchimbi atakwenda mahakamani.

Hakuna kesi nzuri ya kusikiliza kama hii. Wazee watajikongoja. Wagonjwa watapelekwa kwenye machela. Wenye ulemavu wa miguu watapewa kila msaada kufika mahakamani kusikiliza kesi hii muhimu na viziwi watapewa mkalimani.

Ni kesi muhimu kwa kuwa inataka kuthibitisha kwamba Mheshimiwa Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, amekashifiwa.

Hoja kuu hapa ni kuthibitisha. Narudia: Kuthibitisha kashfa. Kuthibitisha kuumia. Kuthibitisha kuporomoka kwa mbwembe na dadansi. Hapo ndipo bahati, na siyo heshima, ya Nchimbi itakapopotea. Twende hatua kwa hatua.

Kwanza, Nchimbi aligombea nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) mwaka 2004 na kushinda. Ilikuwa makeke na mbindembinde. Akabebeshwa tuhuma, lawama na shutuma.

Potelea mbali. Tuhuma, lawama na shutuma vikazaa miaka mitano ya uenyekiti, tena bila usumbufu kutoka kwa yeyote aliyekuwa anagombea. Baraka tupu.

Pili, zikaja tuhuma, lawama na shutuma, kwamba anagawa umoja huo kwa kujenga makundi. Si lolote si chochote. Akaukwaa ukuu. Akawa Mkuu wa Wilaya ya Bunda. Amepeta bila mikwara hadi hatua nyingine. Baraka tupu.

Tatu, zikaja tuhuma, lawama na shutuma. Kwamba Nchimbi ni mwanamtandao wa Jakaya Kikwete. Ule mtandao ambao vijana wengi na wazee wasiozeeka walitaka kujitambulisha nao.

Hizi nazo zikawa tuhuma, lawama na shutuma za kheri. Nchimbi akaukwaa ukubwa. Akawa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo. Baraka tele.

Ndipo zikaja tuhuma, lawama na shutuma kuhusu Amina Chifupa aliyetaka kula mfano wa twiga. Alikuwa akitaka kula majani ya juu kabisa ya mti; akitaka kushindana na vigogo wa UVCCM au wateule wa vigogo.

Hilo liliambatana na tuhuma, lawama na shutuma juu ya mahusiano ya Nchimbi na familia ya Mohammed Mpakanjia na hadi kifo cha Amina.

Si lolote si chochote. Ikawa asubuhi, ikawa usiku, siku nyingine iko hapa. Mheshimiwa Dk. Emmanuel Nchimbi akapanda cheo: Naibu Waziri katika moja ya wizara muhimu nchini, Ulinzi.

Mungu akupe nini. Ni katika tuhuma, lawama na shutuma, ambazo Nchimbi anadai kuwa gazeti la Tanzania Daima limezirejea, ndimo amepata ukubwa wa kisiasa.

Kama tuhuma, lawama na shutuma vimezaa neema kwa Nchimbi, haijafahamika vema, yale marejeo tu ya yaliyokuwa yakisemwa yataleta kheri kiasi gani.

Uwaziri kamili? Ubalozi? Makamu wa rais? Kipi kikubwa kinakuja kinachotabiriwa na kumbukumbu za tuhuma, lawama na shutuma za muda mrefu ambazo Nchimbi hajakanusha na bahati nzuri hazijamuathiri – yeye na nafasi yake?

Na hapa ndipo linakuja suala la “mtu wa umma.” Hakuna ambaye amewahi kuongelea mke wa Nchimbi. Lakini hayo ni makosa. Naye mama huyo sharti tujue anaishije na mtu wa umma: Ni mfano mzuri wa maisha au ni kukurukakara?

Hata nyumba ndogo ya waziri siyo siri wala siyo kitu cha binafsi. Hapana. Nyumba hiyo yaweza kumchelewesha kufanya maamuzi; kusahau wajibu; kusaliti nchi; au yaweza kuwa chanzo cha kuwa chapuchapu na hivyo mfano wa kuiga. Kwa nini tusijue?

Mapato ya waziri, ukwasi wake usiolingana na mapato na hata marafiki wake wasiolingana na hadhi ya waziri, siyo mambo ya binafsi wala siri. Sharti wananchi wajue kiongozi wao vema.

Bahati mbaya haya hayajawahi kufanywa na waandishi wa habari wa Tanzania. Wameambiwa ni siri. Wameghilibiwa kuwa ni mambo ya binafsi. Kidogo kinachopenya ndicho hicho wananukuu na ndicho kimemfikisha Nchimbi pale alipo – Naibu waziri wa wizara muhimu sana.

Wapi sasa Nchimbi ameparuriwa? Wapi Nchimbi amepunguziwa hadhi? Iko wapi hadhi iliyomomonyoka kama kila tuhuma, lawama na shutuma vimezaa vyeo na “utukufu wa kisiasa?”

Kesi ya Nchimbi dhidi ya Tanzania Daima yaweza kuwa na mvuto wa karne, hasa pale Nchimbi na mawakili wake watakapokuwa wanajenga msingi wa kuhalalisha “kashfa inayozaa neema.”

Jambo moja ni muhimu sana. Historia itaendelea kurejewa. Kufutika siyo rahisi. Kwa utaratibu wa Nchimbi, vizazi na vizazi vijavyo vitashitakiwa sana na vitatakiwa kutoa zaidi mifukoni.

Bali kuna hukumu moja haifutiki nayo ni hii: Kuna yaliyotokea na yaliyotokea ni hayo yaliyokaririwa na Tanzania Daima. Hii ndiyo hukumu isiyoshindika. Twende mahakamani.

(Mwandishi wa mshauri wa habari katika asasi mbalimbali nchini. Anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments: