Monday, October 1, 2007

MWENYEKITI WA CCM MUNGU MTU



Na Saed Kubenea
UMUNGU-mtu wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaothibitishwa na matukio kadhaa pamoja na nyaraka mbalimbali za chama hicho, umezidi kudhihirika, MwanaHALISI limegundua.

Miongoni mwa matukio muhimu yanayothibitisha kuwa madaraka ya mwenyekiti wa CCM yanafanana na ya Mungu-mtu, ni pamoja na lile la Januari mwaka 1984, ambapo aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi alivuliwa madaraka.

Jumbe aliyekuwa pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar (BLM) na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Taifa, alivuliwa nyadhifa zake zote hizo katika muda wa dakika chache, katika kile ambacho alichokiita binafsi “madaraka makubwa ya mwenyekiti wake.”

Katika kitabu chake alichokipa jina la The Partner-ship (Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, miaka 30 ya dhoruba) ukurasa wa V111, Mzee Jumbe anasema wazi kwamba aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alimvua madaraka ya urais wa Zanzibar kutokana na madaraka makubwa aliyonayo ndani ya chama na serikali kwa ujumla.

Anasema hakuna mjumbe yeyote wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wala Kamati Kuu (CC), aliyepata wasaa wa kuisoma barua yake aliyomuandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mwenyekiti wa chama hicho, ambayo ilikuwa inaelezea kwa undani kasoro za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964.

Badala yake, Mzee Jumbe anasema mwenyekiti alitumia baadhi ya vifungu kwa utashi wake ili kutimiza dhamira yake. “…Bahati mbaya, kabla ya kuitia saini ili apelekewe Rais wa Janhuri ya Muungano, ilitoweka kiajabu na ikaja kuonekana mikononi mwa Mwenyekiti wa CCM (Rais Nyerere) wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC), mjini Dodoma,” anasema Jumbe katika kitabu chake hicho.

“Siku ya mwisho ya kikao cha siku nne, baada ya kuomba nijiuzulu nyadhifa zote nilizokuwa nazo za Makamu Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; Mwenyekiti wa CCM aliueleza mkutano maneno ambayo aliyanukuu katika barua.

“Kabla ya kutoka mkutanoni, nilitoa changamoto kwa mwenyekiti kuisoma barua yote kwa wajumbe wa NEC. Hili halikufanyika. Sehemu ya barua yangu rais aliisoma kwenye NEC kukidhi haja yake. Si Kamati Kuu ya chama au NEC, ama Baraza la Mawaziri wala Baraza la Mapinduzi vilivyopewa nafasi ya kuijadili barua ile.”

Tukio jingine linalobainisha madaraka makubwa ya kupindukia aliyonayo Mwenyekiti wa CCM, ni lile la Mei 3, 2005 ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Benjamin Mkapa alibadili utaratibu wa kura tatu katika uteuzi wa wagombea urais ndani ya chama katika kile kinachoonekana matumizi makubwa ya madaraka ya mwenyekiti katika chama.

Kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya kanuni za uchaguzi wa CCM, pale kunapokuwa na uchaguzi na ikiwa wale wanaotakiwa kuchaguliwa ni zaidi ya mmoja, kura zitapigwa kulingana na idadi ya nafasi zinazotakiwa.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Mkapa alibadilisha utaratibu huo na kuwataka wajumbe wapige kura moja kwa madai kwamba utaratibu huo ungemuonea mmoja wa wagombea.

Kabla ya uamuzi huo, Katibu Mkuu wa CCM (wakati huo), Philip Mangula, alisema utaratibu wa kura tatu ndio halali na unaotambuliwa na kanuni za chama chake.

“Tujiulize, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za CCM, kura zilizowapitisha wagombea Rais Jakaya Kikwete, Dk. Salim Ahmed Salim na Profesa Mark Mwandosya, kuingia katika mkutano mkuu zilikuwa halali? Au zilipatikana kutokana na mwenyekiti kutumia madaraka yake,” alihoji mjumbe wa NEC-CCM aliyetaka asitajwe jina lake.

Mara kadhaa, Mkapa alikuwa anasisitiza kutumia madaraka yake ya uenyekiti kwa kuwaadhibu wale waliokuwa wanaikosoa serikali yake, hasa wabunge. Miongoni mwa wanaoweza kuelezwa kuwa walipambana na madaraka haya, ni mbunge wa Njombe Magharibi, Thomas Nyimbo.

Akiwa ni mmoja wa wabunge waliokuwa wana thubutu ya kuikosoa serikali bungeni, Nyimbo hakupitishwa na chama hicho kugombea tena ubunge kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, katika kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni kutimiza ahadi ya Mkapa, ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Mwingine ni kada wa siku nyingi wa chama hicho, John Shibuda. Mbali na kuzuiwa mara kadhaa kuwania nafasi mbalimbali za juu za uongozi katika chama, mwishoni mwa mwaka 2002 kada huyo alishushwa katika gari moshi mjini Tabora alipokuwa anasafiri kwenda mjini Dodoma kulipokuwa kunafanyika mkutano mkuu wa CCM uliojumuisha pia uchaguzi.

Kauli iliyotoka wakati ule dhidi ya kitendo hicho ni eti alikuwa ana malengo ya kwenda kuwachafua viongozi wa kitaifa wa chama hicho.

Vilevile, mwenyekiti wa sasa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alitumia madaraka yake ya uenyekiti kwa kuvunja Sekretarieti ya chama iliyokuwa chini ya Mangula na kumteua Yusuf Makamba kushika wadhifa wa Katibu Mkuu. Mangula angeweza kuendelea kutumikia wadhifa huo hadi Oktoba mwaka huu wakati wa mkutano mkuu wa CCM akikamilisha kipindi cha pili cha miaka mitano.

Uchambuzi wetu hauzungumzii mtu binafsi (yaani mwenyekiti wa hivi sasa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete), kama baadhi ya watu wanavyofikiri, bali unazungumzia mamlaka ya kiongozi katika taasisi muhimu kama chama cha siasa hiki kikongwe kinachoshika pia hatamu za uongozi wa nchi.

Pamoja na kwamba CCM kupitia kwa mwanasheria wake, Dk. Masumbuko Lamwai, wametangaza nia ya kulishitaki gazeti hili kwa kudaiwa kuwa limeandika habari za kukikashifu chama, viongozi na wanachama wake, mpaka hatua hii barua ya mwanasheria huyo haiku mikononi mwa MwanaHALISI licha ya kuwa imenukuliwa na gazeti la CCM, Uhuru.

Dk. Lamwai kwa niaba ya chama chake, anadai habari iliyochapishwa na gazeti hili, toleo namba 041 la Jumatano, Aprili 25-Mei 1, mwaka huu, chini ya kichwa kisemacho “Mwenyekiti Taifa CCM mungu-mtu,” imekichafua chama hicho.

Wakati CCM ikitoa tishio hilo, siku moja baadaye Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), ilitoa tamko linalotishia gazeti hili kuchukuliwa hatua kali kwa kutajwa kuwa linaandika habari za kukashifu viongozi wa serikali.

Hatua yenyewe ya Serikali kutoa tamko ililoliita ni la ONYO KALI, inashangaza kwa sababu kabla yake, Mhariri Mtendaji wa MwanaHALISI, Saed Kubenea, aliitwa ofisini MAELEZO na kuelezwa na Mpenda kuwa anahitaji kubadilishana naye mawazo na wala si kwa kuwa gazeti analoliongoza linahusika na kukashifu viongozi wa Serikali.

Gazeti hili limeunganishwa na Tanzania Daima kuelezwa kwa pamoja kuwa yamekuwa ya mwenendo wa kuandika habari zinazowakashifu viongozi, hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Mwisho.

1 comment:

Anonymous said...

BLOG yako ni nzuuuri imetulia sana. HONGERA